• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 21, 2009

  FRANCIS LUCAS HATUNAYE DUNIANI

  Francis Lucas mwenye kapelo, akiwa na Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega enzi za uhai wake. Hapa wanazungumza na Waandishi wa Habari.  KATIBU Mwenezi wa klabu ya soka ya Yanga, Francis Lucas Mtamod, 39, amefariki dunia jana, akiwa nyumbani kwake, Tabata jijini Dar es Salaam kwa ugonjwa wa malaria.
  Mwenyekiti wa klabu hiyo, Imani Madega, alithibitisha kutokea kwa msiba huo na kusema mipango ya mazishi ilikuwa bado inafanywa kwa kusubiri ndugu wa marehemu.
  “Ni kweli mwenzetu ametutoka, taarifa tulizonazo ni kwamba alikuwa akisumbuliwa na malaria na alipata kulazwa kwa muda wa siku nne katika hospitali ya Amana na baadaye aliruhusiwa kurudi nyumbani. Alifariki usiku wa kuamkia leo (jana),” alisema Madega.
  Kabla ya kupata nafasi ya kuitumikia Yanga, marehemu pia alikuwa mwandishi wa habari na mpiga picha mkongwe wa magazeti mbalimbali nchini, kazi ambayo kwa mara ya mwisho, aliifanya akiwa na kampuni ya Habari Corp, inayochapisha gazeti hili, Septemba 2007.
  Francis alizaliwa Agosti 11, 1969, Raha Leo huko Lindi, ambako pia alipata elimu yake ya msingi kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Azania katika ya mwaka 1988-1991. Baadaye, alipata mafunzo ya awali ya uandishi wa habari katika Chuo cha TSJ Agosti, 1995.
  Alianza kufanya kazi ya uandishi na upigaji picha katika gazeti la Mfanyakazi, Motomoto na hatimaye Habari Corp.
  Mwaka 1997, aliwahi kupata tuzo ya mpiga picha bora wa mwaka, iliyotolewa na Chama cha waandishi wa habari za michezo na burudani, TASWA kwa udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania, TBL.
  Wakati huo huo, klabu hiyo imepata pigo jingine, baada ya mwanachama wake, ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tawi la Yanga huko Mtoni, Seif Mpipa, kufariki dunia jana alfajiri.
  Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka kwa mwanachama mmoja wa klabu hiyo, zilisema marehemu, aliyekuwa akisumbuliwa na homa, alitarajiwa kuzikwa jana huko huko Mtoni. Mungu awalaze marehemu mahali pema peponi. Amina.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: FRANCIS LUCAS HATUNAYE DUNIANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top