• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 09, 2009

  HUYU NDIYE MRISHO KHALFAN NGASSA...  Na Florian Kaijage
  KWA muda wa takribani wiki mbili sasa, jina la Mrisho Khalfan Ngassa (pichani kulia) limekuwa likigonga vichwa mbalimbali vya vyombo vya habari nchini hususani magazeti na vituo vya redio. Na kugonga huko kwa jina la Ngassa katika vyombo vya habari katika kipindi hiki hakukutokana hasa na kazi aliyofanya uwanjani na kuwafanya mashabiki washindwe kukaa vitini, bali ni kwa sababu ya harakati za kubadili mwajiri kwa nia ya kupata masilahi bora zaidi katika kazi yake ya kusakata kandanda. Yote hayo yalianza na hatimaye kushika kasi na gumzo kutapakaa kila kona baada ya kufahamika kwa taarifa kuwa kijana huyo anahitajika ilisajiliwe na klabu moja ya Lov ? Ham ya Norway iliyopo daraja la kwanza nchini humo ? siyo daraja la pili kama ilivyokuwa ikitangazwa au kuripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari huku ikielezwa kuwa klabu hiyo ilikuwa tayari kulipa ada ya uhamisho ya dola za Marekani 50,000 kwa klabu ya Yanga na kwamba mshahara wa mchezaji huyo kwa mwezi ungefikia dola za Marekani 10,000 kwa mwezi (Sh milioni 12) Bila kuzingatia maoni yaliyotolewa kuhusu suala la Ngasa kuelekea Norway lilivyoshughulikiwa au litakavyoendelea kushughulikiwa ? maana bado halijamalizika - kwa kipimo chochote kile hizi ni habari njema kwa mpira wa Tanzania na habari ambazo hata wale ambao si manazi wa mpira wa miguu wangependa kuzisikia na hivyo kuufanya mpira kuzidi kuleta maana halisi ya taasisi yenye fursa za kuwatoa wanaojihusisha nayo hasa wachezaji kutoka hatua moja ya mendeleo hadi nyingine na kufanya maisha yao kuwa bora hasa kwa wale wa hapa nchini. Ndiyo, wale wa hapa nchini kwani kwa wengine hili si habari tena kwani yaliyoelezwa hapo juu yamezoeleka lakini kwa hapa nchini bado haijasikika mchezaji anayepokea mshahara ambao hata Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayoheshimika hawezi kuthubutu kufikiria kuupata pamoja na vyeti vya shahada na wasifu vinavyoweza kujaza sanduku ikiwa vitawekwa pamoja ? tena hiyo mishahara mingine ni ya wiki tu ? ni vema vijana wetu wakafika huko. Na hiki ndicho kigezo kimojawapo kitakachoendelea kuufanya mchezo wa mpira wa miguu kuwa wenye hadhi ya hali ya juu kiasi cha kuendelea kuwa na wapenzi wengi kuliko mchezo mwingine wowote. Lakini wakati Ngasa anaonekana kuwa katika njia nyoofu kuelekea Norway au katika nchi zilizopiga hatua kubwa zaidi katika maendeleo ya mpira wa miguu nami binafsi nikimuombea afanikiwe katika harakati zake hizo na kuitangaza Tanzania, ni bora kujiuliza hivi huyu Mrisho Ngasa ni nani na kitu gani kinachomfanya aonekane kuwa mchezaji wa daraja la juu miongoni mwa wale waliopo nchini? Ngasa amefanya nini Timu za taifa kwa klabu yake ya Yanga aliko sasa na kwingine alikowahi kupita? Je maswali hayo yana majibu yakini yanayomfanya Ngassa kuwa bora au ni ngekewa na pengine upendeleo tu kiasi cha kuteka vichwa vya habari? Hili ndilo hasa msingi ya yale yaliyomo ndani ya safu hii ili Watanzania wafuatiliaji na hasa wale wasiofuatilia kwa karibu masuala ya soka waweze kufahamu hazina ambayo Tanzania inayo ndani ya Ngasa. Historia na utumishi kwa Taifa Stars Kumbukumbu rasmi zinaonesha kuwa Mrisho Khalfan Ngasa alizaliwa Aprili 12 1989 mjini Mwanza. Ni mtoto wa Khalfa Ngasa, kiungo wa zamani wa Pamba, ya Mwanza timu iliyewahi kutamba ndani na nje ya Tanzania, Simba ya Dar es Salaam na Taifa Stars. Miongoni mwa vijana aliocheza nao mpira tangu umri mdogo huko Mwanza ni pamoja na Jerson Tegete, kiungo wa Simba Henry Joseph na mlinzi wa Simba Kelvin Yondani. Mrisho Ngassa kwa sasa ni moja ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha kocha wa Taifa Stars, Mbrazili Marcio Maximo kutokana na mchango mkubwa aliokwishatoa katika timu hiyo hadi sasa licha ya kutumikia timu hiyo kwa kipindi ambacho ni pungufu ya miezi 12. Ni sahihi kipindi alichotumikia timu za taifa za wakubwa 'Taifa Stars' na 'Kilimanjaro Stars' timu ya taifa ya Tanzania Bara ni chini ya mwaka mmoja. Ni rahisi mno kuhisi kuwa muda uliotajwa hapa umekosewa na sitashangaa mtu yeyote akiona hivyo na hapa ndio utakapojua umuhimu wa Ngassa kwani mambo aliyokwishayafanya katika kipindi hicho ni makubwa ikilinganishwa na muda wa utumishi wake. Ilimchukua Maximo muda mrefu kiasi kumjumuisha mchezaji huyo mwenye kasi katika kikosi chake licha ya kumuona mara kadhaa katika michezo ya Ligi Kuu Bara na michezo ya kimataifa akiwa Yanga. Mara zote alipokuwa akiulizwa sababu ya kutokumwita Ngassa kikosini, Maximo alikuwa akijibu kuwa alikuwa akimpa muda zaidi Ngassa ili aone kama 'usumbufu' aliokuwa nao dhidi ya walinzi akiwa Yanga angeuendeleza akiwa na Stars na kwamba asingependa kumwita mapema na kisha kumkatisha tamaa iwapo angeshindwa kuendana na mbinu za Mbrazili huyo ? hiyo kwa mujibu wa Maximo ingekuwa sawa na kuua kipaji cha Ngassa. Ngassa alivaa jezi ya Taifa Stars kwa mara ya kwanza Machi 29, 2008 mjini Nairobi wakati wa mchezo wa raundi ya kwanza wa harakati za kuelekea katika fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani zitakazofanyika Ivory Cost ambazo mwishowe Taifa Stars ilifanikiwa kufuzu. Katika mchezo huo Ngasa aliingia katika dimba la Nyayo katika dakika 65 na tangu wakati huo amecheza michezo 19 ya kimataifa akifunga magoli matatu kwa ustadi mkubwa. Magoli hayo ni dhidi ya Cape Verde kwenye mchezo wa Oktoba 11, 2008 jijini Dar es Salaam. Magoli mengine mawili aliyafunga katika Kombe la Chalenji dhidi ya Rwanda na dhidi ya Burundi. Kana kwamba hiyo haitoshi Ngasa amekwishatoa migongeo ya mwisho kumi iliyozaa magoli mbali mbali ya Taifa Stars huku akiwa amefanya kazi kubwa na ya kupigiwa mfano kabla ya kuwagongea wafungaji. Migongeo maridhawa miwili aliyompatia Jerson Tegete katika mchezo dhidi ya Mauritius na hatimaye Stars kushinda 4-1 ugenini, ule aliompatia pia Tegete na kuzaa goli la pili dhidi ya Cape Verde, pasi mbili alizowapatia Henry Joseph na Nurdin Bakari walioiua Sudan mjini Khartoum Desemba 13, 2008 zikitanguliwa ni ile kazi iliyozaa goli la kwanza katika ushindi wa 3-1 jijini Dar es Salaam Novemba 29 na krosi iliyotua kichwani mwa Emmanuel Gabriel na kuzaa goli la pili dhidi ya Waganda jijini Mwanza Mei 3, 2008 ni miongoni mwa kazi safi ambazo Ngassa amelifanyia taifa lake akishirikiana vema na wachezaji wengine ambao pia hawamuangushi. Na itakuwa si sawa kusahau mgongeo wa 'hatari' aliompatia Kigi Makasi na kuzaa goli pekee la mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Msumbiji Novemba 20 jijini Dar es Salaam na mipira miwili murua aliyompatia Danny Mrwanda akifunga dhidi ya Kenya katika nusu fainali na pia dhidi ya Burundi katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu katika Kombe la Chalenji mjini Kampala Januari 11 na 13, 2009. Alikuwemo pia katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana wa umri wa chini ya miaka 17 Serengeti Boys ambacho kilishiriki mashindano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika za mwaka 2005 na kufanikiwa kufuzu kabla ya CAF kuiondoa timu hiyo kwa makosa ya kiutawala juu ya utata wa umri wa baadhi ya wachezaji, lakini pia akawemo katika kikosi cha Bara kilichoshiriki michuano ya Chalenji mwaka 2006 nchini Ethiopia. Utumishi kwa klabu Akiwa amejiunga na timu ya Yanga mwishoni mwa mwaka 2006 akitokea klabu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera, Mrisho Ngasa amekuwa na msaada mkubwa kwa timu yake. Amechezea Yanga chini ya makocha wanne tofauti. Alipotoka Kagera alimkuta Jack Lroyd Chamangwana ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Soka cha Malawi (FAM) kabla ya kuwasili kwa kocha mweye makeke Sredojevic Milutin 'Micho' aliyeiongoza Yanga hadi kufika fainali ya Ligi Ndogo Bara na katika michezo ya Klabu Bingwa Afrika na hatimaye Kombe la Shirikisho, Mkenya Razak Siwa aliyepewa jukumu la kuiongoza timu katika Kombe la Tusker na sasa Dusan Kondic raia wa Serbia. Katika kile kinachothibitisha kuwa Ngassa ana uwezo mkubwa, hakuna kocha yeyote kati ya hao wanne aliyewahi kumwacha nje Ngassa kwa kipindi kirefu kwani hata walioamua kumpanga kama mchezaji wa akiba walifanya hivyo kwa kipindi kifupi tu. Micho kwa mfano alikuwa akimwanzishia benchi lakini kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele ndivyo alivyomjumuisha katika kikosi cha kwanza. Sababu kubwa ya kuazia benchi wakati huo ilitokana na kuwepo kwa mchezaji mzoefu Said Maulid (SMG) aliyekuwa anacheza nafasi ya pembeni kulia kama Ngassa. Lakini Micho alikuja kuona kuwa kijana huyo ni hatari pale alipomwingiza dimbani zikiwa zimesalia dakika 25 mpira kumalizika wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola jijini Dar es Salaam huku magoli yakiwa 0-0 na mashabiki wa Yanga wakiwa hawaelewi somo. Kijana huyo baada tu ya kuchukua nafasi ya Mmalawi James Chilapondwa alibadilisha kabisa kasi ya mchezo na Waangola wakashindwa kuhimiri vishindo kiasi cha kukubali kipigo cha 3-0, magoli yote yakifugwa ndani ya dakika 15 za mwisho na Ngassa akipachika moja nyavuni. Mengine mawili yalifungwa na Abdi Kassim na Shadrack Nsajigwa. Hivyo hivyo Siwa na Chamangwana walikuwa wakimtumia kama mchezaji wa akiba na mara chache aliweza kucheza dakika 90 wakati wa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2007/08. Hata hivyo, Kondic alipokabidhiwa mikoba kamili ya kuiongoza timu kuanzia raundi ya pili ya msimu huo, alimtumia kikamilifu huku akicheza michezo 11 kwa dakika 90 kati ya 13 ya raundi hiyo ya pili. Michezo mingie miwili hakucheza kabisa. Katika msimu huu wa Ligi Kuu 2008/09 Ngassa hakuanza vizuri sana kwani katika michezo mitatu ya kwanza hakuna hata mmoja ambao alianza, huku akicheza dakika 36 katika mchezo dhidi ya JKT Ruvu na dakika 39 dhidi ya Mtibwa Sugar. Baada ya hapo alicheza kwa dakika zote 90 katika mchezo dhidi ya Moro United, Villa Squad, Azam FC, Polisi Dodoma na Polisi Morogoro. Mchezo dhidi ya Siimba alichezo kwa dakika 84 huku akicheza dakika 35 na 37 kweye michezo dhidi ya Toto Africa na Kagera Sugar. Hata hivyo mzunguko wa pili ambao Yanga imecheza michezo mitatu tayari dhidi ya Tanzania Prisons, JKT na Mtibwa Ngasa amecheza michezo yote kwa dakika 90 na kufanikiwa kufuga goli moja huku magoli mengine mawili dhid ya Prisons na JKT akiwa ametoa pasi za mwisho kuwawezesha Shamte Ally na Athuman Idd kuziona nyavu. Alianza kucheza Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2006 akiwa na Kagera Sugar alikosajiliwa na Sylvestre Marsh mwishoni mwa 2005 akimtoa timu ya Channel Africa ya Mwanza. Alikuwa mmoja wa wachezaji waliofanikiwa kunyakua ubingwa wa Kombe la Tusker baada ya kuwafunga waliokuwa mabingwa watetezi Simba kwa magoli 2-1. Aliwahi pia kuichzea Toto Africa. Huyo ndio Mrisho Khalfan Ngassa ambaye mwishoni mwa wiki alifanya kazi kubwa walipocheza dhidi ya Etoile d?Or Mirotsy ya Comoro katika mchezo wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda kwa mabao 8-1.
  KAIJAGE NI OFISA HABARI WA SHIRIKISHO LA SOKA LA TANZANIA (TFF).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HUYU NDIYE MRISHO KHALFAN NGASSA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top