• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 26, 2009

  YANGA WATUPIWA VIRAGO LAMADA

  WACHEZAJI wawili wa kimataifa wa Kenya wanaochezea Yanga, Boniface Ambani na George Owino, wametishia kuondoka nchini leo kurejea kwao, baada ya kufukuzwa Lamada Hotel walipokuwa wanakaa.
  Wakizungumza hotelini hapo jana mchana, wachezaji hao walisema waliwasili mjini Dar es Salaam juzi, lakini wakashangazwa na amri ya kutakiwa kuondoka hotelini hapo, kwa madai kuwa uongozi wa klabu hiyo ulikuwa haujalipa fedha za pango.
  BINGWA lilidokezwa mapema kwamba wachezaji wa klabu hiyo, inayojiandaa kwa mechi ngumu dhidi ya Al Ahly, wanafukuzwa hotelini hapo, ambapo wamekuwa wakikaa kwa muda mrefu.
  Baada ya kufika na kuomba kuonana na meneja wa hoteli, baadhi ya wafanyakazi wa Lamada hotel walianza kujizungusha kuonyesha anakopatikana, lakini mchezaji wa kwanza kukutana na gazeti hili, Mkenya Mike Baraza alipoulizwa kama kuna suala la kufukuzwa, alikubali na kukataa kuongea zaidi.
  “Ni kweli tumefukuzwa, sijui ninapokwenda,” alisema Baraza, akiwa amebeba begi lake, akiondoka katika chumba alichokuwa anakaa na kuelekea kujiunga na wenzake waliokuwa wamekaa sehemu ya wazi karibu na mapokezi.
  Awali, kiongozi mmoja wa hoteli hiyo, alikataa kuhusu madai ya kufukuzwa kwa wachezaji hao, akidai uongozi wa Yanga ulikuwa umewapangishia nyumba nyingine sehemu za Mikocheni, hivyo walikuwa wanaondoka katika hali ya kawaida na si kufukuzwa.
  “Nyumba? Nyumba gani! Haya basi kuna nyumba, hivi sisi wachezaji wa kulipwa tupo zaidi ya kumi tukakae katika nyumba ya vyumba vinne? Sisi siyo wakimbizi, kesho narudi zangu nyumbani,” alisema Ambani, mpachika mabao anayeongoza kwa mabao ligi kuu Tanzania Bara.
  Owino, kiungo wa ulinzi wa timu hiyo, alisema anashangazwa na uongozi wa Yanga, kwani alipowasili nchini juzi, alinyimwa chakula hotelini hapo na alipowatafuta viongozi wake, simu zao ziliita bila kupokelewa.
  “Nimekuja jana sijakula, nampigia simu Mpangala (Emanuel, Katibu Kamati ya Mashindano Yanga) hapokei, Katibu naye (Lucas Kisasa) hapokei, mimi nina kipaji bwana, kesho naondoka narudi zangu nyumbani, tutatafuta timu nyingine,” alisema.
  Kipa mzungu wa Yanga, Obrien Curcovick, alionekana kuchanganyikiwa wakati akipakia mizigo yake katika teksi akiwa katika uelekeo ambao haukufahamika.
  Alipotakiwa kusema chochote, alikataa. “Sina cha kusema, nimechanganyikiwa,” alisema kwa ufupi.
  Katika hoteli hiyo, wachezaji wa Yanga wanaoishi hapo licha ya hao wanne, pia yupo Maurice Sunguti, Ben Mwalala na mchezaji aliyetajwa kwa jina la Ambroso, anayechezea kikosi cha pili cha mabingwa hao wa Tanzania.

  CHITETE AAGA DUNIA

  RAIS wa Shirikisho la soka Tanzania, TFF, Leodgar Tenga, jana aliwaongoza mamia ya waombelezaji kuuaga mwili wa winga wa zamani wa Taifa Stars, Leonard George Chitete, shughuli iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, lililopo hospitali ya taifa Muhimbili, mjini Dar es Salaam.
  Wengine waliokuwepo katika kuuaga mwili huo, ni pamoja na baadhi ya wachezaji wengine wa zamani waliocheza pamoja na marehemu, akiwemo Kitwana Manara ‘Popat’ na Gessani Awadh. Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan ‘Zungu’ naye alikuwepo.
  Marehemu Chitete aliyefariki Jumatatu asubuhi, alitarajiwa kuzikwa jana katika makaburi ya Kinondoni.
  Dada wa marehemu, Maclean Chitete, alisema kaka yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa zaidi ya miaka sita na siku mbili kabla ya kufariki, hali yake ilibadilika na kuwa mbaya, ndipo alipokimbizwa hospitalini hapo.
  Maclean, ambaye pia alikuwa mcheza netiboli nyota enzi zake, alisema marehemu ameacha mke na watoto sita, waliompatia wajukuu wanne. Chitete, mwenyeji wa Mbambabay wilayani Mbinga mkoani Ruvuma alizaliwa Mei 10, 1947 na licha ya Taifa Stars, pia alikuwa winga tegemeo wa Yanga na Pan African.
  Wakizungumza hospitalini hapo, Popat na Gessan walimsifu mchezaji mwenzao huyo wa zamani na kusema alikuwa hatari, mbunifu na aliyekuwa msaada mkubwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WATUPIWA VIRAGO LAMADA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top