• HABARI MPYA

  Alhamisi, Mei 24, 2012

  HISTORIA YA EURO A-Z MJUE NA MWASISI WAKE


  Mabingwa watetezi Hispania

  MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Ulaya, Euro 2012 inayoandaliwa kwa pamoja na Poland na Ukraine itakuwa ni fainali za 14 za michuano hiyo kufanyika.
  Lilikuwa ni wazo la Henri Delaunay, Katibu wa Shirikisho la Soka Ufaransa, ambaye aliibuka na wazo hilo kwa mara ya kwanza kwenye bara hilo, mwaka 1927.
  Kwa mara ya kwanza alipata sapoti kidogo sana na michuano hiyo haikuanza hadi mwaka 1960. Hadi mwaka 1980 ni timu nne tu zilikuwa zinacheza hatua ya fainali, lakini sasa ni timu 16 na imekuwa moja ya michuano mikubwa katika kalenda ya soka.
  Michuano yote 13 iliyotangulia imeacha kumbukumbu kibao – BIN ZUBEIRY  inakuletea wasifu wa michuano hiyo hadi kufikia fainali za mwaka huu.
  Mfungaji wa bao la ubingwa fainali zilizopita za Euro,Torres amerejeshwa kikosini dakika za mwishoni, je atang'ara tena?

  1960
  MICHUANO ya kwanza ilifanyika Ufaransa na bingwa alikuwa Soviet Union. Mabingwa hao waliongozwa na kipa wao gwiji, Lev Yashin langoni kwenye michuano hiyo. Kipa aliyeipa England taji la Kombe la Dunia, Gordan Banks alifunikwa na kipa huyo.

  1964
  Hispania kwa sasa wanatawala katika ulimwengu wa soka, lakini mafanikio yao ya kwanza yalikuja katika Euro ya 1964, wakati walipotwaa taji hilo kwenye ardhi ya nyumbani katika timu iliyoongozwa na Luis Suarez. Kiungo huyo aling’ara kwenye michuano hiyo, ambayo Hispania ilifunika mbaya.

  1968
  Michuano ya tatu ya Ulaya ilifanyika Italia na kama ilivyokuwa Hispania 1964, pia michuano hii ubingwa ulichukuliwa na wenyeji. England ilifika Nusu Fainali na ilifungwa na Yugoslavia katika mechi ya kusisimua, iliyokuwa na upinzani mkali. Alan Mullery wa England alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi hiyo.

  1972
  Waliokuwa mabingwa watetezi wa Ulaya, Italia walishindwa kufuzu kuingia kwenye fainali hizo, wakiangushwa na Ubelgiji waliokuwa wenyeji, katika Robo Fainali. Pamoja na hayo, Ujerumani waliweza, waliwafunga wenyeji hao na kufuzu kutinga fainali za michuano hiyo, ambako waliifunga iliyokuwa USSR mabao 3-0 na kutwaa Kombe.

  1976
  Michuano ‘iliyong’ara’ ya Euro 1976 taji lilichukuliwa na Czechoslovakia walioifunga Ujerumani Magharibi kwenye fainali kwa mikwaju ya penalti mjini Belgrade. Lakini pia ilikuwa michuano ambayo Wales ilikaribia kufuzu.

  1980
  Mfumo wa michuano ulibadilika mwaka 1980, kwa timu nane kuingia kwenye fainali, lakini mwonekano wa matokeo haukubadilika, kwa Ujerumani kutwaa ubingwa. Pamoja na hayo, kulikuwa kuna ‘maajabu’ kadhaa ikiwemo Ubelgiji iliyokuwa na vipaji babu kubwa kufika fainali, mmojawao akiwa ni Jean-Marie Pfaff.

  1984
  Ufaransa walikaribia kutwaa taji la Kombe la Dunia mwaka 1982, kabla ya kupokonywa tonge mdomoni na Ujerumani Magharibi katika Nusu Fainali ya kukumbukwa, lakini hakukuwa na maajabu katika ardhi ya nyumbani, wakati Wafaransa walipoongozwa na gwiji wake Michel Platini kutwaa taji hilo.

  1988
  Ilikuwa ni michuano ambayo mshambuliaji wa Uholanzi, Marco van Basten alikuwa hana wa kumfananisha naye, kutokana na kufunga mabao ambayo yaliiwezesha nchi yake kutwaa Kombe. Pamoja na hayo, ilikuwa habari tofauti kwa USSR, iliyoongozwa na kocha wake gwiji, Valery Lobanovsky walipokaribia kutwaa taji.

  1992
  Denmark haikufuzu kwenye fainali hizo nchini Sweden, lakini walipata nafasi kutokana na Yugoslavia kuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, hivyo kushindwa kushiriki. Na vijana hao wakafanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, wakiifunga Ujerumani kwenye fainali. Kim Vilfort, ambaye alifunga kwenye fainali alielezea namna ambavyo Denmark walikuwa na maandalizi mazuri kabla ya fainali hizo.

  1996
  Euro 96 – michuano ambayo ilipewa jina soka imerejea nyumbani. England ilifika Nusu Fainali, lakini ikafungwa na Ujerumani kwa mikwaju ya penalti. Ujerumani ilifanikiwa kutwaa taji hilo kwa kuifunga Czechs Uwanja wa Wembley. Mshambuliaji wa England, Alan Shearer alifanya vitu adimu sana kwenye fainali hizo.

  2000
  England ilifanikiwa kuifunga Ujerumani, lakini hawakufanikiwa kufuzu kutoka kwenye kundi lao na vijana wa Kevin Keegan walirejeshwa nyumbani kimaajabu. Ufaransa walitwaa Kombe la Dunia nyumbani kwao mwaka 1998 na wakadhihirisha ubabe wao kwa kutwaa taji la Ulaya pia kwenye fainali zilizoandaliwa kwa pamoja na Ubelgiji na Uholanzi. Kiungo Emmanuel Petit aliyeng’ara kwenye michuano hizo alielezea siri ya mafanikio ya nchi yao.

  2004
  Euro 2004: Ugiriki walipoibuka mabingwa. Ilikuwa unakwenda kuwa mwaka wa Ureno, katika fainali ambazo walikuwa wenyeji, lakini wakafungwa na Ugiriki 1-0 kwenye fainali. Cristiano Ronaldo aliumizwa sana na matokeo hayo, kwani ulikuwa mwaka wa kufurahia mafanikio na timu yake ya taifa, lakini ikashindikana.   

  2008
  Katika michuano iliyoandaliwa kwa pamoja na Uswisi na Austria, ambayo ilifana, Hispania waliibuka mabingwa baada ya miaka 44 ya kusubiri taji la kimataifa. Hispania waliifunga 1-0 Ujerumani katika fainali, bao pekee la Fernando Torres dakika ya 33 na sasa wanaingia kwenye fainali za mwaka huu kutetea taji, wakiwa pia mabingwa wa dunia. Je, wataweza? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HISTORIA YA EURO A-Z MJUE NA MWASISI WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top