• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 09, 2009

  MADEGA NA KAULI ZAKE YANGA


  MWENYEKITI wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Wakili Imani Madega amakuwa na mvuto wa kipekee kutokana na kauli zake mbalimbali ambazo amekuwa akitoa tangu ameingia madarakani Mei 30, mwaka 2007.
  Katika toleo hili, DIMBA tumekusanya baadhi ya kauli zake na kuziorodhesha kama kauli za kukumbukwa alizowahi kutoa wakili huyo wa kujitegemea katika kipindi chake cha kuwa madarakani Yanga. Endelea…

  ALIVYOMSUTA MFADHILI MANJI:
  “Habari hizo alizosema Manji juu ya uongozi wangu ni uongo mtupu, ukweli ni kwamba ujio wa Manji ndani ya Yanga unaonekana kama ni ukombozi wa kifedha, lakini ukweli ni kuwa amekuja kwa lengo moja tu, la kuiangamiza klabu ya Yanga kabisa na hatimaye kuunda kampuni ambayo kinadharia yeye ndio atakayekuwa mmiliki mkuu.” Kauli hii aliitoa Oktoba 11, mwaka 2007 baada ya kutokea kutoelewana kati yake na mfadhili wa klabu hiyo, Yussuf Manji.

  ALIVYOWAPA VIDONGE WAZEE WA YANGA
  “Mwisho nasema kuwa sitokuwa tayari kuiona Yanga ikiuzwa na kutawaliwa na mtu mmoja kwa nguvu ya pesa, masikini na mwanawe, tajiri na mali zake, Manji baki na mali zako au heshimu Katiba. Vinginevyo baki na mali zako au fadhili timu nyingine. Wazee na wanachama wachache waroho wa Yanga kuweni macho na msiwasaliti wazee wenzenu ambao walifanya juhudi kuifanya Yanga iwe na jina kubwa, mkiendelea kufanya hivyo kwa hakika historia itawahukumu, uongozi uko imara kutetea maslahi ya Yanga,”. Kauli hii, pia aliitoa Oktoba 11, mwaka 2007, kutokana na wazee na wanachama wa klabu hiyo kumuunga mkono Manji katika mgogoro wake na Madega.

  MWISHO WA SIKU, ALIWAPIGIA MAGOTI:
  “Tofauti zilizojitokeza kati yangu na mfadhili Yussuf Manji zimekwisha na ameniandikia barua kuwa ataendelea na ufadhili na Yanga. Kwa upande wangu napenda kuwataka radhi wale wote niliowakosea kwa matamshi yangu, hususani wazee wangu wa Yanga. Kwa sasa Yanga ni moja na tushirikiane pamoja ili kufanikisha ushindi wa mechi zetu zilizobaki na hasa ile ya kuwashinda watani zetu wa jadi tarehe 24/10/2007,”.
  Kauli hii aliitoa Oktoba 17, mwaka 2007 mjini Dar es Salaam kuomba radhi kutokana na kauli zake alizotoa hapo juu dhidi yao.

  BAADA YA KUFUNGWA NA SIMBA MOROGORO:
  “Kwa mawazo yangu, fedha hizo zilitolewa (na Manji) kwa lengo la kutugombanisha. Wachezaji wetu walicheza chini ya kiwango kwa kutambua kuwa wanavuja jasho, lakini fedha wanapewa wengine wasiowajibika uwanjani,”.
  Kauli hii aliitoa Oktoba 26, mwaka 2007 akijibu kauli ya Yussuf Mzimba, aliyeutaka uongozi wake kueleza jinsi ulivyotumia shilingi milioni 40 zilizotolewa na mfadhili wao, Yussuf Manji kwa ajili ya kuhakikisha timu hiyo inawafunga watani wao wa jadi, Simba Oktoba 24 mwaka huo mjini Morogoro. Manji pia aliwapa Sh. Milioni 10, wazee wa klabu hiyo chini ya Mzimba, lakini Yanga ililala 1-0, kwa bao pekee la Ulimboka Mwakingwe.

  SIMBA ILIPOJITOA TUSKER:
  “Suala la kuchagua Uwanja halikuwa la Simba, naona hawa Kiingereza kimewapiga chenga kwani katika kanuni ya tatu tu (ya mashindano) inaonyesha watakaofanya uteuzi huo (wa Uwanja), tena kwa makubaliano tu, na yatafanyika katika Uwanja mmoja tu,”.
  Kauli hii aliitoa Julai 29, mwaka 2007 baada ya Simba kujitoa kwenye Kombe la Tusker, mwaka huo iliyofanyika mjini Mwanza. Madega aliongeza kuwa Simba wameonyesha kitendo kibaya kwa kujitoa kwenye michuano hiyo baada ya kushindwa kwa shinikizo lao la kutaka utumike Uwanja wa Jamhuri na nyongeza ya fedha za maandalizi.

  YANGA ILIPOIKACHA SIMBA KAGAME:
  “Tulikubaliana pande zote (Simba na Yanga), kuwa tutapeleka timu (Uwanja wa mpya wa Taifa) mara baada ya kutekelezewa matakwa yetu (ya mgawo wa mapato ya milangoni), lakini nimeshangaa kuona wenzetu (Simba) wamebadilika, tunajua kulikuwa na namna ambayo ingetumaliza,”.
  Kauli hii aliitoa Julai 28, mwaka jana, baada ya Yanga kutotokea uwanjani kucheza mechi ya kutafuta mshindi wa tatu katika michuano ya Kombe la Kagame, Julai 27, mwaka jana. Aliongeza kuwa kilichowafanya Simba wakiuke makubaliano ni njaa, ambayo inaweza kuwapeleka pabaya kama hawatakuwa na msimamo katika maamuzi yao.

  YANGA ITASHIRIKI LIGI KUU TU:
  “Kwa sasa tumeamua kwamba, michuano pekee ambayo tutaendelea kushiriki na kuiheshimu ni ligi yetu ya hapa nyumbani, namaanisha Ligi Kuu ya Vodacom (Tanzania Bara),”.
  Kauli hii aliitoa Agosti mwaka jana baada ya klabu hiyo kupunguziwa adhabu na Kamati ya Nidhamu ya TFF, kutoka kufungiwa miaka miwili kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Afrika hadi kutozwa faini ya dola za Kimarekani 20,000.

  BAADA YA AZIMIO LA BAGAMOYO:
  “Kozi ni nzuri, nimebaini kuna udhaifu mkubwa katika uendeshaji, nitajitahidi katiba ya Yanga iendane na ya FIFA na TFF, nimefahamu jinsi ya kuongoza wanachama wangu, masuala mazima ya mgawanyo wa kazi, sio utaratibu uliopo sasa Mwenyekiti ndio anafanya kazi zote,”.
  Kauli hii aliitoa mjini Bagamoyo Novemba 18, mwaka 2007 wakati wa kufunga kozi ya siku tano ya utawala bora na uongozi iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa ajili ya viongozi wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

  ALIPOITOLEA UVIVU TBL:
  “TBL haina uwezo wa kuiingilia Yanga kwa kututaka tuajiri Katibu Mkuu, makubaliano yetu ni kuajiri Mweka Hazina na tunatarajia kutangaza nafasi ya kazi wakati wowote kuanzia sasa, atakayetimiza vigezo tutamuajiri. Haya mambo si ya kukurupuka, nafasi kama ya Katibu Mkuu ni nyeti ambayo mshahara wake hauwezi kuwa Sh200,000, hapa tutaongelea milioni kadhaa, sasa bila kujipanga tutawezaje kumlipa?”
  Kauli hii aliitoa Oktoba 3, mwaka jana, kufuatia agizo la wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kuwataka waajiri watendaji kama ambavyo mkataba baina yao unaelekeza.

  SUALA LA NGASSA KWENDA NORWAY:
  “Najua bado kuna watu ambao wanaamini viongozi tumemzuia Ngassa (Mrisho) kujiunga na timu hiyo (Lov-ham ya Norway), lakini si kweli kwani haiwezekani wakala akawa anazungumza na vyombo vya habari tu bila sisi kujua,”.
  Kauli hii aliitoa Januari 27, mwaka huu kuhusu kiungo wa pembeni wa klabu hiyo, Mrisho Khalfan Ngassa kutakiwa na klabu ya Lov-ham ya Norway.

  SUALA HILO HILO LA NGASSA…
  “Kamati ya utendaji itakaa kulijadili suala hilo na baadae kulitolea maamuzi, kuna haja ya kuangalia umuhimu wa mchezaji huyo kwenye timu yetu ambayo inakabiliwa na michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, ambapo kama tutakubali kirahisi kuruhusu wachezaji, itawawia vigumu kufanya vizuri kwenye michuano hiyo,”.
  Kauli hii aliitoa Januari 28, mwaka huu alipokuwa akizungumzia suala la kiungo wa pembeni wa klabu hiyo, Mrisho Ngassa anayetakiwa na klabu ya Lov-ham ya Norway.

  KOCHA WA VIJANA ALIPOTUA DAR:
  "Atazunguka kutafuta wachezaji atakaoona wanafaa, kuanzia wale wenye umri kati ya miaka 12 na 14 na atakuwa na wakati mzuri kuwatengeneza,”.
  Kauli hii aliitoa Januari mwaka jana baada ya kuwasili mjini Dar es Salaam kwa kocha Civojnov Serdan, Mserbia aliyeelezwa anakuja kutengeneza timu za vijana ndani ya klabu hiyo. Hata hivyo, kocha huyo amejumujika na Profesa Dusan Kondic na Spaso SokoloVski katika timu ya wakubwa, hafundishi timu yoyote ya vijana.

  YANGA YAWEZA KUISHI KWA VIINGILIO:
  “Lakini pia ni vyema watu, hasa wanachama wa Yanga wakafahamu kwamba, mtoto huzaliwa na kukua, huwezi kutegemea kusaidiwa kila siku. Manji amefanya vitu vingi sana kwa klabu hii. Ametulea katika kipindi kigumu, wakati Uwanja wa Taifa ulipokuwa umefungwa, tulichezea Morogoro ambako fedha za kiingilio zilikuwa ni chache. Sasa tumehamia Dar es Salaam, timu inafanya vizuri mashindano ya ndani na nje, wanachama wanahamasika kuja kuishangilia na fedha zinapatikana. Tunaweza kusimama wenyewe,”.
  Kauli hii aliitoa Februari 3, mwaka huu akizungumzia mustakabali wa klabu hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MADEGA NA KAULI ZAKE YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top