• HABARI MPYA

  Thursday, August 31, 2017

  LWANDAMINA AFIWA NA BABA MZAZI

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa Yanga SC, George Lwandamina ameondoka leo Dar es Salaam kwenda kwao, Zambia kwa ajili ya mazishi ya baba yake mzazi, mzee Lwandamina aliyefariki dunia jana baada ya kusumbuliwa na maradhi ya Kiharusi.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo asubuhi wakati anaanza safari yake, Lwandamina amesema kwamba amezipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa baba yake na amelazimika kurejea nyumbani mara moja kwa mazishi.
  “Nasikitika kuthibitisha kifo cha baba yangu mzazi, amefariki jana Zambia na mazishi yatafanyika kesho. Hapa nipo njiani ninaelekea huko kwa shughuli za mazishi yake,”amesema Lwandamina.
  Kocha wa Yanga, George Lwandamina amefiwa na baba yake mzazi jana kwao Zambia 

  Ni ahueni kwa Yanga msiba huu umetokea katika kipindi cha mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa wikiendi hii, maana yake hawatakuwa kwenye mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Kikosi cha Yanga sasa kitabaki chini ya makocha Wasaidizi, Mzambia mwenzake Lwandamina, Noel Mwandila na wazawa, Nsajigwa Shadrack na kocha wa makipa, Juma Pondamali.
  Yanga inatarajiwa kurudi uwanjani kwa mchezo wake wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumatano ijayo dhidi ya wenyeji Njombe Mji Uwanja wa Saba Saba baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lipuli ya Iringa. 
  Hata hivyo kuna uwezekano mchezo huo ukasogezwa mbele au kurudishwa nyuma kutokana na maombi ya wenyeji kwa kuwa Uwanja huo upo katikati ya eneo la shule tatu za Msingi, ambazo siku hiyo zitakuwa katika mtihani wa taifa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LWANDAMINA AFIWA NA BABA MZAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top