• HABARI MPYA

  Jumanne, Mei 29, 2012

  BOBAN AWEKEWA MASHINE YE ECG KIFUANI


  MSHAMBULIAJI wa Taifa Stars na Simba, Haruna Moshi Boban, amefanyiwa uchunguzi wa kiafya na kuwekewa kifaa maalumu kifuani.
  Gazeti la Mwanaspoti leo limeandika kwamba Boban ambaye ni Nahodha Msaidizi wa Simba, aliwekewa kifaa hicho kwa muda wa dakika 24 kutokana na kusumbuliwa na tatizo la presha ya kushuka iliyogunduliwa na daktari wa Simba hivi karibuni.
  Daktari wa Stars, Mwanandi Mwankemwa, ameliambia Mwanaspoti akisema: "Kutokana na tatizo la kuzimia lililomkuta Boban alipokuwa Kinshasa.
  Tumemwekea mashine maalum kwenye moyo katika sehemu ya kifuani, hii ni kwa ajili ya kuchunguza moyo wake kama una tatizo.
  "Kifaa hicho kinaitwa ECG na hufanya kazi sawa na mishipa ya moyo (PQ Waves) na atakaa nacho kwa muda wa masaa 24."
  Kifaa hicho aliwekewa juzi Alhamisi saa nne asubuhi na kiliondolewa jana Ijumaa muda huo.
  Mwanandi amesema, katika muda huo, mashine hiyo itagundua kama kuna tatizo lolote kwa mchezaji huyo.
  Akiwa na kifaa hicho, Boban alishindwa kufanya mazoezi na Taifa Stars na kuungana na Nurdin Bakari ambaye anasumbuliwa na nyama za paja.
  Nurdin amepewa siku saba kwa ajili ya mapumziko na Thomas Ulimwengu ambaye anasumbuliwa na kifundo cha mguu wa kulia, alifanya mazoezi mepesi.
  Mwanandi ameeleza kuwa suala la Boban kuchezea Stars litategemea majibu ya mashine hiyo.
  Lakini jana Ijumaa mchana, Mwankemwa alipoulizwa alisema wanasubiri majibu ya kipimo hicho kutoka kwa madaktari bingwa wa Hospitali ya Hindu Mandal.
  Akizungumzia suala hilo, Boban alisema: "Hali yangu kiafya ni nzuri, sijisikii tatizo lolote, zaidi ya mkono huu unaonisumbua (anaonyesha katika mkono wake wa kulia ambao una uvimbe kwenye kidole cha kati).
  Stars inajipima nguvu na Malawi leo Jumamosi ili kujiandaa na mechi dhidi ya Ivory Coast ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia.
  Boban alizidiwa alipokuwa Kinshasa akijiandaa kurudi Dar es Salaam baada ya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa kiungo wa Simba, Patrick Mafisango. Yeye na Mafisango walikuwa marafiki wa karibu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BOBAN AWEKEWA MASHINE YE ECG KIFUANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top