• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 11, 2009

  MTOTO WA INNO HAULE AFUATAYE NYAYO ZA BABA


  Inno Haule akipokea tuzo ya ufungaji bora kwenye michuano ya Asia, wakati anacheza soka ya kulipwa Urabuni, je mwanawe atafikia huko?
  MTOTO wa nyoka ni nyoka, naam, swadakta. Huo ni usemi ambao umekuwa ukidhihirika na kujirudia mara kwa mara. Kwa mara nyingine tena, mwanasoka chipukizi nchini, kiungo Haule Innocent(PICHANI KULIA) mtoto wa mshambuliaji wa zamani wa kimataifas nchini, Innocent Haule anadhihirisha usemi huo.
  Akiwa mchezo wa Ligi Kuu visiwani hapa kwa mwaka wa tatu sasa, Haule amekwishaweka matumaini ya kufunika umaarufu wa baba yake kisoka.
  Haule Jr. amepania kucheza soka ya kulipwa Ulaya na kuwa mchezaji tegemeo zaidi wa timu ya taifa ya Zanzibar na ya muungano, Taifa Stars.
  Katika mahojiano na DIMBA mwaka jana visiwani Zanzibar, Haule alisema kwamba anafahamu baba yake alifika mbali kisoka na alicheza kwa muda mrefu, jambo ambalo kwake analichukulia kama deni kubwa liinalodai na fidia.
  “Baba yangu ni kati ya wanasoka ambao hawataweza kusahaulika Tanzania, alifanya mambo makubwa, alicheza kwa muda mrefu, lakini mimi nina mipango ya kufika mbali zaidi ya yeye,”anasema Haule.
  “Kwa sababu katika umri huu wa miaka 18 sasa nipo nipo timu ya Ligi Kuu Zanzibar, pia nimekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya vijana kwa miaka minne sasa na nimecheza mashindano mbalimbali.
  Yamenijengea uzoefu wa kutosha na kujiamini pia, bado kuna changamoto nyingi nakutana nazo, naamini tu ninaweza kutimiza ndoto zangu, suala la maana ni kujibidiisha kwa mazoezi,”anasema.
  Haule kwa sasa ni miongoni wachezaji waliowezesha Polisi ya Zanzibar kufika fainali ya Kombe la Mapinduzi, dhidi ya Miembeni, mechji ambayo itafanyika leo kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa.
  Awali ya hapo, Polisi iliitoa Yanga kwa mikwaju ya penalti, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, mchezo ambao pia ulifanyika kwenye Uwanja wa Amaan.
  Anauzungumzia mchezo huo kwa kusema:
  “Unajua timu za Bara, hasa hizi sijui Simba na Yanga huwa zinazidharau sana timu za huku, yaani wao wanakuwa kama hawaji kushindana, wanakuja kushinda. Sasa wakikutana na hali ya ushindani kidogo, wanachanganyikiwa, yaani kwa kweli hizio SImba na Yanga ni timu rahisi sana kufungika, kwanza wachezaji wake wanakuwa kama wamekwisharidhika fulani hivi, wanona timu za huku kama si sawa yao,”anasema.
  Haule anasema hizo ndizo sababu ambazo ziliifanya Yanga ishinde kutwa moja visiwani hapa, tangu iwasili Januari 6 ikitokea Dar es Salaam.
  Lakini akiwazungumzia kiutaalamu, Haule anasema Yanga ni timu nzuri yenye wachezaji wazuri na anashangaa mashabiki wa klabu hiyo kukata tamaa kwa kufungwa na Polisi.
  “Kwanza kufungwa ni sehemu ya mchezo, si kila anayefungwa basi hana uwezo, Yanga watulie tu, wana timu nzuri,”anasema.
  Kuhusu mchezo wao wa leo dhidi ya Miembeni, Haule anasema utakuwa mgumu lakiji wao wana matumaini makubwa ya kushinda.
  “Miembeni wazuri, tena kwa sasa tuna upinzani nao mkali sana, kwa kweli hiyo mechi itakuwa patashika nguo kuchanika, ila sisi tumejiandaa kwa ajili ya kuchukua hili Kombe,”anasema.
  Akiizungumzia Ligi ya Zanzibar, Haule anasema kwamba pamoja na kusheni vipaji vingi, lakini imedhoofu kutokana na kukosa udhamini.
  “Hapa kuna vipaji sana, wachezaji wengi wazuri nadhani tangu umefika hapa umewaona, lakini tatizo ndiyo hilo, hakuna wadhamini, kwa hiuyo wacheaji wanakosa changamoto ya kutosha,”anasema.
  Akizungumzia sababu za Polisi kukosa tiketi ya kucheza michuano ya Shirikisho nla Soka Afrika (CAF), baada ya kuambulia nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, Haule anasema;
  “Hauwezi kuwa kwenye nafsasi ile ile miaka yote, hata England, Hispania, Italia, Ufaransa, timu zinapishana, ili si vizuri kutoka nje ya timu tano tano bora, sisi tulikuwa wa nne, waliobahatika ni mwaka wao huu,”anasema.
  Haule anasema wanaamini 2008, Polisi itarajea kwenye chati na leo watatuma salamu kwa kuanza kutwaa Kombe la Mapinduzi, wakimenyana na mabingwa wa Zanzibar, Miembeni.
  Haule Innocent Haule, alizaliwa Juni 2 mwaka 1991 Magomeni mjini Dar es Salaam.
  Elimu yake ya Msingi alipata katika shule ya Mtoni Mtongani, kabla ya kujiunga na sekondari ya Makongo alikosoma hadi Kidato cha Nne.
  Timu yake ya awali kuchezea kiungo huyo ni Scar Face iliyokuw ana maskani yake Mtoni, ikiwa inacheza Ligi Daraja la Daraja la Tatu wilayani Temeke.
  Baadaye alihamia Scud ya Temeke aliyoichezea hadi mwaka 2004 alipotua visiwani hapa, kujiunga na Tembo, ambayo sasa inajulikana kama Ras Rehema.
  Haule anasema kwamba, mwaka 2005 alichukuliwa na Polisi ya hapa baada ya kung’ara kwenye michuano ya Challenge ya vijana chini ya umri wa miapa 19 na kuiwezesha Zanzibar iliyokuwa mwenyeji kutwaa Kombe hilo.
  Zanzibar ilitwaa Kombe hilo baada ya kuifunga Uganda kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.
  Anasema anaikumbuka sana fainali hiyo, kwani alipewa dhamana ya kuipa au kuinyima ubingwa kwenye mikwaju ya penalti na akafanikiwa kufanya ambacho mashabiki wengi walikuwa wakiomba.
  “Tulikuwa tuko nyuma kwa penalti moja, sasa mimi nikawa nakwenda kupiga ya tano, ambayo nikifunga tunaendelea kupigiana, lakini nikikosa, Uganda wanashangilia ubingwa.
  Uwanja mzima ulikuwa kimya kabisa wananisikilizia mimi nitafanya nini, basi nilikwenda bila wasiwasi, kwa sababu mimi penalti tangu nikiwa mdogo, ni mtaalamu, basi nilipiga penalti nzuri ile mbaya, Uwanja mzima ukaripuka kwa shangwe.
  Penalti zilizofuata za mwisho, ndiyo Waganda wakakosa, sisi tukapata tukanyakua ubingwa, ilikuwa furaha kubwa sana kwetu kuweza kubakisha Kombe lile nyumbani,”nakumbuka Haule.
  Haule ambaye mwaka huu, ameajiriwa na jeshi la Polisi baada ya kutimiza umri wa miaka 18, anasema kwamba ataendelea kuichezea timu hiyo hadi apate timu ya kuchezea soka ya kulipwa nje.
  “Mimi siwezi kuhama timu hii, kwa sababu kwanza imekwishanipatia ajira, sioni sababu ya kuhama hama, hapa naomba mungu nipate nafasi ya kwenda nchi zenye maslahi zaidi kisoka, siyo kutoka hapa kwenda timu nyingine ya hapa hapa,”anasema.
  Ilikuwaje Haule akaijiingiza kwenye soka?
  “Mimi kwanza huu mchezo ulikuwa kwenye damu, tangu niko mdogo nilikuwa napenda sana soka, lakini pia baba naye alichangia kwa kiasi kikubwa mimi kupenda soka, kwa sababu alikuwa ananichukua tunaenda wote uwanjani wakati anacheza,” anasema.
  Haule anasema katika wanasoka wa Tanzania, anavutiwa na kipa namba wa klabu ya Simba, Juma Kaseja wakati kwa Waafrika wanaocheza Ulaya, anakunwa mno na mpachika m,abao wa Cameroon na Barcelona ya Hispania, Samuel Eto’o.
  Baba yake Haule, Inno Haule alikuwa mpachika mabao tegemeo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Starsw tangu mwaka 1983 hadi 1991 alipotimkia Oman.
  Inno Haule aliibukia kwenye klabu ya Miembeni mwaka 1977 kabla ya kujiunga na Simba ya Dar es Salaam mwaka 1981 aliyoichezea hadi 1986 aliporejea Miembeni, ambako alikaa msimu mmoja tu na kuhamia Small Simba.
  Mwaka 1991 alihamia Oman Club ya Oman, aliyoichezea hadi mwaka 1996 aliporejea Small SImba ambako alicheza hadi 1999 kabla ya kwenda kumalizia soka yake katika timu ya Kizimkazi, aliyoichezea hadi mwaka 2002.
  Mama yake Haule aitwaye Maida Mohammed ni mfanyabishara mjini Dar es Salaam na anaishi Temeke.
  Huyo ndiye Haule Innocent Haule, mtoto wa mpachika mabao hodari wa zamani nchini, Inno Haule, je ataweza kufuata nyayo za baba yake? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MTOTO WA INNO HAULE AFUATAYE NYAYO ZA BABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top