• HABARI MPYA

  Monday, August 21, 2017

  PAMBANO LA NGAO JUMATANO TAIFA...SIMBA WAITANGULIA YANGA DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Wekundu wa Msimbazi Simba, kimewasili leo mchana jijini Dar es Salaam kwa ndege, kikitokea Unguja ambapo waliweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, utakaopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa.
  Wakati Simba wakitua kwa ndege, wapinzani wao Yanga wanatarajiwa kurejea jijini kesho saa nane mchana wakitokea Pemba ambapo nao waliweka kambi ya takribani wiki moja na nusu kujiandaa na mchezo huo.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, kocha wa Simba, Joseph Omog, alisema kuwa, kikosi chake kipo kwenye hali nzuri na wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya wapinzani wao Yanga.
  Alisema, baada ya kurejea jijini leo jioni watafanya mazoezi katika Uwanja wa Boko Veterani, uliopo Ununio jijini Dar es Salaam.
  Kwa upande wao Yanga, kupitia Ofisa Habari wake, Dissmas Ten, alisema kuwa kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea kesho saa nane mchana na kuingia moja kwa moja kambini.
  Alisema, wachezaji wote wapo katika hali nzuri na wamejiandaa na ushindi kwenye mchezo huo, na wanaamini hilo linawezekana.
  “Mipango yetu na kutwaa kombe hilo, kama ilivyo kawaida yetu, tunamakombe mengi lakini bado tunahitaji kuongeza zaidi, tukianzia na kombe hilo na baadae kombe la Ligi Kuu,” alisema Ten.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PAMBANO LA NGAO JUMATANO TAIFA...SIMBA WAITANGULIA YANGA DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top