• HABARI MPYA

  Sunday, August 27, 2017

  HII YA BUSWITA MBONA IMEZUKA ZUKA TU NA HAIONYESHI DALILI ZA MCHEZAJI KUTENDEWA HAKI

  KIUNGO wa Yanga, Pius Buswita amefungiwa kucheza soka ndani na nje ya nchi kwa mwaka mmoja kwa kosa la kusaini mikataba na klabu mbili, nyingine ikiwa ni Simba. 
  Hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyokutana kwa siku mbili mfululizo Agosti 20 na 21, 2017, mjini Dar es Salaam kupitia usajili wa wachezaji wa klabu 40.
  Katika idadi hiyo ya timu 40, Kamati chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa ilipitia klabu 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa mujibu wa katiba na kanuni za mashindano yanayosimamiwa na kuendeshwa na TFF.
  Ndipo katika taarifa yake, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ikasema imegundua na kubaini kuwa mchezaji Pius Busita amesaini mikataba ya klabu mbili tofauti katika msimu huu wa 2017/18.
  Kamati imebaini kwamba mchezaji huyo aliyechezea Mbao FC ya Mwanza msimu uliopita, amevunja Kanuni ya 66 ya Ligi Kuu ya Vodacom ambayo inaelekeza adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja. Na kwa sababu hiyo, Buswita amefungiwa kucheza mpira wa miguu kwa mwaka mmoja.
  Lakini kuna mambo ya kujiuliza kuhusu suala la Buswita ambayo majibu yake hayapatikani moja kwa moja zaidi ya TFF na Kamati yake kutolea ufafanuzi.
  Kamati inaposema imegundua na kubaini kuwa mchezaji Pius Busita amesaini mikataba ya klabu mbili tofauti katika msimu huu wa 2017/1 inamaanisha nini?
  Tunafahamu kuna mkataba wa awali, mkataba kamili wa usajili na hati ya makubaliano ya kusaini mkataba taratibu zitakapokamilishwa – wa Buswita na Simba ni upi?  
  Awali, katika usajili wao, Simba hawakuwasilisha jina la Buswita, zaidi ya Yanga pekee.
  Lakini kwenye taarifa ya awali kabisa ya TFF juu ya wachezaji waliolalamikiwa, jina la Buswita halikuwemo.
  Taarifa ya awali ya TFF ni hii; “TFF imepokea malalamiko ya Kagera Sugar ya Kagera dhidi ya Azam FC ya Dar es Salaam kuhusu mchezaji Mbaraka Yussuf wakati Majimaji ya Songea pia imelalamika Azam kuhusu mchezaji Idd Kipangwile.
  Kwa ujumla TFF imepokea malalamiko kutoka baadhi ya timu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji vya soka zikidai fidia baada ya wachezaji wao kusajiliwa na klabu nyingine msimu wa 2017/18.
  Jana Agosti 14, 2017 ilikuwa siku ya mwisho kwa timu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji kuwasilisha malalamiko yao TFF kuhusu fidia za mafunzo; ada ya usajili; ada za maendeleo na kuvunjwa kwa mikataba kutoka katika timu walizochezea hadi msimu uliopita.
  Alliance ya Mwanza imelalamikia Pamba pia ya Mwanza kuhusu mchezaji Juma Nyangi ambako madai hayo yamekwenda mbali zaidi yakisema kuwa mchezaji husika amebadili jina kwa lengo la kudanganya.
  Kwa upande wake, African Lyon imeondokewa na wachezaji 19 na inadai fidia katika timu, wachezaji kwenye mabano za Majimaji (Saleh Malande); Lipuli (Hamad Manzi, Lambele Reuben na Mussa Nampoka); Young Africans (Rostand Youthe Jehu); Tusker FC (Abdul Hilal) na Ndanda kwa wachezaji Hamad Tajiri na Baraka Majogoo.
  Madai mengine ni dhidi ya Coastal Union kwa wachezaji Baraka Jaffary, Omary Salum, Raizen Hafidh na Fred Lewis huku madai mengine ni kwa Kagera Sugar kwa wachezaji Omar Abdallah, Abdallah Mguhi na Vicent Ludovic na Alhaji Zege .
  Madai mengine ni dhidi ya timu ya Kinondoni Municipality Council (KMC) ambayo imewasajili Halfan Twenye, Yussuf Abdul na Rehani Kibingu wakati Singida United inalalamikiwa kumsajili Miraji Adam ilihali Njombe Mji inadaiwa fidia kwa kumsajili mchezaji Salum Juma.
  Malalamiko mengine ni ya Kisa Academy ya Kinondoni, Dar es Salaam dhidi ya timu za Mbeya City (Idd Seleman); Majimaji (Jafar Mohammed); Mbao (Ally Rashid); Stand United (Said Mbati) na Friends Rangers (Hassan Abubakar).
  Madai mengine dhidi ya timu za Coastal Union (Abubakar Nyakarungi na Ahmed George); The Mighty Elephant (Maliki Hamad); Kagera Sugar (Hussein Idd) na Azam FC (Omary Maunda).
  Kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kinatarajiwa kuketi Jumapili kupitisha usajili lakini kabla kitapitia malalamiko hayo na kuchukua uamuzi,”. Mwsho wa taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas. 
  Ilikuwaje katika taarifa hii Buswita hakutajwa, lakini suala lake likapelekwa moja kwa moja kwenye Kamati?
  Pamoja na yote, lakini yanayozungumzwa zungumzwa pembeni na viongozi wa klabu zote kuhusu mchezaji huyo ni kwamba, awali alifanya mazungumzo na Simba na wakampa fedha kidogo kwa ahadi wangemmalizia nyingine ili asaini mkataba.
  Haielezwi kama alipwa fedha hizo kwa maandishi au la. Lakini inadaiwa, Simba ilikuwa inasubiri mchezaji huyo amalize mkataba wake na Mbao ndiyo imsainishe mkataba kamili.
  Hata hivyo, Yanga ikaenda kuzungumza na klabu ya Buswita, Mbao FC na kufikia nayo makubaliano ya kumnunua na baadaye ikaenda kumalizana na mchezaji mwenyewe.
  Kilichofuata inadaiwa, Buswita alipowapelekea Simba fedha zao wakagoma kuzipokea na ikaonekana kama suala hilo mwisho wake itakuwa kulipana fedha baina ya klabu na mchezaji.
  Lakini kinachofuatia mchezaji chipukizi mwenye kipaji anafungiwa mwaka mzima kwa kosa la kuzungumzika. Na bahati mbaya Kamati ya Sinamtwa imefanya maamuzi yake bila hata kumsikiliza mchezaji mwenyewe.
  Wakati Kamati ya Sinamtwa inakutana Jumapili Dar es Salaam, Buswita alikuwa kambini Pemba na timu yake iliyokamilisha taratibu za kumsajili kutoka Mbao FC – hivyo huoni saa ngapi aliitwa kwenye kikao kuulizwa kuhusu madai ya Simba.
  Inaonekana kabisa kwa jinsi suala lilivyopelekwa hadi hatua kuchukuliwa, mchezaji hakutendewa haki.   
  Na kwenye mitandao ya jamii, Yanga wanalalamika wanaonewa kwa sababu Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia na Makamu wake, Michael Wambura pamoja na Wajumbe karibu wote wa Kamati ya Utendaji ni manazi wa Simba.
  Sitaki kuamini hayo madai ya Yanga kwamba eti wanaonewa kwa sababu viongozi wa TFF ni Simba – bali inawezekana ni mapungufu ya kawaida ya kiutendaji na wahusika wanaweza kurudi kwenye mwongozo kufuata taratibu katika suala la mchezaji huyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HII YA BUSWITA MBONA IMEZUKA ZUKA TU NA HAIONYESHI DALILI ZA MCHEZAJI KUTENDEWA HAKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top