• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 09, 2009

  KIEMBA: Kiungo aliyekimbia kucheza bure Yanga

  na ojuku abraham
  NI rahisi kumtambua akiwa uwanjani. Siyo tu kwa sababu ya staili yake ya usokotaji nywele katika mtindo wa rasta, bali kutokana na uwezo wake wa kusakata kandanda, hasa katika kuumiliki.
  Anajua mpira, angalau kwa kiwango cha wachezaji wa hapa nyumbani. Namna ya upokeaji wake wa mpira, jinsi anavyotoa pasi na hata anavyokokota, inaonyesha wazi kwamba ni mmoja kati ya wanasoka wenye vipaji vya hali ya juu katika Tanzania kwa sasa.
  Anaitwa Amri Kiemba Ramadhani aliyezaliwa mjini Kigoma, Juni 17, 1983 ni mtoto wa baba Athumani Amri Athumani na mama Mariam Fadhil.
  Huyu ndiye mchezaji ambaye aliyemkuna mno kocha wa klabu ya Asante Kotoko ya Ghana, Bashir Hayford ambaye pia aliwahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana ya Ghana, chini ya umri wa miaka 17, aliyekuja na klabu hiyo nchini mwaka 2006 kwa ajili ya mechi za kirafiki.
  Hayford ambaye ana shule yake ya watoto nchini Ghana, baada ya kukunwa na soka ya kijana huyo, akiichezea Yanga dhidi ya Kotoko Uwanja wa taifga, Dar es Salaam na CCM Kirumba mjini Mwanza, aliuomba uongozi wa klabu hiyo umuuzie kijana huyo. Hata hivyo, Yanga yenye maskani yake makutano ya twiga na Jangwani, walikataa.
  “Huyu kijana nikimchukua mimi, baada ya miezi sita tu, namuuza bei mbaya sana Ulaya,”alisema Hayford.
  Lakini leo ni mwaka wa tatu tangu kocha huyo atamke maneno hayo na Kiemba hayupo tena Yanga, anaichezea klabu ya Moro United ya Ligi Kuu pia, kulikoni?
  “Mimi nilisikia habari hizo, kwamba Kotoko walikuwa wananitaka, lakini viongozi wa Yanga hawakuwahi kuniambia, basi ndio ikawa hivyo hivyo,”anasema Kiemba katika mahojiano na DIMBA Alhamisi.
  Historia ya Kiemba, inaanzia mbali, lakini hasa kipaji chake kilikuja kugunduliwa na Mkuu wa shule ya sekondari ya Makongo, Kanali mstaafu, Iddi Kipingu ambaye alimchukua mara tu baada ya kumaliza elimu yake ya msingi pale Burka, iliyopo mjini Arusha na kumsogeza kwenye shule yake, jijini Dar es Salaam.
  Huo ulikuwa ni mwaka 2000. Katika taratibu ambazo Kipingu, anayechukuliwa kama mdau mkubwa wa soka nchini alijiwekea, ni kuwatoza nusu ya ada wanafunzi wote ambao walikwenda hapo kwa ajili ya kuendeleza vipaji vyao, Kiemba akiwa miongoni mwao.
  Lakini nusu hiyo ya ada, bado haikuwa nafuu kwa mchezaji huyo, kwani hali ngumu ya maisha ilimlazimu kuacha shule. “Kipingu alikuwa amepanga kutuendeleza sana kielimu pamoja na kimichezo, lakini hali yangu haikuwa nzuri, nikajikuta naondoka na kuendelea na mpira,” anasema.
  Hivyo mwaka 2003, akajikuta akijiunga na timu ya Karume, 44KJ ya mjini Mbeya ambayo hata hivyo, hakukaa nayo sana kwani msimu uliofuata, akaelekea Arusha, kujiunga na timu ambayo sasa haipo tena, Pallsons.
  Lakini, kutotimizwa kwa makubaliano kati yake na uongozi wa timu hiyo, iliyokuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara wa madini, ukamlazimisha kuondoka na kujiunga na Kagera Sugar, ambayo wakati huo ilikuwa ikipigania kupanda ligi kuu kutoka daraja la kwanza.
  “Nilipokuwa Pallsons, tulikuwa na mtu mmoja anaitwa Alphonce Modest, yeye akachukuliwa na Kagera kwa ajili ya kuwa kocha. Sasa baada ya mimi kuondoka, akaniita, nikaenda Kagera ambako tulicheza hadi kupanda Ligi Kuu. Nilicheza pale kwa misimu miwili, 2004/2005,” anasema.
  2006, Kiemba alijiunga na Yanga na kuanza kuichezea katika ligi ndogo kipindi ambacho Shirikisho la soka Tanzania (TFF), lilikuwa linabadili kalenda yake ya msimu, ili kwenda sambamba na ya kimataifa.
  Katika Ligi ndogo, Kiemba aliiwezesha Yanga kufika fainali na kufungwa na Simba kwa mikwaju ya penalti, baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, hivyo kuambulia tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho, badala ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  “Kwa sababu ya Yanga kupata nafasi hiyo na CAF (Shirikisho la soka Afrika) kutaka majina ya wachezaji yatumwe mapema, uongozi wa Yanga ulinitaka nisaini kwanza fomu ziende CAF halafu baadaye ndiyo tuzungumze kuhusu mkataba, nikakataa.
  Akaja mtu mmoja anaitwa Amani Ibrahim Makungu, huyu alikuwa ni mfadhili wa Miembeni, akanishawishi nijiunge na timu yake, nikasaini mkataba wa miezi nane na kuichezea hadi kuipa ubingwa wa Visiwani mwaka jana.”
  Katika wachezaji ambao walikisaidia kikosi hicho kutwaa ubingwa huo wa visiwani mwaka jana, ni pamoja na beki wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Samson Mwamanda, Thomas Maurice, Farouk Ramadhan, Mbarouk Suleiman na Mohamed Golo.
  Kuelekea msimu huu wa ligi, mmoja wa Wakurugenzi wa Moro United, aliyemtaja kwa jina moja la Seif, alimfuata na kumshawishi kujiunga na timu hiyo, ambayo hivi sasa ina maskani yake mjini Dar es Salaam.
  “Kwa sasa nipo hapa, sijui mwakani nitakuwa wapi kwa sababu hatujui kitakachotokea. Tunacheza vizuri, suala la kushuka daraja halipo kabisa katika akili zetu, tutapambana hadi mwisho ili tuendelee kubakia.
  Lakini hata hivyo, pamoja na uwezo wake mkubwa wa kusakata kandanda, bado hayumo katika kikosi cha timu ya taifa, kilicho chini ya kocha Marcio Maximo: “Kuchezea timu ya taifa ni ndoto ya kila mmoja, lakini huwezi kujisikia vibaya kwa kutokuwepo, kwa sababu tupo wachezaji wengi wazuri. Mimi nafikiri kinachofanya nisiwepo ni kutokana na mfumo wa ufundishaji wa mwalimu, huenda anaona mimi siwezi kukaa vizuri pale kwenye mipango yake.
  “Sina kinyongo naye na wala sina hofu, najua ipo siku kama bahati yangu na mimi nitaitwa kuchezea. Siwezi kusema mimi ni zaidi ya viungo wengine waliopo pale, ila kama nilivyosema mwanzo, kinachotutofautisha wachezaji ni mifumo inayotumiwa na walimu.
  Kuhusu mtazamo wake katika soka la sasa, Kiemba anakerwa na viongozi wanaoendeleza utamaduni wa kupunja maslahi ya wachezaji, kwani umepitwa na wakati.
  “Viongozi wengi wa mpira siku hizi utakuta ni wale waliokuwa wachezaji siku za nyuma, baada ya kuwa walishindwa kutengeneza maisha yao wakati ule, sasa wanatumia nafasi wanazopata hivi sasa kujaribu kujinufaisha. Matokeo yake wanashindwa kubuni mipango ya maendeleo kwa timu na wachezaji wao.
  “Pia, Watanzania hivi sasa wamebadilika, akili zao zinaona mbali sana. Zamani soka ilionekana ni mchezo wa watu waliokosa kazi za kufanya, lakini leo hii ni ajira, tena kubwa tu. Hili ni jambo kubwa na la msingi.
  “Binafsi ninashukuru Mungu kwamba ingawa sijacheza soka kwa kiwango kikubwa sana, lakini nimefanikiwa kuwa na sehemu yangu ya kuishi, na ninawasomesha pia baadhi ya ndugu zangu. Kwangu mimi ni kitu kizuri”.
  Kiemba, ambaye hushirikiana na ‘rasta’ mwenzake, Nizar Khalfan katika safu ya kiungo ya Moro United, anamhusudu mno Mrisho Ngassa wa Yanga, kwa aina ya uchezaji wake.
  “Ngassa ni mchezaji ambaye anaweza kuisaidia timu wakati wowote kwa juhudi zake binafsi. Ana vitu vingi vinavyoweza kuibeba timu. Ni mtu ambaye ananifurahisha na kama upo naye timu moja, unatambua kwamba wakati wowote atafanya mambo kuwa sawa,”.
  Kiemba aliwahi kukutana na mchezaji huyo mwenye kasi katika kikosi cha Yanga. Alipoondoka Kagera Sugar kutua Jangwani, winga huyo naye ndiyo kwanza alijiunga na Kagera akitokea nyumbani kwao, Mwanza.
  Kiemba, amemuoa Maimuna ambaye ni mama wa nyumbani na hadi sasa wamebahatika kuwa na mtoto mmoja wa kiume, Shaaban, mwenye umri wa miezi nane.
  Ni wa pili kuzaliwa katika familia yao ya watoto watano. Wengine ni kaka yao mkubwa, Athumani, dada yao, Safia, Mohamed na Muhando, kitinda mimba mwenye umri wa miaka 12 sasa. Huyo ndiye Amri Kiemba Ramadhani, kiungo aliyekataa kucheza Yanga kwa mali kauli.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIEMBA: Kiungo aliyekimbia kucheza bure Yanga Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top