• HABARI MPYA

    Wednesday, August 23, 2017

    SHUGHULI PEVU SIMBA NA YANGA TAIFA LEO...LWANDAMINA KUENDELEZA UNYONGE KWA OMOG?

    Na mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mzambia wa Yanga, George Lwandamina leo ataiongoza timu hiyo katika mchezo wa tatu dhidi ya Simba, akiwa na rekodi ya kufungwa mechi zote mbili zilizotangulia.
    Yanga inakutana na mahasimu wao wa jadi, Simba katika mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii kuanzia Saa 11:00 jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuashiria ufunguzi rasmi wa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Huo utakuwa mchezo wa tatu kwa Mzambia, George Lwandamina tangu achukue nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm Desemba mwaka jana na mechi mbili zilizopita zote alipoteza.  
    Januari 10, mwaka huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar – Yanga ilifungwa kwa penalti 4-2 na Simba baada ya sare ya 0-0 katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi.
    Na Februari 26, mwaka huu, Simba ikatoka nyuma na kushinda 2-1 kwa mabao ya Mrundi Laudit Mavugo dakika ya 66 na mzawa, Shiza Kichuya dakika ya 81, baada ya Simon Msuva kuanza kuifungia Yanga kwa penalti dakika ya tano.
    Kocha Mzambia, George Lwandamina amefunga mechi zote mbili alizokutana na Simba chini ya kocha Mcameroon, Joseph Omog

    Na mechi zote Lwandamina amefungwa na Simba ikiwa chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog akisaidiwa na Mganda, Jackson Mayanja ambao wote leo watakuwepo kwenye benchi la Simba kama kawaida.
    Katika benchi la Yanga kuna mabadiliko kidogo, kocha msaidizi wa msimu uliopita, Juma Mwambusi hayupo na nafasi yake imechukuliwa na beki na Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele. 
    Kwenye benchi la Simba, ameondoka kocha wa makipa Mkenya, Iddi Salim na nafasi yake kuchukuliwa na golikipa wa zamani wa timu hiyo, Muharami Mohammed ‘Shilton’.
    Kiungo Haruna Niyonzima leo ataibukia kwa mahasimu Simba, baada ya miaka sita ya kucheza Yanga tangu alipojiunga nayo mwaka 2012 akitokea APR ya kwao, Rwanda. Yanga pia imempoteza mchezaji wake mahiri na aliyekuwa tegemeo katika safu ya ushambuliaji, Simon Msuva aliyehamia Difaa Hassan El- Jadida ya Ligi Kuu ya Morocco.
    Mshambuliaji Ibrahim Hajib naye leo ataibukia kwa watani, Yanga baada ya kuibukia timu ya vijana ya Simba na kupandishwa kikosi cha kwanza cha timu hiyo alikopatia umaarufu. Simba pia haitakuwa na beki wake, Abdi Banda aliyehamia Baroka FC ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
    Lakini timu zote zimejiimarisha kwa usajili mzuri wa wachezaji wapya, wanaotarajiwa kuchukua nafasi leo kama Aishi Manula, Said Mohammed, Erasto Nyoni, Ally Shomary, Salim Mbonde, Jamal Mwambeleko, Yussuf Mlipili, Paul Bundala, Shomary Kapombe, John Bocco, Nicholas Gyan na Emmanuel Okwi kwa upande wa Simba na Youthe Rostand, Ramadhan Kabwili, Gardiel Michael, Abdallah Haji ‘Ninja’, Papy Kabamba Tshishimbi, Raphael Daudi, Pius Buswita na Baruan Akilimali kwa Yanga. 
    Timu zote zilikuwa kambini upande wa pili wa Muungano wa Tanzania kwa wiki nzima – Yanga walikuwa kisiwani Pemba na Simba walikuwa Unguja na kabla ya mchezo wa leo, kila timu imecheza mechi sita za kujipima na kila moja ilipoteza mchezo mmoja.
    Simba ilifungwa 1-0 na Orlando Pirates, kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Bidvest Wits nchini Afrika Kusini, ikashinda 1-0 na Rayon Sport ya Rwanda, 1-0 na Mtibwa Sugar, 0-0 na Mlandege na kumalizia kwa ushindi wa 5-0 dhidi ya Gulioni FC, wakati Yanga ilishinda 5-0 na Moro Kids, 3-2 na Singida United, ikafungwa 1-0 na Ruvu Shooting, ikashinda 2-0 na Mlandege, 1-0 na Chipukizi na 1-0 na Jamhuri.    
    Kwa ujumla makocha wote wana changamoto ya kuviunganisha vikosi vyao baada ya usajili wa wachezaji wapya wengi ili kutengeneza uwiano mzuri wa timu iweze pia kucheza kwa uelewano.
    Mara ya mwisho Yanga kuifunga Simba ilikuwa ni Februari 20, mwaka 2016 ushindi wa 2-0 uliotokana na mabao ya mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma dakika ya 39 na Amissi Tambwe dakika ya 72, ambao kwa pamoja leo wanatarajiwa kuiongoza tena timu hiyo.
    Lwandamina atafuta uteja kwa Simba leo? Hilo ndilo swali na majibu yatapatikana baada ya mchezo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHUGHULI PEVU SIMBA NA YANGA TAIFA LEO...LWANDAMINA KUENDELEZA UNYONGE KWA OMOG? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top