• HABARI MPYA

  Jumamosi, Mei 26, 2012

  STRIKER LA TAIFA STARS LAKUBALI KUTUA YANGA

  Javu akimtoka Ramadhani Chombo katika mazoezi ya timu ya taifa

  MSHAMBULIAJI Hussein Javu ameweka wazi kuwa yupo tayari kuichezea Yanga lakini akasisitiza ana mkataba wa miaka miwili na Mtibwa Sugar.
  Javu, ambaye alikuwa kwenye kikosi cha Jan Poulsen aliyemaliza mkataba wa kuinoa timu ya taifa, Taifa Stars, ameachwa na kocha mpya Kim Poulsen, ambaye alitangaza kikosi chake hivi karibuni.
  Gazeti la Mwanaspoti limeandika leo kwamba, lilifanya mahojiano na mchezaji huyo jana Jumatatu mjini Dar es Salaam na akasema; "Itategemea makubaliano ya uongozi pande zote mbili, wakikubaliana mimi sina la kupinga juu ya hilo,"
  "Najua Yanga ni klabu kubwa na yenye mashabiki wengi tofauti na ilivyo Mtibwa," alisema mshambuliaji huyo mwenye mabao sita kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara iliyofika kikomo Mei 6, mwaka huu kwa Simba kutwaa taji hilo.
  Alisema kuchezea Yanga ni changamoto kubwa kwake kujijenga kisoka zaidi na kujifunza mengi kutoka kwa wachezaji wenzake tofauti na ilivyo kwa Mtibwa Sugar ya Turiani Morogoro.
  Mwanaspoti linajua Javu na Said Bahanuzi wa Mtibwa ni miongoni mwa washambuliaji wanaopewa kipaumbele kusajiliwa na Yanga kwa msimu ujao na kukata kiu ya mabao kwa mabingwa hao watetezi wa Kombe la Kagame.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: STRIKER LA TAIFA STARS LAKUBALI KUTUA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top