• HABARI MPYA

  Friday, May 25, 2012

  KIKAO CHA KAMATI YA MGONGOLWA CHAMALIZIKA, HALI BADO TETE YANGA


  MWENYEKITI wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alex Mgongolwa (pichani kulia) amesema katika kikao chao cha jioni ya leo, wameshindwa kuamini kwamba Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Llod Baharagu Nchunga  amejiuzulu na wameomba uthibitisho kutoka kwa sekretarieti ya klabu hiyo, ili wachukue hatua zaidi katika kutatua mgogoro unaoendelea kwenye klabu hiyo.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY hivi punde, Mgongolwa amesema kwamba bado wanaendelea kusistiza Yanga wafuate Katiba yao katika hilo.
  “Tumeomba watuletee rekodi za Wajumbe waliojiuzulu, watatupatia kesho, tukishapata tutawapa mwongozo kwa mujibu wa Katiba,” alisema Mgongolwa.
  Akizungumzia kitendo cha Nchunga kusema anaikabidhi timu kwa Baraza la Wadhamini wa klabu baada ya kujiuzulu, Mgongolwa alisema katika hilo yuko yuko sahihi, ila akasema Wajumbe wote ambao bado hawajajiuzulu nyadhifa zao bado wanatambuliwa kama Wajumbe halali na wanapaswa kutambuliwa.
  Baraza la Wazee Yanga
  Mapema leo mchana, kikao cha Kamati ya Utendaji ya Yanga kujadili barua ya Nchunga kujiuzulu kilishindwa kufanyika, kutokana na safu kutotimia.
  Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa aliiambia BIN ZUBEIRY mchana kwamba, Mbaraka Igangula yupo Afrika Kusini wakati Khalifa Mgonja yupo Arusha,
  Mwesigwa alisema kwa sababu hiyo, wanasubiri Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji wafike Dar es Salaam ndipo kikao kifanyike. Wakati huo huo, Wazee wa klabu hiyo walikutana na waandishi wa Habari leo mchana makao makuu ya klabu na kusema kwamba, hawamtambui Mjumbe yeyote wa Kamati ya Utendaji, kwani Nchunga ameondoka na watu wake wote.
  Aidha, baadhi ya Wajumbe waliotangaza kujiuzulu wameanza kuzikana barua zao, wakidai walilazimika kuandika kutokana na vitisho walivyokuwa wakipewa. 
  Jana, Nchunga (pichani kushoto) alitangaza kujiuzulu Uenyekiti wa Yanga, akisema timu anaikabidhi kwa Baraza la Wadhamini, ambalo kwa sasa linaundwa na wajumbe watatu, Mama Fatuma Karume, Deo Filikunjombe na Francis Kifukwe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIKAO CHA KAMATI YA MGONGOLWA CHAMALIZIKA, HALI BADO TETE YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top