• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 25, 2009

  ABEBE BIKILA: MWAFRIKA WA KWANZA KUTWAA MEDALI YA DHAHABU OLIMPIKI


  ILIKUWA ni katika michuano ya Olimpiki ya mwaka 1960, mjini Rome, Italia wakati Abebe Bikila (pichani juu) alipoweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza kutwaa Medali ya Dhahabu kwenye michuano hiyo.
  Bikila alichaguliwa kwenye timu ya Ethiopia iliyoshiriki Olimpiki dakika chache kabla ndege iliyobeba kikosi cha timu kwenda Rome haijaondoka, alichukua nafasi ya Wami Biratu, ambaye aliumia kifundo cha mguu katika mechi ya mchezo wa soka.
  Meja Onni Niskanen aliwachukua Bikila na Mamo Wolde kwa ajili ya kukimbia mbio ndefu, zijulikanazo kama Marathon.
  Wadhamini waliotoa viatu kwa wanamichezo wa Olimpiki ya mwaka huo, walikuwa wamebakiza jozi chache hivyo Bikila alilazimika kwenda kuangalia kama atapata vya kumtosha na mwishowe akaambulia pea moja tu ambayo nayo pia haikuweza kumtosha vizuri.
  Kwa sababu hiyo, hakutumia viatu hivyo kwenye michuano hiyo na saa chache kabla yam bio hizo, iliamualiwa Abebe akimbia pekupeku.
  Bikila alionywa na Niskanen kuhusu wapinzani wake ambao mmojawao alikuwa ni Rhadi Ben Abdesselam wa Morocco, ambaye alitarajiwa kuvaa jezi namba 26.
  Kutokana na sababu ambazo hazikufahamika, Rhadi hakwenda kuchukua jezi aliyotakiwa na alisistiza kuvaa jezi yake ya kawaida namba 185.
  Baadaye kabisa mchana, zilipokaribia kuanza katika eneo la Arch of Constantine, nje ya Colosseum, mwanariadha wa Australia, Ron Clarke alizungumzia juu ya Bikila kukimbia pekupeku.
  Wakati wa mbio, Bikila aliwapita wakimbiaji kadhaa akitafuta mtu aliyevaa namba 26 na baada ya kilomita kama 20, Bikila alijikuta anachuana na mtu aliyevaa namba 185 wakiwa wanaachana kwa umbali mdogo mno.
  Lakini Bikila aliendelea kukimbia kumsaka huyo aliyevaa namba 26, ambaye alikuwa hamfahamu hata kwa sura hivyo hakujua kama ni mtu anayekimbia kulia kwake.
  Waliendelea kukimbia bega kwa bega hadi mita 500 za mwisho wakati Abebe alipoongeza kasi na kumaliza wakati mpinzani wake, Rhadi alimaliza sekunde 26 baadaye.
  Bikila alishinda kwa kutumia muda wa saa 2: dakika 15, sekunde16.2 na kuweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza kutwaa Medali ya Dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki.
  Baada yam bio hizo, wakati Bikila alipoulizwa kwa nini alikimbia bila viatu, alijibu: “Nilitaka dunia ijue kwamba nchi yangu Ethiopia hushinda kwa kujituma na ushujaa."
  Niskanen baadaye alipata taarifa kwamba, ikiwa Rhadi asingekimbia kwenye mbio za mita 10,000 siku chache kabla ya mashindano hayo, mbio hizo zingefutwa.
  Bikila alirejea Ethiopia kama shujaa na Wahabeshi walitamba kwa kusema; “Iliwachukua mamilioni ya Wataliano kuvamia Ethiopia, lakini askari mmoja wa Ethiopia aliiteka Rome,”.
  Mfalme wan chi hiyo, Haile Selassie alimpandiaha cheo hadi kuwa Koplo sambamba na kumzawadia Medali ya nyota wa Ethiopia.
  Muda mfupi baada ya michuano ya Olimpiki, Jeneral Mengistu Neway alipanga kufanya mapinduzi na Bikila, ambaye alikuwa haelewei lolote kuhusu siasa na pamoja na kushinikizwa kushiriki, mwanariadha huyo alikataa kuuwa walengwa na wakati jaribio la mapinduzi hayo liliposhindikana, wote waliohusika walipewa adhabu ya kifo.
  Lakini Bikila alisamahewa na Mfalme wa nchi hiyo, baada ya watu wengi kujitokeza kumuombea msamaha.
  Mwaka 1961 Bikila alikimbia Marathon nchini Ugiriki, Japan na katika Jiji la Kosice nchini Czechoslovakia, ambako kote alishinda.
  Kati ya Oktoba mwaka 1961 na Aprili 1963 hakukimbia kwenye mashindano yoyote ya kimataifa kabla ya kujitosa kwenye Boston Marathon ya mwaka 1963 abako alishika nafasi ya tano, hicho kikiwa kipindi kipekee alichoshiriki mbio hizo ndefu bila kushinda.
  Alirejea Ethiopia na hakushiriki mashindano yoyote hadi ilipowadia michuano ya Addis Ababa mwaka 1964, ambako alishiriki na kushinda kwa kutumia muda wa saa 2: dakika 23, sekunde 14.
  Siku 40 kabla ya michezo ya Olimpiki mwaka 1964 mjini Tokyo, japan, akiwa kwenye maandalizi, mjini Addis, Abebe Bikila alianza kusikia maumivu.
  Kutokana na kutojali juu ya maumivu hayo na kuendelea na mazoezi, alizimia na akakimbizwa hospitali ambako alikutwa na ugonjwa wa kidole tumbo na baada ya kutibiwa alijisikia vizuri. Alianza taratibu kukimbia kimbia kwenye eneo la hospitali.
  Katika michuano ya Olimpiki 1964, Abebe Bikila alikwenda Tokyo na ingawa kutokana na hali yake hakutarajiwa kukimbia, lakini alijitosa kwenye kinyang’anyiro safari hiyo akikimbilia viatu vya Asics. Alitumia mbinu ile ile ya mwaka 1960 kukaa na vinara hadi kilomita 20 kuelekea mwisho aliongeza kasi. Baada ya kilomita 15 alijikuta yupo na Ron Clarke wa Australia na Jim Hogan wa Ireland. Muda mfupi kaba ya kubakisha kilomita 20, alimpangua kwanza Hogan, baadaye Kokichi Tsuburaya wa Japan aliyekuwa nafasi ya tatu kabla ya kuingia kwenye Uwanja wa Olimpiki akiwa peke yake na kupokewa kwa shangwe na umati wa watu wapatao 70,000.
  Alimaliza mbio ndefu na kuweka rekodi mpya ya dunia, akitumia muda wa saa 2 dakika12, sekunde 11:2, ikiwa ni dakika nne, sekunde nane mbele ya mshindi wa Medali ya Fedha Basil Heatley wa Uingereza. Kokichi Tsuburaya alikuwa wa tatu.
  Aidha, aliweka rekodi pia ya kuwa mwanariadha wa kwanza kihistoria kushinda kwenye Marathon ya Olimpiki mara mbili.
  Baada ya kumaliza mbio hizo, alielekea upande wa mashabiki akisangilia huku akifanya mazoezi ya viungo kabla ya kusema kwamba anaweza kukimbia kilomita 10 zaidi.
  Bikila alirejea Ethiopia akipata mapokezi ya kishujaa kwa mara nyingine na Mfalme wan chi hiyo alimpandisha cheo tena na kumpa gari nyeupe aina ya Volkswagen Beetle.
  Katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 1968 kwa mara nyingine, Bikila na Mamo Wolde walijitosa kwenye Marathon. Bikila alitakiwa kuvaa jezi namba moja.
  Safari hii Bikila aliachia ngazi baada ya kukimbia kwa kilomita 17 tu, kutokana na kuumia mguu wake wa kulia, hivyo kubaki akimuangalia rafiki yake na mkimbiaji mwenzake kipenzi wa siku nyingi, Mamo Wolde akiibuka mshindi. Mamo Wolde alisema baadaye kwamba kama Bikila asingeumia, alikuwa ana uhakika angesginda mbio hizo.
  Mwaka 1969, wakati wa machafuko ya kisiasa mjini Addis, Bikila alikuwa anaendesha Volkswagen Beetle yake na wakati akijaribu kulikwepa kundi la watu waliokuwa wakiwalinda wanafunzi, alipoteza mwelekeo wa kulimudu gari lake na kutumbukia nalo kwenye mtaro.
  Mwenyewe alitupwa nje ya gari wakati ajali hiyo ilimsababishia ulemavu japokuwa alipelekwa kwenye hospitali ya Stoke Mandeville nchini Uingereza alichoambulia ni kupata nafuu na si kuepuka kabisa ulemavu.
  “Mtu wa mafanikio amekutana na janga, ilikuwa ni kwa nguvu za Mungu nilishinda Olimpiki, na ilikuwa ni kwa uwezo wa Mungu pia nikapata ajali. Nakubali ushindi huo kama navyolikubali janga hili. Sina budu kukubaliana na yote yaliyotokea kama ukweli wa maisha na kuishi kwa furaha,”alisema Bikila baada ya kupata janga hilo.
  Baadaye Niskanen alimshawishi kushiriki mashindano ya walemavu na Abebe alitania kwamba angeshinda Olimpiki ijayo akiwa kwenye kiti cha walemavu.
  Abebe alikaribishwa kama mgeni rasmi kwenye michuano ya Olimpiki ya mwaka 1972 mjini Munich, Ujerumani ambako alishuhudia swahiba wake Mamo Wolde akishindwa kuvunja rekodi yake ya kushinda mara mbili mfululizo Marathon ya michuano hiyo baada ya kushika nafasi ya tatu Mmarekani Frank Shorter.
  Baada ya Shorter kupokea Medali yake, alikwenda kumpa mkono Bikila.
  Oktoba 23, mwaka 1973, Abebe Bikila alifariki dunia mjini Addis Ababa akiwa na umri wa miaka 41 kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya kuvuja kwenye ubongo, matatizo ambayo yalitokana na ajali aliyopata miaka minne kabla ya kifo chake.
  Nyota huyo wa Afrika, aliacha mke na watoto wanne wakati mazishi yake mjini Addis Ababa yalihudhuriwa na watu wapatao 75,000 wakati Mfalme wa Ethiopia, Haile Selassie alitenga siku ya kitaifa ya kumbukumbu ya kifo cha shujaa huyo wa Ethiopia.
  Uwanja mmoja mjini Addis Ababa umepewa jina kwa heshima yake.
  Shule ya Jumuiya ya Wamarekani mjini Addis Ababa waliipa jina la shujaa huyo, klabu yao ya mazoezi mwishoni mwa miaka ya 1960.
  Agosti mwaka 2005, kwa pamoja na kituo cha A Glimmer of Hope Foundation na washirika wake, Israel na Dave Welland, waliamua kuibadilisha jina shule ya Oromo na kuwa Yaya Abebe Bikila Primary Village School, ikiwa ni heshima ya jamii ya wana Mendida kwa mwanariadha huyo.
  Shule hiyo ipo mita mia chache kutoka kijiji cha Jato, Ethiopia.
  Abebe Bikila alizaliwa Agosti 7, mwaka 1932, siku ambayo zilifanyika mbio za Marathon kwenye Olimpiki ya Los Angeles, Marekani. Alizaliwa katika kijiji cha Jato, umbali wa kilometa tisa kutoka mji wa Mendida, Ethiopia.
  Baba yake alikuwa mchungaji wa mifugo na Abebe aliamua kujiunga na jeshi la Mfalme Selassie ili aweze kuisaidia familia yake.
  Kiuto chake cha kwanza cha kazi kilikuwa Addis Ababa ambako alianza kama askari asiye na cheo na huko ndiko alipokutana na Onni Niskanen, raia wa Sweden aliyepewa kazi ya kufundisha Riadha na serikali ya Ethiopia, ambaye alikunwa na kipaji chake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ABEBE BIKILA: MWAFRIKA WA KWANZA KUTWAA MEDALI YA DHAHABU OLIMPIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top