• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 05, 2009

  YANGA BADO POINTI SITA KUTANGAZA UBINGWA

  BAO la mshambuliaji wa Taifa Stars, Jerry Tegete (pichani juu), lilitosha kuisogeza klabu yake ya Yanga kwenye ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kuinyuka Moro United katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.
  Ushindi huo umewafanya mabingwa hao watetezi kushinda mchezo wao wa nne mfululizo huku ikikataa nyavu zake kuguswa tangu kuanza kwa duru la pili la michuano hiyo.
  Tegete alifunga bao hilo katika dakika 57 akimalizia vyema kazi maridadi ya Mkenya Michael Barasa, ambaye alimpasia winga mahiri Mrisho Ngassa aliyewapiga chenga wachezaji kadhaa wa Moro United na kutoa pasi kwa mfungaji.
  Ushindi huo wa vijana wa Dusan Kondic umekuwa 'kiduchu' baada ya wiki iliyopita kuitikisa soka ya Afrika kwa kuikamua Etoile d'0r Mirontsy ya Comoro mabao 8-1 katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika.
  Yanga inazidi kupaa kwenye kinyang'anyiro cha ligi hiyo baada ya kujikusanyia pointi 42, ikiwa mbele ya Kagera Sugar inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 16 na pointi 18 dhidi ya mahasimu wao Simba waliojikita katika nafasi ya tatu.
  Moro United imebaki na pointi 15 ikiendelea kusota katika nafasi ya tisa ya msimamo wa ligi hiyo yenye timu 12.
  Hata hivyo kocha wa Moro United, Fred Minziro, baada ya mchezo alilalamikia bao hilo, akisema halikuwa halali akimtuhumu mwamuzi, Oden Mbaga, kwa kukosa umakini.
  Licha ya kutoka uwanjani vichwa chini, Moro United ilionyesha kandanda safi kipindi cha pili huku nyota wake, Amri Kiemba, Nizar Khalfan na Samwel Ngassa wakiipa shida safu ya ulinzi ya mabingwa hao wa Bara.
  Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliotarajia kufanyika jana baina ya maafande wa Tanzania Prisons ya Mbeya na Mtibwa Sugar ya Manungu, Morogoro mchezo huo umesogezwa mbele kwa siku moja na sasa utafanyika leo.
  Prisons iliomba mchezo huo usogezwe kutokana na uchovu walionao baada ya kulambwa mabao 2-0 na Khalij Sert ya Libya katika mchezo wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumapili iliyopita.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA BADO POINTI SITA KUTANGAZA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top