• HABARI MPYA

  Wednesday, May 30, 2012

  ANAYOTAKA MANJI, SIJUI KAMA YATATEKELEZWA, LAKINI...


  Na Mahmoud Zubeiry

  KATIKA mada yangu iliyopita nilisema, mustakabali wa klabu ya Yanga utazamwe upya kufuatia, Mwenyekiti wake, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga kujiuzulu, baada ya vita kubwa aliyokuwa akipigwa na wapinzani wake.
  Bado naendelea kusistiza; Nchunga anastahili sifa, ameonyesha yeye ni Yanga damu. Si mroho wa madaraka. Ni mtu aliyeweka maslahi ya Yanga mbele. Huyu ni mfano wa kuigwa. Lakini baada ya Nchunga kujiuzulu, pamoja na kwamba mfanyabiashara Yussuf Manji ameahidi kuihudumia timu kwa mwaka mmoja, bado ipo haja sasa ya mustakabali wa klabu hiyo kutazamwa upya.
  Nilisema mustakabali wa klabu kutazamwa upya, kwa sababu imeonekana ni vigumu mno Katiba kumlinda kiongozi aliye madarakani, iwapo kundi fulani litaamua kwa dhati kuingia msituni kumng’oa.
  Nilitoa mfano vita aliyopigwa Nchunga- ilikuwa kali na ikafikia lazima aondoke kwa maslahi ya klabu. Alitengenezewa zengwe zito. Alipigwa kila upande- hakuwa na namna yoyote zaidi ya kujinasua.
  Walioongoza mapambano dhidi ya Nchunga, akina Ibrahim Akilimali, Bakili Makele na wengine- ni wale wale ambao kwa zaidi ya miaka 10 wamekuwa mstari wa mbele katika vurugu na migogoro kwenye klabu hiyo.
  Kumbukumbu zipo, Bakili na Akilimali walishiriki kikamilifu kumng’oa Mzee Rashid Ngozoma Matunda mwaka 1999 na hawa hawa walimtia kashikashi nzito Wakili Imani Omar Madega, ingawa huyo walimshindwa.
  Sioni kwa sababu gani hawa watakoma kwa mtu mwingine yeyote atakayekuja baada ya Nchunga, kwa sababu wamekwishazoea. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kutoa mfano mmoja enzi za uhai wake kuhusu ubaguzi.
  Alisema dhambi ya ubaguzi ni sawa na dhambi ya kula nyama ya mtu, ukishakula nyuma ya mtu, hutaacha utaendelea kula.
  Naweza kuuleta mfano huu katika hii desturi ya mapinduzi kwenye klabu ya Yanga- naona kuna dalili za kutosha itaendelea tu hata ije katiba ya aina gani.
  Tena watu hawa wamepiga hatua kubwa, kiasi cha kuona bora Yanga ife, lakini kiongozi fulani ang’oke madarakani. Inasikitisha.
  Mapendekezo ya Manji kuhusu mabadiliko ya Katiba hata yafanyiwe kazi- lakini kuna uwezekano likaibuka kundi la kumpinga na kupambana naye kikamilifu. Hiyo ndio tabia ya Yanga.
  Kwa ‘uhuni’ aliofanyiwa Nchunga, hakuna hakika kama atatokea mtu mwingine mwenye hekima na kujiheshimu kufikiria kuongoza Yanga- inatia woga. Lakini kwa nini ifikie huko, kweli tutegemee kuiona Yanga bora na ya kisasa bila mtu mwenye hekima na upeo mkubwa?
  Ndipo hapo unapoonekana umuhimu wa mustakabali wa Yanga kutazamwa upya- kwa sababu wapo watu, kila sekunde ya maisha yao inaitegemea klabu hiyo. Watu hao ukiwatazama sura zao, wako tayari hata kuua mtu, anayekuja na sera za kutaka kuwatoa Yanga.
  Jamal Malinzi alikiona cha moto, tu kwa kutaka fedha za klabu zinapoingia ziende moja kwa moja benki- makomandoo walianza kumpiga vita tangu hapo hadi akang’oka.
  Hii haitaisha na wala asijidanganye mtu eti atakuja kukaa Yanga kwa raha, hata siku moja! Manji mwenyewe ameshatukanwa sana na wavaa ndala- yaani upo umuhimu wa mustakabali wa klabu hiyo kutazamwa upya.
  TFF imeagiza uchaguzi ufanyike Julai kujaza nafasi za wajumbe waliojiuzulu, akiwemo Mwenyekiti- vema, lakini kutokea hapo nini mustakabali wa klabu? Hilo ndilo suala ambalo kila mwana Yanga anapaswa kujiuliza kwa sasa.
  Naposema wana Yanga, siwahusishi wale ambao wanategemea klabu ili kulisha familia zao, na kwa ujumla kuendesha maisha yao. Hao si wana Yanga, kwa sababu mwana Yanga mzuri ni yule ambaye anafikiria ataifanyia nini klabu, si klabu imfanyie nini yeye.
  Manji ana mapendekezo yake ya Katiba, ambayo anataka yafanyiwe kazi na uongozi utakaoingia madarakani Julai- sidhani kama matakwa ya Manji yatatekelezwa na kiongozi yeyote.
  Hatari ambayo kiongozi yeyote wa Yanga anatakiwa kuiepuka ni kupitisha Katiba ambayo mwisho wa siku, itaiondoa timu kuwa mali ya wanananchi na kuwa mali ya mtu mmoja- kwa namna yoyote ile, kwani kufanya hivyo itakuwa sawa na kuiuza klabu.
  Lakini upo umuhimu sasa wa Yanga kuendana na mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa klabu hiyo- kwa kutangaza tenda za kuiendesha klabu na watu kuingia mikataba na uongozi wa klabu, kuimiliki timu kwa muda fulani.
  Kwa sasa Yanga inapata nini kwa mwaka? Sijui zaidi ya kelele za madeni lukuki. Uongozi utakaoingia madarakani, utangaze tenda ya kuikabidhi klabu kwa kampuni au mtu, kwa dau mathalani la Sh. Milioni 500 kwa miaka mitatu.
  Nitafafanua. Kwa mfano Rostam Aziz anaamua kuilipa Yanga Milioni 500, anapewa mkataba wa kuimiliki klabu kwa muda wa miaka mitatu. Atasajili timu, atalipa mishahara, ataingia mikataba ya udhamini ya miaka mitatu, lakini Yanga itabaki kuwa vile vile na asili yake.
  Mkataba utampa masharti muwekezaji, ambayo asipoyatimiza atatakiwa kuiachia timu, apewe mtu mwingine- mfano kuhakikisha waajiriwa wote wanalipwa kwa wakati, matokeo mazuri na kutokiuka miiko na asili ya klabu.
  Wapo watu wana uwezo wa kujitokeza kuchukua dili hiyo- na Yanga itanufaika mno. Kwa sasa Yanga haiingizi chochote- lakini vipi ikiwa haiingii gharama yoyote na kila baada ya miaka mitatu, akaunti yake inapotokea Milioni 500?
  Fedha hizo zinaweza kutumika kwa miradi mingine ya maendeleo ya klabu, kama ujenzi wa Uwanja na kadhalika, wakati mtu aliyeingia mkataba wa kumiliki klabu, naye anatengeneza fedha nzuri kutokana na mikataba ya udhamini, mauzo ya bidhaa zenye nembo ya klabu, mapato ya milangoni, mauzo ya wachezaji na kadhalika, ikiwemo zawadi za mashindano.
  Hayo ni mawazo yangu, lakini najua wapo wengine wana mawazo mazuri katika kuijenga Yanga isiyo na migogoro na yenye manufaa, itakayokuwa inawapa faraja mashabiki wake. Hoja ni kuutazama upya mustakabali wa klabu. Nawasilisha.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ANAYOTAKA MANJI, SIJUI KAMA YATATEKELEZWA, LAKINI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top