• HABARI MPYA

  Jumapili, Mei 27, 2012

  KILA LA HERI TWIGA STARS ADDIS LEO


  Twiga Stars


  TIMU ya taifa ya soka ya wanawake Tanzania, Twiga Stars leo inatarajiwa kushuka dimbani kwenye Uwanja wa Addis Ababa, Ethiopia kumenyana na wenyeji Ethiopia katika mechi ya kwanza ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake.
  Twiga iliyoondoka nchini Alhamisi na msafara wa watu 24 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi itacheza na Ethiopia, imepania kufanya vizuri leo, ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kufuzu kwenye Fainali hizo za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu, Equatorial Guinea.
  Baada ya mechi ya leo, Addis Ababa, timu hizo zitarudiana Juni 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Twiga Stars ikifanikiwa kuitoa Ethiopia itakuwa imepeta tiketi ya kwenda Equatorial Guinea.
  Wachezaji waliopo Addis na kikosi cha Twiga ni Amina Ally, Asha Rashid (nahodha), Esther Chabruma, Ettoe Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fadhila Hamad, Fatuma Bashiri, Fatuma Khatib, Fatuma Mustafa, Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwanahamisi Omari, Mwanaidi Tamba, Mwapewa Mtumwa, Rukia Hamis, Semeni Abeid na Zena Khamis.
  Kwa upande wa Benchi la Ufundi ni Charles Mkwasa (Kocha Mkuu), Nasra Mohamed (Kocha Msaidizi), Furaha Francis (Meneja wa Timu), Mwanahamisi Abdallah (Mtunza Vifaa) na Christina Luambano (Daktari wa Timu).
  Twiga Stars ambayo, Mkuu wake wa msafara huko ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka ya Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la SokaTanzania (TFF) itarejea nyumbani Mei 28 mwaka huu saa 6 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines.
  Katika mechi mbili za kujipima nguvu kabla ya mchezo huo, Twiga ilifungwa 4-1 na Zimbabwe na 5-2 na Afrika Kusini, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini makocha wameahidi kufanyia kazi mapungufu na kusema Watanzania watarajie matokeo mazuri leo. 
  Mungu ibariki Twiga Stars. Ibariki Tanzania. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KILA LA HERI TWIGA STARS ADDIS LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top