• HABARI MPYA

  Ijumaa, Februari 27, 2009

  USIKU WA MWAFRIKA WAANZA KUNOGA TENA BILLICANAS

  ILIKUWA kama mambo yanaanza upya taratibu ndani ya ukumbi wa maraha, Club Billicanas, ulipofunguliwa upya, baada ya ukarabati wake, lakini sasa bila shaka mambo yanaanza kwenda bambam.
  Sasa Club Billicanas taratibu inaanza tena kuvutia watu kwa wingi, ikiwa katika mwonekano na mandhari nzuri zaidi baada ya ukarabati makini, ulioifanya klabu hiyo ionekane ya kisasa zaidi.
  Miongoni mwa ratiba kongwe za Club Billicanas ambazo zimekuwa zikiteka hisia za wengi ni onyesho la Usiku wa Mwafrika, ambao kwa kawaida bendi zenye kupiga muziki wa asili ya Afrika hutumbuiza kila Jumatano.
  Kabla ya Billicanas kufungwa, katika Usiku huo zimewahi kutumbuiza bendi mbalimbali na mara ya mwisho ni African Stars ‘Twanga Pepeta’, iliyokuwa ikifanya vitu vyake siku hiyo.
  Lakini kwa sasa baada ya kufunguliwa, katika Usiku wa Mwafrika ni bendi ya Akudo Impact ndiyo inayotumbuiza.
  Akudo inayotamba na albamu yake ya Impact, sambamba na nyimbo kadhaa mpya, zinazotarajiwa kuwamo kwenye albamu yao ya pili, hakika imeumudu usiku huo.
  Bendi hiyo yenye wanamuziki nyota kama waimbaji Christian Bella na kaka yake Nico, Tarcise Masela, Zagreb Butamu Kasongo, Alain Kabasele, marapa Toto Ze Bingwa na Canal Top, inawakusanya watu kutoka sehemu tofauti za Jiji la Dar es Salaam hadi Club Billicanas kila Jumatano.
  Akudo yenye mpiga gita la bass anayesifika nchini, Decanto kama ilivyo mpiga solo wao, Mabeka Bampadi ‘Pitchou Meshal’ Jumatano wiki hii ilikonga nyoyo za waliojitoma katika ukumbi huo kama ilivyo ada yake.
  Onyesho lilianza taratibu wakati watu wakiwa wameelekeza shingo zao kwenye Televisheni zilizomo ukumbini humo, wakifuatilia mchezo kati ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya wenyeji Ivory Coast mjini Abidjan, kwenye michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN).
  Ni wakati huo ambao Andrew Sekedia alipokuwa akiwaliwaza watu hao kwa kinanda chake kitamu, kabla ya skwadi zima la Akudo kuvamia jukwaani na kuanza rasmi burudani ya Usiku wa Mwafrika.
  Kama ilivyo ada, watu walikuwa wakinyanyuka na kwenda kucheza kulingana na mtu jinsi alivyopendezewa na wimbo uliokuwa ukitumbuizwa wakati huo.
  Bado tungo zake Chris Bella katika nyimbo Safari Siyo Kifo na Yako Wapi Mapenzi zinanoga zaidi kwenye bendi hiyo, kwani hivyo ndivyo vibao ambavyo viliwaamsha wengi kucheza siku hiyo.
  Lakini nyimbo pia Crazy In Love utunzi wake Mabeka Bampadi nao ulikonga nyoyo za watu waliokuwapo kwenye ukumbi wa Billicanas Jumatano hiyo, ambao pia walishuhudia na mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
  Pia wimbo Maisha uliotungwa na Issa Kabeya nao ulichengua sawa na Inauma Sana Moyoni utunzi wake Masela, Huruma uliotungwa na Zagreb na Walimwengu Si Binadamu ambao umetungwa kwa ushirikiano wa wanamuziki wote wa bendi hiyo.
  Wakati mchezo kati ya Stars na Ivory Coast ulipomalizika kwa Tanzania kushinda 1-0 kutokana na bao pekee la Mrisho Ngassa aliyeruka kama mkizi kuusukumia nyavuni mpira uliotokana na krosi ya Henry Joseph, ndipo mambo yaliponoga zaidi.
  Kwani Akudo, maarufu kama Vijana wa Masauti, ndipo walipoanza kulishambulia jukwaa mfululizo, wakati ambao pia idadi ya watu ukumbini ilizidi kuongezeka marapa Ze Bingwa na Calan Top wakichengua zaidi kwa vionjo vyao vitamu.
  Kali zaidi ni kijembe kwa wapinzani wao wa jadi, FM Academia, pale wanaposema; “Eeeeh ni vijana wa masauti, siyo wazee wa masuti”.
  Akudo wenyewe kwa kawaida hupiga pamba nyepesi. Kwa mfano Jumatano hiyo walikuwa wamevalia nguo mchanganyiko kama suruali za jeans na fulana, surualia na shati za linen, wengine suti za michezo, hakika walipendeza. Wapinzani wao FM, wenyewe jukwaani ni maarufu kwa suti zao za nguvu.
  Ikumbukwe Akudo inadhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), ambao pia ni wadhamini wa Taifa Stars.
  Januari 26, mwaka huu, SBL iliongeza mkataba wake wa kuidhamini Akudo kwa mwaka mmoja zaidi, ambao thamani yake ni shilingi Milioni 200.
  Hafla ya kusaini mkataba huo ilifanyika kwenye ofisi za SBL zilizopo Chang’ombe mjini Dar es Salaam, upande wa Serengeti ukiwakilishwa na Meneja Masoko wake, Suchen Roy, wakati kwa Akudo Impact alikuwa ni Mkurugenzi wa Fedha, Adam Bundala.
  Yote kwa yote, Usiku wa Mwafrika umeanza kunoga tena ndani ya Club Billicanas, iliyofunguliwa upya Januari 7, mwaka huu, baada ya ukarabati uliodumu takriban mwaka mmoja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: USIKU WA MWAFRIKA WAANZA KUNOGA TENA BILLICANAS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top