• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 11, 2009

  NURDIN AELEKEZA SILAHA ZA KUIUA AHLY


  BEKI anayemudu kucheza kiungo pia, Nurdin Bakari Hamadi (PICHANI KULIA), amesema kwamba iwapo wataitoa Etoile d'O Mirontsy ya Comoro, watakuwa na kibarua kigumu mbele yao mbele ya mabingwa mara sita Afrika, Al Ahly ya Misri, hivyo watahitaji maandalizi makini.
  Akizungumza na DIMBA jana mjini Dar es Salaam, juu ya maandalizi ya mchezo huo, ameshauri kila upande ucheze vizuri katika idara yake, yaani kuanzia uongozi, makocha na wachezaji.
  "Viongozi lazima wajue kwamba, tunahitaji maandalizi mazuri, ikiwemo kucheza mechi angalau mbili au tatu dhidi ya timu za Uarabuni, lakini siyo Libya, nasema hivyo kwa sababu mpira wa Uarabuni unafanana, sasa tukicheza na timu za huko, itatusaidia sana kukusanya vitu kabla ya kukutana na hawa watu,"alishauri Nurdin.
  Zaidi ya hapo, Nurdin alisema kwamba Yanga msimu huu wana kikosi kizuri, lakini anachokiona kwa sasa ni kuelekeza nguvu nyingi kwenye Ligi Kuu, jambo ambalo ni zuri, lakini ameshauri michuano hiyo mikubwa Afrika, pia ipewe nguvu.
  Kwa upande wake, kiungo mwingine wa klabu hiyo, Vincent Barnabas Saramba, alisema kwamba duniani hakuna kitu kisichowezekana, hivyo Yanga kuitoa Al Ahly, inawezekana kabisa.
  "Mungu hajatuumbia kufungwa na Waarabu kila siku, watu lazima waelewe, Yanga ya sasa siyo ile waliyoizoea iliyokuwa inafungwa fungwa na Waarabu, Yanga ya sasa wachezaji wake wana uwezo mkubwa, na ninaamini tutaweka historia,"alisema.
  Kwa upande wake, kiungo mwingine wa klabu hiyo, Mrisho Khalfan Ngassa alisema kwamba, dhamira ya Yanga msimu huu ni ubingwa tu, tena yeye wala haumizwi kichwa kabisa na Waarabu hao.
  "Mimi sijisumbui kuwafikiria wapinzani, mechi yoyote ile tunakutana uwanjani, tutajuana huko huko, kama wao mabingwa wa Misri, sisi mabingwa wa Tanzania, sisi tunataka wao ndio watuhofie, siyo sisi tuwahofie wao,"alisema Ngassa.
  Yanga itakayorudiana na Etoile nchini Comoro Jumapili wiki hii, ikiwa na hazina ya mabao 8-1 iliyoshinda kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam, ikifuzu hapo itakutana na Ahly, mechi ya kwanza itachezwa Cairo, kati ya Machi 13 na 15 wakati marudiano yatakuwa Dar es Salaam kati ya Aprili 3 na 5.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NURDIN AELEKEZA SILAHA ZA KUIUA AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top