• HABARI MPYA

  Wednesday, August 02, 2017

  MGOSI AVULIWA UMENEJA SIMBA, APELEKWA TIMU B

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi ameondolewa kwenye Umeneja wa timu na nafasi yake kupewa, Dk. Cossmas Kapinga.
  Taarifa ya Hajji Sunday Manara, Msemaji wa Simba imesema kwamba mabadiliko hayo yamefanyika katika kikao cha kamati ya Utendaji ya klabu ya Simba iliyokutana hivi karibuni mjini Dar es Salaam.
  Baada ya Daktari huyo wa zamani wa timu kupewa Umeneja – mshambuliaji wa zamani wa Wekundu hao, Mgosi amepangiwa majukumu mengine ndani ya klabu kwa mujibu wa Manara. 
  Kapinga ataanza kazi yake mpya mara baada ya kikosi cha Simba kurejea kutoka nchini kutoka Afrika Kusini, ambako kimeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya, wakati Mgosi, sasa atakuwa kocha msaidizi na Meneja wa Timu ya vijana, sambamba na mchezaji mwingine wa zamani wa timu, Nico Nyagawa.
  Mussa Mgosi (kushoto) ameondolewa kwenye Umeneja wa Simba na nafasi yake kupewa Dk. Cossmas Kapinga 

  Wakati Mgosi ni Kocha Msaidizi na Meneja wa Simba B, Nyagawa atakuwa Kocha Msaidizi na Mratibu, wote wakifanya kazi ya Kocha Mkuu na mchezaji mwingine wa zamani wa timu, kiungo Nico Kiondo. 
  Manara amesema katikati ya mwezi huu Mgosi atafanya mafunzo ya ukocha leseni C, ambayo yatampa fursa ya kuongeza ujuzi kwenye majukumu yake mapya ya ualimu ndani ya timu yetu. 
  Wakati huo huo: Benchi la Ufundi la Simba chini ya Kocha Mkuu, Mcameron Joseph Marius Omog limeridhishwa na kiwango cha timu katika mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji Orlando Pirates licha ya kufungwa 1-0 katika kambi yao ya Afrika Kusini. 
  “Ingawa tumepoteza mchezo wetu wa jana, lakini tumekwishaanza kupata mwelekeo wa kikosi na katika siku chache zijazo tayari tutakuwa tumekwishapata kikosi cha kwanza,”alisema Mwalimu Omog. 
  Simba kesho itashuka kwenye Uwanja wa Sturrock Park uliopo ndani ya Chuo kikuu cha Wits kilichopo Bloemfontein mjini Johannesburg dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Afrika Kusini, Bidvest Wits. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MGOSI AVULIWA UMENEJA SIMBA, APELEKWA TIMU B Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top