• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 26, 2009

  SAKATA LA WACHEZAJI YANGA KUFUKUZWA HOTELINI, MADEGA ATOA UFAFANUZI


  Hii ndio nyumba waliyopangiwa wachezaji wa Yanga kutoka Kenya


  SIKU moja baada ya wachezaji wa kigeni wa Yanga kutimuliwa katika hoteli waliyokuwa wakiishi, Lamada iliyopo Ilala mjini Dar es Salaam, uongozi wa klabu ya hiyo umesema wachezaji hao walipaswa kuhama mapema ila waligoma.Juzi, wachezaji Ben Mwalala, Boniface Ambani, George Owino, Maurice Sunguti, Boniphace Ambani na Mike Barasa walitimuliwa kwenye Hoteli ya Lamada, Ilala, baada ya uongozi wa hoteli kuwaambia kama wanataka kuishi pale basi wajilipie.Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega, alisema wachezaji hao waligoma kuhamia kwenye nyumba waliyopangiwa Sinza jijini na badala yake kutaka kuendelea kuishi Lamada.Madega alisema Yanga hawako tayari kuyumbishwa na wachezaji hao raia wa Kenya na ndiyo maana uongozi uliweka mkakati na hoteli hiyo wa kuwaondoa hapo, mkakati uliofanikiwa.“Tulisitisha malipo tulipoona wanagoma kuhama. Hatuwezi kubembeleza wachezaji fulani wakati timu ni ya wachezaji wote waliosajiliwa,” alisema Madega, aliyechukizwa na tabia za wachezaji wageni.Walipoongea na gazeti hili juzi, wachezaji hao walisema hawakuwa tayari kwenda kuishi wachezaji 10 kwenye nyumba ya vyumba vinne.Hata hivyo, baadaye wachezaji hao waliotishia kurudi kwao, walifuata maelekezo na kuhamia Sinza.
  LIGI YA VIJANA TANZANIA...


  Ni Azam au Villa bingwa leo?  FAINALI itakayomtoa bingwa wa Ligi ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 inatarajiwa kufanyika kesho kati ya Azam FC na Villa Squad, kwenye Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa, Dar es Salaam.Miamba hao wamefuzu kuingia fainali baada ya kuwafunga Mtibwa na Polisi Morogoro kwenye michezo ya nusu fainali juzi.Azam waliichapa Mtibwa Sugar mabao 4-1, huku Villa wakiwabwaga Polisi kwa mabao 3-1.Azam, vijana wa jijini Dar es Salaam, wanaingia fainali wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja katika kundi la pili na kuziacha nyuma timu za Moro United, Prisons na Yanga, wakati Villa nao wakiwa vinara wa kundi la tatu.Mchezo huo unatarajiwa kuwa mkali, huku makocha wa timu hizo wakitambiana.Kocha wa Azam, Itamar Amokin, juzi alinukuliwa akisema kuwa ataibuka na ubingwa wa michuano hiyo kwa kuwategemea washambuliaji wake nyota, kina Sino Agustino na Kheri Habib, anayeongoza kwa ufungaji.Naye kocha wa Villa, Richard Mbuya, amekitambia kikosi chake akikiita cha mauaji.Bingwa wa michuano hiyo atajinyakulia zawadi ya kikombe na medali za dhahabu, mshindi wa pili akiondoka na medali za fedha na mshindi wa tatu akijipatia medali za shaba.Zawadi hizo zimetolewa na mdhamini wa michuano hiyo, Kampuni ya Bakhresa Food Product, kupitia maji ya Uhai na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodeger Tenga.

  Copa Coca Cola Songea mambo yaanza  CHAMA cha Soka Manispaa ya Songea (SUFA) kimeanza kugawa fomu za kushiriki michuano ya mwaka huu ya vijana chini ya miaka 17, maarufu kama Copa Coca Cola.Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Songea jana, Katibu wa Kamati ya mashindano hayo Manispaa ya Songea, Godfrey Mvula, alitoa wito kwa timu za soka za shule za sekondari na za mitaani kujitokeza kuchukua fomu hizo.Alisema ligi hiyo inaendeshwa kwa kufuata kalenda ya TFF na katika manispaa hiyo ligi hiyo itaanza kutimua vumbi kesho.Mvula alisema mashindano hayo ni muhimu kwa vijana, kwani huwapa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na baadaye kuchezea timu za wilaya, mkoa na baadaye kushiriki michuano hiyo katika ngazi ya taifa.Katika kuhakikisha zoezi hilo linakwenda kama ilivyopangwa, kamati ya michuano hiyo imepanga ada ya shilingi 35,000 kwa kila timu mshiriki ambazo zitatumika kuendeshea michuano hiyo.“Kwa mujibu wa kanuni na sheria za usajili, mchezaji atatakiwa kuonyesha cheti cha kuzaliwa kilichotolewa kisheria ili kuutambua umri wake,” alisema Mvula.Katibu huyo alitoa onyo kwa viongozi wa timu yoyote watakaofanya udanganyifu wa umri kwa wachezaji kwa lengo la kutafuta ushindi na kwamba timu hiyo itafutwa na kuondolewa katika michuano.Katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo ya michuano hiyo, ilibainika kuwa kulikuwapo na udanganyifu wa umri na kuwachezesha vijeba katika michuano ya vijana na kusababisha kuwapo kwa vurugu za mara kwa mara viwanjani.


  Timu ya Marekani yaja kucheza Dar

  TIMU ya soka ya Vancouver Whitecaps ya Ligi Daraja la Kwanza ya Marekani Kaskazini inayojumuisha timu kutoka nchi za Marekani na Canada, inatarajiwa kufanya ziara ya kimichezo nchini kuanzia Machi 6 hadi 18 mwaka huu. Akizungumzia ziara hiyo jana jijini Dar es Salaam, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, alisema ujio wa timu hiyo maarufu kutoka Marekani na Canada utasaidia kuitangaza Tanzania na mpira wa miguu katika nchi kubwa duniani.Alisema Tanzania itafaidika na ziara hiyo kwa kuzingatia ubora na viwango vya soka vya nchi hizo duniani, ambapo kwa taarifa ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambayo ilitolewaFebruari mwaka huu, Tanzania ipo katika nafasi ya 103, Canada nafasi ya 88 huku Marekeni ikiwa katika nafasi ya 20.Alisema Marekani inafahamika zaidi katika soka baada ya kufanikiwa kushiriki fainali za Kombe la Dunia mara nane tofauti na Tanzania ambayo kwa sasa inapigania kucheza fainazli za Kombe la Mataifa ya Afrika.“Hivi sasa kila mpenzi wa soka anazifikiria fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani huko Afrika Kusini hasa wale waliopo katika nchi zilizopo karibu na nchi hiyo mwenyeji ambazo zimekuwa zikijipanga kuhakikisha zinafaidika na fainali hizo,” alisema.Tenga alisema Tanzania imo mbioni kuangalia jinsi itakavyoweza kufaidika kutokana na fainali hizo kwa kuhakikisha inapata timu ambazo zitapenda kufanya mazoezi au kucheza mechi za kirafiki kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo pamoja na kupata mashabiki watakaopitia nchini kwa mapumziko na kujionea vivutio vilivyopo nchini.Alisema kuwa ikiwa nchini, Vancouver Whitecaps itacheza mechi tatu mojawapo ikiwa dhidi ya timu ya taifa, Taifa Stars.Rais huyo aliongeza kwamba, wakati wa ziara hiyo wachezaji na viongozi wa timu ya Vancouver Whitecaps watatembelea baadhi ya shule na kuzungumza na watoto kuhusiana na mchezo wa soka na ikiwezekana watafanya nao mazoezi katika kuhamasisha ari ya vijana hao kujiendeleza kimichezo.Hata hivyo, Tenga alitoa shukrani zake kwa serikali kutokana na msaada wake kuhakikisha ziara hii inafanyika pamoja na kuipongeza kampuni ya LZ Enterprises kwa kusimamia na kuratibu ujio wa timu hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAKATA LA WACHEZAJI YANGA KUFUKUZWA HOTELINI, MADEGA ATOA UFAFANUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top