• HABARI MPYA

  Jumamosi, Januari 31, 2009

  YANGA YAFANYA KUFURU TAIFA

  Boniphace Ambani katikati akishangilia moja ya mabao yake manne aliyofunga

  ILIKUWA shangwe tupu kwa mashabiki wa Yanga Jumamosi Januari 31, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada timu yao kuichabanga Etoile d’Or Mirontsy ya Comoro kwa mabao 8-1 katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Shukrani kwao, washambuliaji Boniphace Ambani, aliyefunga mabao manne, Jerry Tegete aliyetikisa nyavu mara mbili, Mrisho Ngassa na Wisdom Ndholvu ambao walifunga bao moja kila mmoja katika mchezo ‘ulioutapisha’ Uwanja wa Taifa.
  Yanga iliuanza mchezo huo kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya tatu, kupitia mkongwe wa Kenya, Ambani. Ambani pia anaongoza kwa kupachika mabao katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, akiunganisha kwa kichwa krosi ya beki wa kulia, Shadrack Nsajigwa.
  Kabla ya kupiga krosi hiyo, Nsajigwa alipokea pasi ya Kiggi Makassy.
  Hata hivyo, mchezo ulionekana kama utakuwa mgumu, wakati Wacomoro hao walipokuja juu na kusawazisha bao hilo dakika ya 21, mfungaji akiwa ni Aboubakar Ali, aliyetumia vyema makosa ya beki wa kushoto, Amir Maftah.
  Baada ya bao hilo, Yanga walisota kutaka kufunga bao la pili, lakini hawakufanikiwa hadi kipyenga cha kumaliza ngwe ya kwanza kilipopulizwa.
  Licha ya kuipangua vizuri ngome ya Etoile hadi kipa wake katika dakika ya 41, lakini kiungo wa pembeni wa Yanga, Mrisho Ngassa, alijikuta akifanya kazi bure baada ya kumpasia Ben Mwalala, ambaye alikuwa tayari amekwishaotea, hivyo pamoja na kutikisa nyavu, mwamuzi alilikataa bao hilo.
  Dakika moja kabla ya mapumziko, kiungo wa Yanga, Geoffrey Boniface, alitoka baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Nurdin Bakari. Hadi mapumziko, timu hizo mbili zilikuwa sare ya bao 1-1.
  Jerry Tegete aliyeingia dakika ya 46 badala ya Ben Mwalala, aliiongezea uhai safu ya ushambuliaji ya Yanga, ambayo kipindi cha kwanza ikiundwa na Ambani, Ngasa na Mwalala haikuwa tishio kwa Etoile.
  Tegete aliifungia Yanga bao la pili katika dakika ya 54 kwa shuti kali. Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa Abdi Kassim ‘Babi’ aliyeubetua kwa Nurdin ambaye alipiga kichwa kilichotua mguuni mwa mfungaji.
  Dakika ya 67, Ngasa alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Rattaoni Moadji.
  Dakika ya 70, Ambani, ambaye jana aliibuka kuwa nyota wa mchezo, alifunga bao la tatu kwa mkwaju wa penalti baada ya Ngasa kuchezewa rafu eneo la hatari.
  Wisdon Ndlovu, beki wa kimataifa wa Malawi, aliifungia Yanga bao la nne, akiunganisha kwa mgongo kona safi iliyochongwa na Babi.
  Tegete naye alifunga bao la tano dakika ya 76 akiunganisha krosi safi ya Vincent Barnabas, wakati Ambani aliwainua tena vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 79, akipokea pasi ya Ngassa, ambaye angeweza kufunga mwenyewe kama angetaka.
  Ngasa baada ya kuwatengenezea wenzake mabao mengi, hatimaye katika dakika ya 81, aliambaa na mpira na kwenda kufunga bao la saba kwa mabingwa hao wa Tanzania, baada ya kuchomekewa pasi safi na Nsajigwa.
  Dakika tano kabla ya mpira kumalizika, Ambani alifunga bao lake la nne katika mchezo huo, na la nane kwa Yanga jana akiunganisha kona safi iliyochongwa na Abdi Kassim ‘Babbi’.
  Baada ya bao hilo, furaha ya kocha wa Yanga, Profesa Dusan Kondic, ilionekana kupitiliza na kuamua kupunguza wachezaji wake uwanjani, akimtoa Maftah bila kuingiza mtu mwingine.
  Hata hivyo, Etoile si wachovu moja kwa moja, kwani mshambuliaji wao, Mikidadi Daoud alionekana kuisumbua sumbua kidogo ngome ya Yanga.
  Kwa ushindi huo, Yanga imejiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele, Raundi ya Kwanza, ambako itakutana na mabingwa mara sita barani Afrika, Al Ahly (National) ya Misri.
  Yanga: Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Amir Maftah, Wisdom Ndhlovu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Geoffrey Boniface/Nurdin Bakari, Mrisho Ngasa, Abdi Kassim, Boniphace Ambani, Ben Mwalala/Jerry Tegete na Kigi Makassy/ Vincent Barnabas.
  Etoile: Moddasse Mohmed, Mahadali Bazar, Mikdad Daoud, Rattaoni Moadji, Kasiwine Bazar, Nadhufouldine Zoguene, Djalmadine Alloui, Rakibou Oussein, Aboubakar Ali, Bourhane Nidhoine, Assani Issaif
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA YAFANYA KUFURU TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top