• HABARI MPYA

  Jumanne, Februari 03, 2009

  SIMBA KUMTOA BURE NAFTALI ULAYA

  KLABU ya Simba ya Dar es Salaam imesema ipo tayari kumuachia beki wake chipukizi, David Naftali, aende kukomazwa na klabu moja ya Ubelgiji, ambayo imekunwa na kipaji cha mchezaji huyo.
  Pamoja na kuivutia klabu hiyo, beki huyo aliyejaribiwa na klabu hiyo nchini Dubai alipokwenda kukutana nayo mapema mwezi uliopita, hakuchukuliwa kwa sababu hajakamilika kuwa mchezaji wa kulipwa.
  Akizungumza na DIMBA juzi mjini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kassim Dewji, alisema kilichomfanya chipukizi huyo kukosa nafasi ya kusajiliwa na timu hiyo, licha ya kuonyesha uwezo mkubwa, ni kukosa kwake uzoefu wa kutosha katika mikiki mikiki ya soka la Ulaya.
  “Walichosema wale jamaa ni kwamba Naftali ni mzuri na ana uwezo, lakini kama tunataka tumruhusu mchezaji huyo akakae na timu hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja ili aweze kukomaa na baada ya muda huo, ndipo utaratibu wa kuuzwa ufanywe.
  “Kama wao watamhitaji au watamuuza katika klabu nyingine, tutajua wakati huo. Lakini habari kwamba kulikuwa na wakala aliyetaka dau kubwa siyo kweli, mimi ndiye ninayehusika na uuzwaji wa wachezaji wa timu yetu nje, kabla wakala hajaamua lolote ni lazima awasiliane na sisi kwa maslahi ya klabu,” alisema Dewji.
  Naftali, pamoja na mchezaji mwingine wa timu hiyo, Mnigeria Emeh Izuchukwu, walikwenda kufanya majaribio kwenye timu hiyo iliyokuwepo ziarani Uarabuni. Katika mazoezi hayo, Naftali alionekana kuwavutia wazungu hao walioonyesha nia ya kumchukua.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA KUMTOA BURE NAFTALI ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top