• HABARI MPYA

  Thursday, May 24, 2012

  BREAKING NEWS: NCHUNGA AJIUZULU YANGA BAADA YA KUVAMIWA USIKU WA MANANE NYUMBANI KWAKE  Nchunga akitangaza kujiuzulu leo jioni hii ofisini kwake
  MWENYEKITI wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ametangaza kujiuzulu wadhifa wake jioni hii ofisini kwake, jengo la NSSF, barabara ya Bibi Biti, Dar es Salaam, siku moja baada ya kuvamiwa na kundi la watu nyumbani kwake, Mbezi, Jijini usiku wa wa manane.
  Hata hivyo, Nchunga amekataa kulihusisha tukio la kuvamiwa kwake usiku wa jana na kujiuzulu kwake, akisema kwamba amefikia uamuzi huo kuinusuru Yanga, kwa sababu wapo watu wako tayari Yanga ife, lakini wamng'oe yeye madarakani, kitu ambacho yeye hapendi kitokee.
  Nchunga alisema kwamba majira ya saa nane usiku wa jana, alivamiwa na kundi la watu takribani 15, lakini hawakufanikiwa kufanya chochote kutokana na ulinzi mkali uliopo katika nnyumba hiyo.
  "Kwanza mbwa walianza kubweka, walinzi wakashituka wakaomba msaada kwa walinzi wenzao, nasi tukapuga simu polisi, wakaja haraka sana na kukuta watu hao wamekwishakimbia,"alisema


  TAARIFA YA KUJIUZULU KWA NCHUNGA:  LLOYD NCHUNGA BIHARAGU
  C/O LLOYD ADVOCATES,
  Morogoro/Bibi TIti  Mohamed Rd,7th Floor, J.K. Nyerere Pension towers
  P.BOX 75111, Dar-Es- Salaam,Tanzania.


                                                                     

  TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUJIUZULU NAFASI YA UENYEKITI WA KLAB YA YANGA.
  Ndugu wana Habari, najua kwamba taarifa hii itawafedhehesha wajumbe na wanayanga wanaotuunga mkono,hasa ukizingatia maamuzi ya pamoja ya vikao vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita kwamba hakuna wa kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu ambao tulipanga ufanyike tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo la kujiuzulu linalotolewa na baadhi ya wazee na wanaojiita vijana wa klab, kwa wajumbe wa kamati ya utendaji, na hasa mimi kama mwenyekiti.
  Nawashukuru wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote tulikuwa tunawajibika nayo.
  Tangu tumeingia madarakani tumeweza kushirikiana na kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja, yaani; Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2010/2011, na Ubingwa wa  Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tuliuwa uteja kwa watani wetu wa jadi kila tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya tarehe 6 Mei 2012, ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa katika klab yetu.
  Hali kadhalika tumeshirikiana  mpaka tumeweza kuboresha mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium Lager, tumeingia mkataba na  kampuni ya NEDCO  kuendeleza mali zetu katika mtaa wa mafia na uwanja wetu wa KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata hati miliki za maeneo yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua za mwisho za kumalizia michoro.
  Hali kadhalika tuliingia mkataba wa kuzalisha na kuuza bidhaa zenye nembo yetu na hasa baada ya kufanya marekebisho yatokanayo na matakwa ya sheria kule BRELA na pia mkataba na kampuni ya NEXUS LTD, ambayo itakuwa inatutafutia wadhamini wa nje na ndani, kufanya promosheni zetu na kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali na kukusanya data za wanachama na kusajili  wapya tukiwa na malengo ya kukusanya shilingi 300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu. Haya yote tuliyafanya tukilenga kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja.
  Kwa ridhaa yenu tumekua tukiendelea na mazungumzo na makampuni mbali mbali kwa ajili ya udhamini na kwa sababu maalum, nitazitaja katika hati ya makabidhiano kwa kiongozi ajaye.
  Aidha, tumeshirikiana katika kufanya mambo mbali mbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na sikukuu ya kuadhimisha miaka 77 ya Yanga, sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na waliokumbwa na maafa, na kongamano la vijana lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika Yanga ikiwa ni pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya Yanga, ambapo maombi yapo kwa msajili Manispaa ya Ilala.
  Haya yote nayataja ikiwa ni kuwashukuru kwa ushirikiano na ikiwezekana muweze kuyakamilisha yaliyobaki ambayo mtaona yalikuwa mazuri.
  Lakini pia tulipopata matatizo tulikuwa pamoja.  Nichelee kusema tu kwamba tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu Makamu Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe wetu  ndugu Seif A. Seif, Ali Mayayi, na wengineo, kwani tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika suala la kujiuzulu ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili mkuu ambaye sasa ameonyesha nia ya kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali, tulitumia kila jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana.
  Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani wetu goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa.
  Ninachokiona mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia. SIWATUHUMU WACHEZAJI MOJA KWA MOJA, isipokuwa  mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa, inaonyesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza kuubaini mapema.
  Sioni mantiki katika hoja kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k.  Au ati mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo  tuvune bao 5!
  Kwa wanaoijua Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji walicheza kwa morali.
  Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia.
  Baada ya mapinduzi kushindikana na TFF kuonya kuhusu mapinduzi hayo, wazee kupitia msemaji wao , Mzee Akilimali wamesikika katika kipindi cha Michezo  cha Redio moja maarufu hapa nchini wakidai kwamba ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea kuongoza!
  Hii imenikumbusha HEKMA ZA MFALME SELEMANI akiamulia ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wamgawane nusu kwa nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko kumkata nusu.
  Kwa hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti  wa Yanga kwani ni klab ninayoipenda hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba yetu.
  Vile vile siko tayari kuona klab yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi.
  Natumaini kamati ya utendaji kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa  mafanikio zaidi.
   Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na nikiwa  na uwezo wa kufanya hivyo.
  YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO.
  Wasalaam,


  LLOYD NCHUNGA BIHARAGU.

  Nakala kwa:-
  Mama Fatma Karume,Mdhamini
  Francis Kifukwe, Mdhamini
  Bwana Yusuf Manji – Kwa taarifa


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BREAKING NEWS: NCHUNGA AJIUZULU YANGA BAADA YA KUVAMIWA USIKU WA MANANE NYUMBANI KWAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top