• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 02, 2009

  PRISONS, MIEMBENI, MUNDU HOI AFRIKA

  PRISONS imeshindwa kuendeleza raha kwa mashabiki wa soka nchini baada ya kulambwa mabao 2-0 na Khalij Sert ya Libya katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF) uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.
  Timu hiyo ya maafande wa magereza, iliwatoa vichwa chini mashabiki waliofurika kwenye uwanja huo ambao siku moja kabla walitoka kwa kukenua wakati Yanga ilipoishindilia Etoile d'Or Mirontsy ya Comoro kwa mabao 8-1 kwenye mchezo wa hatua ya awali ya Klabu Bingwa Afrika.
  Kipigo hicho cha nyumbani kinaifanya Prisons kuwa katika wakati mgumu kuhusiana na nafasi ya kuvuka raundi inayofuata.
  Khalij Sert ilipata mabao yake katika kila kipindi na sasa itasubiri kucheza katika uwanja wake wa nyumbani ili kujihakikisha kusonga mbele kwenye kiunyang'anyiro hicho.
  Katika mchezo huo, Prisons walionekana kuzidiwa na wageni hao na hivyo 'wajelajela' hao kutoka Mbeya wameachwa na maumivu kabla ya kusafiri hadi mjini Tripoli, Libya kwa ajili ya mechi ya marudiano wiki mbili zijazo.
  Khalij Sert ilifanya uzinduzi wa nyavu za Prisons katika dakika ya tatu ya mchezo baada ya Abdulah Shaiji kutumia makosa ya kipa Exavery Mapunda kufunga bao hilo la kwanza kwa timu yake.
  Wawakilishi hao wa Libya nusura watikise nyavu kwa mara ya pili, wakati shuti la Idris Salim kutoka nje kidogo ya goli la Prisons katika dakika 19 na kuifanya timu kuendelea kuwa na uhai.
  Vijana wa Mshindo Msola, nusura wapate bao la kusawazisha, lakini kukosekana kwa umakini wa wachezaji Yona Ndabila na Fred Chudu kulisababisha timu hiyo kupoteza nafasi za wazi.
  Kipa Mapunda alifanya kazi ya ziada mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kuzuia shuti la karibu la Saadulah el Hafidh na kufanya matokea yabaki 1-0 hadi mapumziko.
  Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, lakini bao la 'tall' wa Khalij Sert, Esheikh Sodoalai katika dakika 61 lilizima kabisa shangwe za mashabiki wa wenyeji waliokuwa kwenye mchezo huo.
  Sodoalai alifunga bao hilo baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Prisons na kupiga mpira ambao Mapunda alishindwa kutoa msaada wa kuinusuru timu yake.
  Nao wawakilishi wa Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Miembeni ililala 2-0 kwa Monomotapa mjini Harare, wakati katika Kombe la Shirikisho Mundu ilichapwa 6-1 na Red Arrows mjini Lusaka juzi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PRISONS, MIEMBENI, MUNDU HOI AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top