• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 21, 2009

  PHIRI: DIDA SIO SIMBA ONE

  KOCHA Patrick Phiri wa Zambia, anayeinoa Simba, amesema licha ya mlinda mlango wake, Deogratius MuNIshi ‘Dida’ kuwamo katika timu ya Taifa Stars, yeye bado hajapata golikipa chaguo namba moja kikosini mwake.
  “Nilikuwa siwafahamu hawa magolikipa wengine, lakini Dida anaonekana bado mdogo. Wote nimewajaribu na wameonyesha uwezo, ila bado sijampata wa kuweza kuwa namba moja.
  “Wanaonyesha mwelekeo na kama wataendelea hivi, hadi mwisho wa msimu huu, nitakuwa nimempata wa kuanza kikosini,” alisema Phiri, wakati akielezea mikakati ya maandalizi kwa ajili ya mechi zilizobaki za ligi kuu Tanzania Bara.
  Alisema anatarajia kuanza mazoezi kesho katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe na wachezaji watafanya mazoezi wakitokea majumbani mwao, lakini baada ya wiki moja, wataelekea kambini tayari kwa kinyang’anyiro hicho.
  “Unajua nina wachezaji saba katika timu ya taifa (hata hivyo Jabir Aziz ameachwa) iliyosafiri kwenda Ivory Coast. Kwa hiyo nitaanza na hawa waliopo katika kuwajenga. Sina wasiwasi na wale waliopo Taifa Stars kwa sababu wanapata mazoezi ya kutosha huko waliko.
  “Lengo letu ni kuhakikisha tunaichukua nafasi ya pili, iwe isiwe. Nilipokuja mwezi mmoja uliopita, timu ilikuwa katika nafasi ya sita, lakini sasa ipo nafasi ya tatu, ni maendeleo makubwa.
  “Hata katika uchezaji wa kawaida, wameimarika sana kwa kipindi chote ambacho nimekuwa nao. Kila mmoja ana ari na hii inanipa moyo sana,” alisema Phiri, aliyewahi pia kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Zambia, Chipolopolo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PHIRI: DIDA SIO SIMBA ONE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top