• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 23, 2009

  STARS YALALA KWA SENEGAL  abdul mohammed, abidjan
  BAO la kichwa la kipindi cha kwanza lililofungwa na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Senegal, Simba wa Teranga, Mamadou Traure lilizima ndoto za Taifa Stars za kuanza vyema michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 katika mchezo uliofanyika mjini hapa jana.
  Stars iliyopo katika Kundi A la michuano hiyo pamoja na timu za Zambia na wenyeji Ivory Coast, ilianza vizuri mchezo huo na kuonekana kuwamudu wapinzani wao hao kutoka Afrika Magharibi.
  Lakini makosa ya beki Juma Jabu katika dakika 30 yalitoa mwanya wa kupigwa krosi ambayo iliunganishwa kwa kichwa na Traure na mpira kumshinda kipa 'Afande' Juma Dihile na kujaa nyavuni.
  Kuingia kwa bao hilo kuliifanya Senegal kuimarika zaidi huku Stars ikicheza vibaya katika sehemu yake ya katikati.
  Stars iliyocheza kwa mtindo wa kutumia mshambuliaji mmoja pekee, Jerry Tegete, iliwakaba vizuri Simba wa Teranga na mara kadhaa nahodha wa timu hiyo, Sidy Ndiaye alipata tabu mbele ya winga Mrisho Ngassa ambaye na kuzawadiwa kadi ya njano.
  Ndiaye alikuwa na kazi moja ti katika mchezo huo, kumdhibiti Ngassa kazi aliyofanikiwa kwa kiasi kikubwa.
  Kocha Mkuu wa Stars, Marcio Maximo alifanya mabadiliko ya mapema zaidi katika kipindi cha kwanza kwa kuwatoa Godfrey Bonny na Haruna Moshi 'Boban' na kuwaingia Nurdin Bakari na Mussa Hassan 'Mgosi'.
  Mabadiliko hayo hayakubadili zana mchezo katika kipindi hicho cha kwanza kwa kuwa safu ya kiungo ya Stars iliendelea kupwaya na kuwafanya Senegal kutawala sehemu hiyo.
  Kipindi hicho Stars ilipoteza nafasi kadhaa za kufunga kupitia kwa nyota wake Tegete, Ngassa na Henry Joseph ambao walilisogelea kwa karibu lango la Simba wa Teranga lililokuwa likilindwa na Mamadou Ba.
  Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Stars wakitafuta namna ya kupata bao la kusazisha kwa kujipanga vizuri zaidi.
  Lakini vijana hao kutoka Tanzania waliendelea kukosa nguvu katika kiungo na mbinu za kuipenya ngome ya Senegal iliyokuwa imejengwa na wachezaji warefu.
  Mfumo wa kutumia mipira mirefu ulishindwa kufanya kazi mbele ya safu hiyo ya ulinzi.
  Stars ilibadilika na kutuliza mpira chini, lakini 'kuwekwa chini ya ulinzi' kwa winga wake, Ngassa kulipunguza makali ya mbinu hiyo.
  Benchi la ufundi la Stars lilifanya tena mabadiliko kwa kumtoa Tegete na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Abdi Kassim 'Babi' katika dakika 57.
  Mabadiliko hayo yaliongeza ari kwa Stars kusaka bao la kusawazisha lakini ngome ya Senegal iliendelea kuwa makini na kukataa kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
  Katika mchezo huo, Stars pia ilifungwa nje ya uwanja kutokana na kuwa na mashabiki wachache tofauti na Senegal ambao walikuwa wengi na kuzima kabisa shangwe za Watanzania hao uwanjani.
  Hadi filimbi ya mwisho Stars ilitoka vichwa chini kwa bao hilo moja.
  Katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa mjini hapa, wenyeji Ivory Coast waliwatoa vichwa chini mashabiki wao baada ya kukung'utwa mabao 3-0 na Zambia.
  Mshambuliaji mahiri wa Zambia 'Chipolopolo', Given Singuluma alipiga 'hat-trick' katika mchezo huo na kuipa ushindi timu yake.
  Stars itarejea tena uwanjani kesho kutwa Jumatano kwa kumenyana na Ivory Coast katika mchezo utakaoamua mustakabali wa timu hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: STARS YALALA KWA SENEGAL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top