• HABARI MPYA

    Saturday, August 19, 2017

    HATIMA YA KIPA MCAMEROON YANGA KUJULIKANA KESHO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kesho inatarajiwa kuzikutanisha klabu za Yanga na African Lyon zote za Dar es Salaam katika kikao cha kujadili suala la kipa Mcameroon, Youthe Rostand Jehu.
    Rostand alichezea African Lyon msimu uliopita, lakini baada ya timu hiyo kuteremka Daraja, amehamia kwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC. Hata hivyo, Lyon inayomilikiwa na Rahim Kangenzi ‘Zamunda’ imewasilisha malalamiko TFF ikidai Yanga haikufuata taratibu kumchukua kipa wake huyo.
    Kwa ujumla Lyon imeondokewa na wachezaji 19 akiwemo Rostand baada ya kushuka Daraja na inadai wachezaji wote wote hawakufuata taratibu katika kuondoka kwao, hivyo inadai fidia kwa klabu zilizowachukua.
    Hizo ni pamoja na Majimaji iliyomchukua Saleh Malande, Lipuli iliyowachukua Hamad Manzi, Lambele Reuben na Mussa Nampoka, Tusker FC ya Kenya iliyomchukua Abdul Hilal na Ndanda FC ya Mtwara iliyowachukua Hamad Tajiri na Baraka Majogoo.
    Madai mengine ni dhidi ya Coastal Union kwa wachezaji Baraka Jaffary, Omary Salum, Raizen Hafidh na Fred Lewis huku madai mengine ni kwa Kagera Sugar kwa wachezaji Omar Abdallah, Abdallah Mguhi na Vicent Ludovic na Alhaji Zege .
    Madai mengine ni dhidi ya timu ya Kinondoni Municipality Council (KMC) ambayo imewasajili Halfan Twenye, Yussuf Abdul na Rehani Kibingu wakati Singida United inalalamikiwa kumsajili Miraji Adam ilihali Njombe Mji inadaiwa fidia kwa kumsajili mchezaji Salum Juma.
    Malalamiko mengine ni ya Kisa Academy ya Kinondoni, Dar es Salaam dhidi ya timu za Mbeya City (Idd Seleman); Majimaji (Jafar Mohammed); Mbao (Ally Rashid); Stand United (Said Mbati) na Friends Rangers (Hassan Abubakar).
    Madai mengine dhidi ya timu za Coastal Union (Abubakar Nyakarungi na Ahmed George); The Mighty Elephant (Maliki Hamad); Kagera Sugar (Hussein Idd) na Azam FC (Omary Maunda).
    Kamati imewaita viongozi au wawakilishi wa klabu za Azam FC, Pamba FC, African Lyon, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Singida United, Tusker FC, Yanga, Njombe Mji, Majimaji, KMC, Ndanda FC, Coastal Union,  Stand United, Rhino FC, Mbao FC, Toto Africans, Stand United, Mbeya City na Lipuli pamoja na wachezaji Mbaraka Yussuf na Frank Hamisi katika kikao cha kesho.
    Pamoja na Luon, klabu nyingine na vituo vya kuibua na kukuza vipaji pia vimewasilisha malalamiko TFF kudai fidia mbalimbali kama vile za mafunzo; ada ya usajili; ada za maendeleo na kuvunjwa kwa mikataba kutoka katika timu walizochezea hadi msimu uliopita.
    Baadhi ya malalamiko yaliyopokelwa TFF ni ya Majimaji ya Songea dhidi ya Azam FC ya Dar es Salaam kuhusu mchezaji Idd Kipangwile.
    Alliance ya Mwanza imelalamikia Pamba pia ya Mwanza kuhusu mchezaji Juma Nyangi ambako madai hayo yamekwenda mbali zaidi yakisema kuwa mchezaji husika amebadili jina kwa lengo la kudanganya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATIMA YA KIPA MCAMEROON YANGA KUJULIKANA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top