• HABARI MPYA

    Monday, August 28, 2017

    KIMWAGA AZUA HOFU AZAM BAADA YA KUUMIA MTWARA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WINGA wa kushoto wa Azam FC, Joseph Kimwaga jana alisafirishwa kwa ndege kurejea jijini Dar es Salaam kufanyiwa uchunguzi wa goti lake la mguu wa kushoto lililopata mshtuko.
    Kimwaga aliyekuwa ameanza kurejea vema kwenye kiwango chake kilichomtambulisha huko nyuma, amepata majeraha hayo kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu cha TTC cha mkoani Mtwara, Alhamisi iliyopita wakati Azam FC ikijiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ndanda.
    Lilikuwa ni tukio la kushitukiza kwani hakukuwa na mgongano wowote dhidi ya mchezaji mwingine, bali wakati akimiliki mpira pembeni ya uwanja akijiandaa kupiga mpira alijikuta akishindwa kukanyagia mguu wake baada ya kupata maumivu makali alipojaribu kufanya hivyo.
    Joseph Kimwaga jana alisafirishwa kwa ndege kutoka Mtwara kuwahi Dar es Salaam kufanyiwa uchunguzi wa goti lake la mguu wa kushoto 

    Baada ya tukio hilo, Kimwaga alipatiwa huduma ya kwanza na daktari wa timu, Mwanandi Mwankemwa, kabla ya kukimbizwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara kupatiwa matibabu ya awali na kusahauri apelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ili kufanyiwa kipimo cha MRI kubaini undani wa tatizo lake.
    Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffary Idd, amesema kuwa mchezaji huyo tayari amewasili jijini hapa tayari kabisa kufanyiwa kipimo hicho kesho Jumatatu.
    Idd amesema kuwa mara baada ya kufanyiwa kipimo hicho, itajulikana kama tatizo alilonalo litaweza kutibiwa nchini au kusafarishwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi ili kuokoa kipaji chake.
    Hii ni mara ya pili Kimwaga kuumia kwenye goti lake hilo, mara ya kwanza alivunjika miaka mitatu iliyopita hali iliyofanya kupelekwa nchini Afrika Kusini kufanyiwa matibabu na kurejea tena uwanjani.
    Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora ya NMB na Tradegents, imekuwa ikijalia vilivyo afya za wachezaji wake na haijawahi kusita kumsafirisha nje ya nchi kwa matibabu nyota wake pale inapogundulika tatizo hilo ni ngumu kutibiwa hapa nchini.
    Imewahi kufanya hivyo kwa kiungo Frank Domayo, aliyesajiliwa kutokea Yanga na kugundulika ana tatizo la muda mrefu la nyama za paja jambo lililokuwa likitishia uhai wa kipaji chake, lakini Azam FC ikamsafirisha haraka nchini Afrika Kusini na kupata matibabu mazuri.
    Wengine baadhi yao walioko kwenye orodha hiyo ni mabeki Ismail Gambo, Samih Nuhu, nahodha wa zamani John Bocco, nahodha msaidizi, Aggrey Moris, Pascal Wawa, Shaaban Idd, Mbaraka Yusuph, ambao walienda kufanyiwa uchunguzi wa kiafya nchini humo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIMWAGA AZUA HOFU AZAM BAADA YA KUUMIA MTWARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top