• HABARI MPYA

  Jumamosi, Mei 26, 2012

  VAN BASTEN MPACHIKA MABAO AMBAYE HAJATOKEA KAMA YEYE EURO


  Van Basten

  UNAPOMTAJA Marcel ‘Marco’ van Basten, unamaanisha mmoja wa wachezaji waliowahi kung’ara na timu ya taifa ya Uholanzi, ambaye hadi leo bado anaheshimika katika kizazi cha zama za kati za soka la kuvutia la nchi hiyo.
  Van Basten alizaliwa Oktoba 31, 1964 mjini Utrecht, Uholanzi na kuanza kusakata soka kwenye timu ya mtaani kwao ya EDO, alipokuwa na umri wa miaka saba na mwaka uliofuata akahamia UVV Utrecht, alikodumu kwa miaka 10 kabla hajacheza kwa muda kwenye klabu ya Elinkwijk.
  Amejijengea heshima kuwa mmoja wa washambuliaji wakali zaidi wa Uholanzi, akiwa mchezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo miaka ya 1980 na mwanzoni mwa 1990, akiwa pia mchezaji wa AFC Ajax na AC Milan, ambaye sasa ni kocha.
  Amepachika nyavuni mabao 277 akiwa kwenye soka la juu, huku akikutwa mara kwa mara na majeraha yaliyokuwa yakimkabili. Baadaye alikuwa kocha wa AFC Ajax na timu ya taifa.
  Akicheza soka la kiufundi na mashuti makali, van Basten alitajwa kuwa mwanasoka bora wa Ulaya kwa miaka mitatu (1988, 1989 na 1992) na mwaka 1992 akawa mwanasoka bora wa dunia.
  Kwenye upigaji kura kumsaka mwanasoka bora wa karne ulioendeshwa na gazeti moja la Ufaransa, van Basten alikamata nafasi ya 25 huku akiwa nafasi ya nane kwa nchi hiyo.
  Machi 2007, Sky Sports ilimtangaza van Basten kama mwanasoka bora namba moja miongoni mwa waliolazimika kuachana na soka mapema.
  Alisajiliwa na AFC Ajax msimu wa 1981–82 na alicheza mechi ya kwanza na timu hiyo Aprili 1982 na kufunga bao lake la kwanza kwenye ushindi wa mabao 5–0 dhidi ya NEC.
  Alicheza mashindano ya Ulaya msimu wa 1982–83, akipambana na mfungaji bora wa Ulaya wakati huo, Wim Kieft, kwenye nafasi ya ushambuliaji na kufunga mabao tisa kwenye mechi 20 za ligi. Kieft alihama msimu uliofuata na kumwachia namba ya kudumu van Basten.
  Van Basten
  Alikuwa mfungaji bora wa ligi kuanzia msimu wa 1983–84 hadi 1986–87, akifunga mabao 117 kwenye mechi 112. Msimu wa 1985–86 aliweka kimiani mabao 37 kwenye mechi 26 za ligi, ikiwa ni pamoja na mabao sita ya mechi dhidi ya Sparta Rotterdam na matano dhidi ya Heracles Almelo na kushinda kiatu cha dhahabu cha Ulaya. Pia alifunga bao la ushindi kwenye fainali ya Kombe la Washindi Ulaya kwenye mechi dhidi ya Lokomotive Leipzig mwaka 1987.
  Mwaka 1988, Silvio Berlusconi wa AC Milan alimsajili pamoja na magwiji Ruud Gullit na Frank Rijkaard. Katika msimu wa kwanza, Milan ilishinda kombe la Scudetto baada ya miaka nane, lakini van Basten, akisumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu, alicheza mechi 11 tu.
  Msimu wa 1988–89, van Basten alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya akiwa maefunga mabao 19 kwenye Serie A na mawili kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Ulaya (Klabu Bingwa) dhidi ya Steaua Bucureşti.
  Msimu uliofuata aliongoza tena ufungaji kwenye Serie A na kuisaidia Milan kutetea taji la Ulaya kwa kuichapa SL Benfica kwenye mechi ya fainali, lakini ikapokonywa taji la Italia, Scudetto na Sampdoria msimu uliofuata.
  Baada ya van Basten kukosana na kocha Arrigo Sacchi, Berlusconi akamtimua kocha huyo na kumpa kazi Fabio Capello msimu uliofuata na kuifanya Milan imalize ligi bila kufungwa, huku van Basten akifunga mabao 25 na kuipa taji la Italia timu hiyo na yeye kuwa mwanasoka bora tena.
  Novemba 1992, alikuwa mchezaji wa kwanza kupachika mabao manne kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa siku walipopambana na IFK Göteborg ya Sweden.
  Timu hiyo iliendeleza rekodi ya kutofungwa msimu wa 1992–93 na kucheza mechi 58 zaidi kabla ya kupata kichapo cha kwanza. Soka la van Basten lilikuwa la hali ya juu msimu huo na kupata tena uanasoka bora wa Ulaya, hivyo kufikia rekodi ya magwiji, Johan Cruyff na Michel Platini kushinda tuzo hilo mara tatu.
  Tatizo la kifundo cha mguu lilirejea tena wakati wa mechi dhidi ya AC Ancona na kumlazimisha kurejea kwenye mlolongo wa upasuaji. Alirejea kwenye mechi chache za mwisho wa msimu kabla Milan haijalitema taji la Ulaya kwa Olympique de Marseille.
  Mechi hiyo ya fainali ilikuwa ya mwisho kwake kuchezea klabu hiyo ya Italia. Miaka miwili iliyofuata ilikuwa ni ya kusaka kurejea kwenye fomu, lakini hatimaye akatangaza kustaafu mwaka 1995, akiwa na umri wa miaka 30 tu.
  Baada ya hapo alicheza soka ‘la ukubwani’ wakati wa mechi ya maonyesho ya Demetrio Albertini kwenye Uwanja wa San Siro, Machi 2006 na kufunga bao la kichwa kabla ya kutolewa mwanzoni mwa kipindi hicho cha kwanza.
  Julai 22, 2006, alicheza mechi ya maonyesho wakati wa kuadhimisha miaka 11 ya Dennis Bergkamp akiwa Arsenal, na hii ilikuwa ndio mechi ya kwanza kuchezwa kwenye Uwanja wa Emirates, akichezea upande wa maveterani wa Ajax. Aliingia kipindi cha pili akiwa na Johan Cruyff.
  Pamoja na umwamba wake uwanjani, akiwa amewahi kuifunga England kwa ‘hat-trick’, akiifunga pia Ujerumani na Urusi wakati huo mabao yote yakiwa ya ushindi kwa nchi yake kwenye mashindano ya kimataifa, lakini van Basten hakuwahi hata mara moja kufunga bao kwenye fainali za Kombe la Dunia.
  Katika nusu fainali ya Euro 1992, Uholanzi ilipoteza mechi kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Denmark, huku Peter Schmeichel akipangua shuti la penalti la van Basten.
  Baadaye alianza kazi ya ukocha, ingawa alipostaafu mwaka 1995 alisema asingethubutu kugeukia ukocha. Lakini baadaye alisomea kazi hiyo kwenye chuo cha Royal Dutch Football Association (KNVB) na akaanza kazi akiwa msaidizi wa mchezaji mwenzake wa zamani, John van't Schip kwenye timu ya pili ya AFC Ajax mwaka 2003–04. Julai 2004 akatajwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Uholanza, akisaidiwa na van't Schip.
  Alianza kuonyesha misimamo mikali kama bosi kwa kuwatema wachezaji wenye majina makubwa kama Clarence Seedorf, Patrick Kluivert, Edgar Davids na Roy Makaay, huku akimweka benchi Mark van Bommel, kwa madai kuwa ama wamepitwa na wakati au wameshindwa kuisaidia timu ya taifa.
  Na huenda kwa mara ya kwanza ndani ya miongo kadhaa, hakuna mchezaji tegemeo kwenye timu ya taifa aliyeitwa kutoka klabu tatu kubwa; AFC Ajax, PSV na Feyenoord huku akitaka kumwita mshambuliaji Salomon Kalou, lakini mamlaka za uhamiaji zikamnyima uraia wa Uholanzi kabla Kalou hajakubali wito wa nchi yake, Ivory Coast.
  Ingawa ilitinga fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006 bila kufungwa, Uholanzi ilijikuta ikichapwa bao 1–0 na Ureno na kutupwa nje wakati wa mtoano, kisha van Basten kukosolewa kwa kumwacha Ruud van Nistelrooy (aliyeifungia Uholanzi mabao 28) kabla ya mechi hiyo, na kumchukua Dirk Kuyt ambaye hakufunga hata bao moja kwenye mashindano hayo.
  Ingawa maofisa wa soka walitaka van Basten aiongoze timu ya taifa hadi wakati wa kusaka tiketi ya kwenda Afrika Kusini, mwenyewe aliingia mkataba wa miaka minne na AFC Ajax Februari mwaka 2008, lakini ikiwa ni baada ya kuiongoza Uholanzi kwenye Euro 2008 na kufungwa robo fainali na Russia ya Guus Hiddink. Aliachana na Ajax Mei 2009, baada ya timu hiyo kushindwa kupata nafasi ya Ligi ya Mabingwa.

  WASIFU WAKE:
  JINA: Marcel van Basten
  KUZALIWA: 31 Oktoba 1964 (1964-10-31) (age 46)
  ALIPOZALIWA: Utrecht, Netherlands
  KLABU ALIZOCHEZEA:
  Mwaka       Klabu
  1982–1987           Ajax (Mechi 133, mabao 128)
  1987–1993           AC Milan (Mechi 147, maba 90)
  (Tangu 1983 hadi 1992, aliichezea Uholanzi mechi 58 na kuifungia mabao 24) 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: VAN BASTEN MPACHIKA MABAO AMBAYE HAJATOKEA KAMA YEYE EURO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top