• HABARI MPYA

  Jumanne, Februari 03, 2009

  Wachezaji Yanga wajazwa malaki ya pesa

  Wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya mabao yao Jumamosi

  WACHEZAJI 18, waliovaa jezi katika mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kila mmoja amepewa Sh 280,000 kama posho ya mchezo huo, wakati ambao hawakuvaa, kila mmoja alipewa Sh 160,000.
  Kwa mujibu wa habari za ndani kutoka Yanga, ambazo DIMBA imezipata, kila mchezaji alipewa fungu lake Jumatatu, ikiwa ni siku mbili tangu waitandike Etoile d’Or Mirontsy ya Comoro mabao 8-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mabao ya Yanga kwenye mchezo huo, yalitiwa kimiani na Boniphace Ambani, aliyefunga manne, Jerry Tegete mawili, Mrisho Ngassa na Wisdom Ndholvu ambao kila mmoja alifunga bao moja.
  Kwa ushindi huo, Yanga imejiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele, Raundi ya Kwanza, ambako itakutana na mabingwa mara sita barani Afrika, Al Ahly (National) ya Misri.
  Wachezaji wa Yanga waliovaa jezi na kucheza siku hiyo walikuwa ni Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Amir Maftah, Wisdom Ndhlovu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Geoffrey Boniface aliyempisha Nurdin Bakari, Mrisho Ngasa, Abdi Kassim, Boniphace Ambani, Ben Mwalala aliyempisha Jerry Tegete na Kigi Makassy aliyempisha Vincent Barnabas.
  Ambao walivaa lakini hawakucheza ni Steven Marashi, Castory Mumbara, Shamte Ally na Nahodha Freddy Mbuna.
  Ambao hawakuvaa kabisa ni Obren Curkovic, Abubakar Mtiro, Hamisi Yussuf, George Owino, Athumani Iddi, Razack Khalfan, Ally Msigwa,
  Gaudence Mwaikimba, Maurice Sunguti, Mike Barasa na Iddi Ally Mbaga.
  Leo Yanga inatarajiwa kuhamishia makali yake kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzanjia Bara, wakati itakapomenyana na Moro United, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Katika mzunguko wa kwanza, Yanga yenye pointi 39, iliifunga Moro United mabao 2-1 kwenye Uwanja huo, kitu ambacho kitachochea kasi ya timu hiyo yenye pointi 15, ambayo ipo katika mstari wa kushuka daraja, kuweza kucheza kwa nguvu ya kuhitaji pointi tatu. Zote zimecheza mechi 14 hadi sasa.
  Itakuwa ni mechi ambayo Yanga itahitaji ushindi ili iweze kupumzika vyema kileleni, kwani itabakiza mechi mbili tu, kuweza kujiandikia historia ya kutwaa taji hilo mapema kabla ligi kumalizika.
  Kwa sasa Yanga ina pointi 39 na ili kujihakikishia ubingwa mapema kabla ya ligi kumalizika, inasubiri ushindi katika mechi zake tatu kuanzia leo, ili itimize 48, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.
  Baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na JKT Ruvu juzi mjini Dar es Salaam, Simba sasa inaweza kutimiza pointi 45 iwapo tu itashinda mechi zake zote zilizosalia, wakati Kagera inaweza kumaliza na pointi 47, Mtibwa 45 na Toto Afrika ya Mwanza 42 sawa na JKT.
  Moro ipo pointi moja tu mbele ya timu mbili za Polisi Morogoro na Villa Squad, zenye pointi 14 na chini kabisa ipo Polisi Dodoma yenye pointi saba.
  Endapo itapoteza mchezo huo, itakuwa na wakati mgumu kuweza kubakia ngazi hiyo, kwani ushindani wa timu zilizo hatarini kushuka daraja ni mkubwa kuliko hata zile zinazotaka ubingwa.
  Wakati Uwanja wa Taifa ukiwa katika vita hiyo, jijini Mbeya, wenyeji Prisons ambayo imepoteza michezo yake minne iliyopita, itacheza dhidi ya wakata miwa wa Turiani, Mtibwa Sugar, katika mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkubwa.
  Mtibwa yenye pointi 21, itawania kushinda ili iweze kuwemo katika kinyang’anyiro cha nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, huku Prisons, yenye jukumu la kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, ikiwa na pointi 19, nayo itapigana kuwemo katika orodha ya timu zinazoitaka nafasi hiyo na wakati huo huo, kukaa mbali na mstari unaokaliwa na timu zenye hatari ya kushuka daraja.
  Prisons ina historia nzuri na uwanja wake wa nyumbani wa Sokoine, ingawa imekuwa haina meno inapocheza ugenini, kitu kinachoiongezea nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi wake wa kwanza leo ndani ya mechi tano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: Wachezaji Yanga wajazwa malaki ya pesa Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top