• HABARI MPYA

  Monday, August 21, 2017

  MAJI MAJI ‘YAKUNJUA NAFSI’, YARIDHIA KIPWAGILE AKIPIGE AZAM

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Maji Maji ya Songea ‘imekunjua nafsi’ na kumridhia mchezaji wake, Iddi Kipagwile kuhamia Azam FC ya Dar es Salaam kwa kuondoa pingamizi ililoweka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Maji Maji ilimuwekea pingamizi  mchezaji huyo asiidhinishwe kuichezea Azam FC, ikidai ilikuwa bado ina mkataba naye – lakini sasa inaondoa pingamizi hilo kufungua milango ya maisha mapya kwa Kipagwile.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo ofisi za klabu ya Azam FC, barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga amesema kwamba baada ya mazungumzo na uongozi wa Maji Maji mwafaka umepatikana.
  “Tulikuwa tuna kikao cha pamoja na baina yetu uongozi wa Azam FC na uongozi wa Maji Maji na baada ya maongezi tumefikia maafikiano kwamba Iddy Kipagwile sasa ni  mchezaji halali wa Azam CM,”amesema.
  Maganga amesema baada ya mwafaka huo, klabu inaelekeza nguvu zake katika maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza wiki ijayo.
  Na katika sehemu ya maandalizi hayo, Maganga amesema kesho watacheza mchezo wa kirafiki na kikosi cha pili cha timu yao, Azam Academy Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Baada ya mchezo huo, timu itasafiri Jumatano kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona Agosti 26, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAJI MAJI ‘YAKUNJUA NAFSI’, YARIDHIA KIPWAGILE AKIPIGE AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top