• HABARI MPYA

    Wednesday, August 23, 2017

    YANGA WABABE MARA NYINGI, SIMBA WAZEE WA DOZI NZITO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WAKATI watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga wanakutana jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii, mashabiki wa timu hizo wanatambiana kwa mambo mawili.
    Yanga wanajivunia kuwafunga mara nyingi zaidi wapinzani wao katika mechi zilizozikutanisha timu hizo, wakati Simba wanajivunia vipigo vya mabao mengi, vikiongozwa na kile cha 6-0.   
    Katika mechi 98  za Ligi Kuu na iliyokuwa Ligi Kuu ya Muungano zilizozikutanisha timu hizo tangu mchezo wa kwanza Juni 7, mwaka 1975, Yanga imeshinda mara 36 wakati Simba imeshinda mara 26 na mechi nyingine 33 timu hizo zikitoka sare.  
    Mgogoro wa mwaka 1976 ulioibuka na kuigawa Yanga hadi kuzaliwa Pan African, ulisababisha athari nyingine kadhaa za kihistoria kwenye klabu hiyo, zaidi ya mgawanyiko huo.
    Amebadilisha jezi; Mshambuliaji Ibrahim Hajib (kushoto) akipinda krosi pembeni ya wachezaji wa Yanga. Hajib leo ataibuka na jezi ya kijani  

    Baada ya mgogoro wa Yanga Kandambili na Yanga Raizoni, rasilimali nyingi za klabu hiyo, yakiwemo mabasi ziliteketea. Lakini pengine hilo inawezekana lisiwaumize sana wana Yanga, kuliko kipigo kutoka kwa watani wao wa jadi, Simba, cha mabao 6-0.
    Baada ya mgogoro huo, kwa sababu wachezaji wote walimfuata mzee Tarbu Mangara aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yanga walilazimika kuunda upya timu yao, wakisajili wachezaji wapya. Tangu mwaka 1977, Yanga walikuwa vibonde wa Simba hadi mwaka 1981, walipojikomboa.
    Tangu kuanzishwa kwa Ligi ya Tanzania, mwaka 1965 hadi mwaka 1976 Yanga inakutwa na mgogoro huo, ilikuwa imekutana na watani wao wa jadi, Simba kwenye mechi 10. Katika mechi hizo, Yanga walishinda saba, Simba waliibuka kidedea mara mbili na mara moja ilikuwa ni sare.  
    Kati ya mara saba ambazo Yanga iliifunga Simba, ndani yake kuna kipigo cha mabao 5-0, Juni Mosi mwaka 1968, enzi hizo Simba bado ikiitwa Sunderland. 
    Siku hiyo, mabao ya Yanga yalitiwa kimiani na Maulid Dilunga dakika za 18 kwa penalti na 43, wakati mengine yalifungwa na Salehe Zimbwe dakika za 54 na 89 na kuhitimisha karamu ya mabao, lilifungwa na Kitwana Manara 'Popat' dakika ya 86.
    Kwa homa ya kipigo hicho, kwenye mchezo uliofuata Machi 3, mwaka 1969, Simba waliishia njiani maeneo ya Chang'ombe na kurejea klabuni kwao, wakihofia kutandikwa zaidi, hivyo watani wao wa jadi, kupewa pointi za chee.
    Baada ya hapo, timu hazikukutana hadi Juni 4, mwaka 1972, Simba wakiwa madhubuti tayari kuweza kuhimili vishindo vya Yanga. Katika mchezo huo, timu hizo zilitoka sare ya 1-1, tena Sunderland ikitangulia kupata bao kupitia mshambuliaji wake, Willy Mwaijibe, dakika ya 11, kabla ya Kitwana Manara kusawazisha dakika nane baadaye.
    Juni 18, mwaka huo huo 1972, timu hizo zilikutana tena na bao pekee la Leonard Chitete (sasa marehemu) lilitosha kuendeleza ubabe wa Yanga kwa Simba.
    Haidari Abeid 'Muchacho' alikomesha tabia ya Simba kufungwafungwa na Yanga, katika mechi baina ya watani hao wa jadi, Juni 23, mwaka 1973, akifunga bao pekee lililowalaza mapema wana Jangwani, dakika ya 68. 
    Wakati Simba ikiamini imekwishapata dawa ya Yanga, Agosti 10, mwaka 1974 katika mchezo uliowakutanisha watani hao wa jadi nje ya Dar es Salaam, kwa mara ya kwanza, Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza, Wekundu wa Msimbazi walikiona cha moto.
    Wekundu wa Msimbazi walianza vizuri kwa kuwatungua Yanga bao la mapema dakika ya 16 tu ya mchezo, mfungaji akiwa ni Adamu Sabu. Lakini zikiwa zimesalia dakika tatu mchezo kumalizika, mjini Dar es Salaam, mashabiki wa Simba wakiwa wamekwishajikusanya kuanza misafara ya kuelekea makao makuu ya klabu hiyo, Mtaa wa Msimbazi kushangilia ushindi, walikuwa wanyonge ghafla baada ya mtangazaji wa Radio Tanzania (RTD), Ahmad Jongo kutangaza bao la kusawazisha la Gibson Sembuli (sasa marehemu).
    Kwa bao hilo, mchezo huo kwa sababu ulikuwa wa kuamua bingwa, ilibidi uhamie kwenye dakika 30 za nyongeza. Dakika ya saba Sunday Manara aliwainua vitini mashabiki wa Yanga waliokuwa Nyamagana kwa kufunga bao la pili. Naam, huo ulikuwa ushindi wa mwisho wa Yanga kwa Simba, kwani baada ya hapo, mgogoro wa Yanga Kandambili na Yanga Raizoni uliitafuna klabu hiyo.
    Hatimaye ikawadia siku chungu zaidi katika maisha ya Yanga kwenye utani wao na Simba, ilikuwa ni Julai 19, mwaka 1977 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, enzi hizo Simba ikinolewa na Mbulgaria, Dimitar Samsarov.
    Simba ikiwa na 'mziki' wake ule ule uliokuwa ukichuana na Yanga tangu mwaka 1974, ilikutana na Yanga mpya kabisa iliyoundwa na wachezaji kama kipa aliyekuwa Mwadui ya Shinyanga, Bernard Madale.
    Yanga walishindwa kuimudu kasi ya Simba na kujikuta wakitandikwa mabao 6-0, mabao ya Wekundu wa Msimbazi yakitiwa kimiani na Abdallah Kibadeni katika dakika za 10, 42 na 89, Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika za 60 na 73, wakati Selemani Sanga alijifunga mwenyewe dakika ya 20. Kipigo hicho kilikuwa sababu tosha ya kipa Madale kutupiwa virago Jangwani. 
    Lakini Yanga iliendelea kuchezea vipigo tu walipokutana na Simba, japokuwa Oktoba 7, mwaka 1979 walipunguziwa dozi kwa kiwango cha nusu nzima, kutoka bao sita hadi tatu. 
    Yanga ilichapwa 3-1 siku hiyo, mabao ya Simba yakifungwa na Nico Njohole dakika ya tatu, Mohammed Bakari 'Tall' dakika ya 38 na Abbas Dilunga dakika ya 72, wakati lile la kufutia machozi la Yanga lilifungwa na Rashidi Hanzuruni dakika ya nne.
    Oktoba 4, mwaka 1980, Yanga ilipigwa tena 'nusu dozi' ya 6-0, mabao ya wana Msimbazi yakitiwa kimiani na Abdallah Mwinyimkuu dakika ya 29, Thuwein Ally dakika ya 82 na Nico Njohole dakika ya 83.
    Hatimaye saa ya ukombozi iliwadia Jangwani, Juma Hassan Mkambi akiitwa 'Jenerali' enzi zake alikomesha uteja wa Yanga kwa Simba, Septemba 5, mwaka 1981, kwa bao lake pekee dakika ya 42. Siku hiyo, mabeki wa Yanga walifanya kazi kubwa ya kulinda bao hadi dakika 90 zilipotimia, wana Jangwani wanainua mwali wao.
    Naam, Mkambi alifuta uteja wa Yanga kwa Simba na kuanzisha rasmi enzi za Jangwani kuwanyima raha wana Msimbazi, kwani katika mechi iliyofuata, Aprili 29, mwaka 1982, bao la Rashid Hanzuruni dakika ya pili tu ya mchezo liliifanya Simba ilale tena 1-0.
    Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kuwakutanisha watani wa jadi, tangu kuanza kwa Ligi ya Bara kutoka Klabu Bingwa ya Taifa na katika mchezo wa marudiano, Simba walikiona tena cha moto, walitandikwa 3-0, Septemba 18, mwaka huo, 1982.
    Mabao ya Yanga siku hiyo yalitiwa kimiani na Omar Hussein 'Keegan'
    katika dakika ya pili na ya 85, wakati lingine lilifungwa na Makumbi Juma 'Homa ya Jiji' au 'Bonga Bonga' dakika ya 62. GONGA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HII
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WABABE MARA NYINGI, SIMBA WAZEE WA DOZI NZITO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top