• HABARI MPYA

    Thursday, February 05, 2009

    Mjue Asha, ‘Mama Yanga’ aliyepigwa faini na CECAFA

    na somoe ng'itu
    Kama ambavyo wataalamu wa mpira wa miguu wanavyosema kuwa mchezaji wa 12 uwanjani ni mashabiki wanaofika kuangalia mechi zinapokuwa zinafanyika kwenye viwanja kuanzia ngazi ya klabu hadi ya timu ya taifa.
    Hapa nchini kuna mashabiki mbalimbali, mmoja wao ni Asha Abdallah Zuru maarufu kwa jina la `Asha- Yanga`.
    Shabiki huyo amepachikwa jina hilo kutokana na mapenzi yake na klabu yake ya Yanga ya hapa jijini Dar es Salaam.
    Tofauti na mashabiki wengine, Asha- Yanga amekuwa ni shabiki namba moja wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars kutokana na kuwa karibu na timu hiyo inapokuwa inajiandaa na mechi zake za mashindano mbalimbali kuanzia mazoezini hadi wakati wa mechi.
    Asha ameliambia Nipashe kuwa yeye soka ndio kitu anachokipenda hapa duniani na humpa starehe kubwa pale anapoona timu ya taifa inafanya vizuri katika mashindano inayoshiriki.
    Alisema kuwa anawashangaa watu wanaosema kuwa wanapenda mpira wakati hujitokeza uwanjani pale tu timu zao zinapokuwa zinacheza na pale zinapokuwa zinafanya vibaya wamekuwa hawaonekani.
    Alisema kwamba yeye anafika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam kuangalia mechi zote za ligi zinazochezwa hapo hata kama ni za timu za daraja la kwanza au mechi za kirafiki za kujaribu wachezaji.
    ``Mpira ndio ugonjwa wangu mkubwa, siwezi kukaa nyumbani wakati nina uwezo wa kwenda uwanjani kuangalia mechi, na kama mechi hiyo inachezwa nje ya Dar es Salaam halafu sijaenda ujue nimekwana kweli kweli,`` alisema Asha.
    Alisema kuwa amekuwa akiifuatilia Stars kuanzia mwaka 1989 kwa kutokosa mechi zake zote zinazofanyika hapa jijini na mikoani huku akiongeza kuwa alikuwa akipata machungu ya kushindwa kusafiri na timu hiyo kwenye michezo iliyokuwa inafanyika nje ya nchi.
    ``Hata katika mkoba wangu ukiangalia huwezi kukosa ratiba za mechi za ligi kuu au Stars ambayo huwa nawaomba TFF- Shirikisho la soka Tanzania wanitolee nakala, wamenizoea na hakuna anayeninyima,`` aliongeza.
    Alisema kuwa mechi ya kwanza kusafiri nje ya nchi na Stars ni iliyofanyika Mei mwaka jana nchini Uganda ambapo walifanikiwa kutoka sare ya 1-1 na kuiondoa timu ya taifa ya nchi hiyo, The Cranes kwa jumla ya mabao 3-1.
    Aliitaja safari nyingine aliyosafiri na Stars ni kwenda Dakar, Senegal ambapo timu yake ilifungwa mabao 4-0 na baadaye alikwenda Younde, Cameroon na kupoteza tena mchezo ikiwa ni mechi za kutafuta nafasi ya kushiriki fainali zilizopita za Kombe la Mataifa ya Afrika huko Ghana.
    Shabiki huyo hakuwa nyuma na hakusita kuambatana na Stars licha ya kuwa imepoteza matumaini na kwenda katika fainali hizo kwa kusafiri mpaka Cape Verde.
    ``Mechi za Mwanza, Arusha na Morogoro hizo ndio huwa sizikosi kama vile za uwanja wa Taifa mdogo wangu, nawaomba na wengine wabadilike na kuwa na moyo wa kusafiri na timu inayopeperusha bendera halisi ya taifa letu,`` aliongeza.

    MECHI YA STARS ILIYOMUUMIZA
    Asha aliliambia gazeti hili kuwa mechi ambayo machungu yake ni vigumu yeye kuyasahau ni dhidi ya timu ya taifa ya Msumbiji iliyofanyika mwaka juzi kwenye uwanja Mpya ambapo, Stars ilifungwa bao la dakika za mapema na hadi mechi hiyo inamalizika hakuna bao lingine lililopatikana.
    Alisema kuwa hiyo ndiyo mechi ambayo ilikuwa na msisimko mkubwa lakini matokeo yaliyopatikana yaliwahuzunisha mashabiki wengi.
    Alisema pia alikubaliana na matokeo hayo kwa sababu asiyekubali kushindwa si mshindani na hilo ndio lililotokea kwa upande wa timu yake.
    ``Iliniuma sana siku ile, mpaka leo sipendi kukumbuka kilichotokea, nafikiri si mimi peke yangu, kila vijana wakijaribu kutaka kusawazisha hali ilikataa,`` alisema.
    Hata hivyo aliongeza kuwa Stars inapofungwa hata kama ni mechi ya kirafiki husijikia vibaya sana lakini analazimika kukubaliana na matokeo.
    Alisema kuwa huwa mpole pale anapoona kuwa timu yake imefungwa kimchezo na si hila za soka kuwa zimetumika.

    MECHI YA STARS ILIYOMPA FURAHA
    Baada ya kufanikiwa kuitoa Uganda, kila mtu alikuwa anasema kuwa safari ya Stars kwenda Ivory Coast katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CHAN) zinazoshirikisha wachezaji wa ndani itaishia Sudan.
    Asha alisema kuwa kauli hizo na akifuatilia rekodi ya Stars na Sudan alikuwa hana raha licha ya Stars kufanikiwa kupata ushindi wa 3-1 katika mechi ya kwanza iliyofanyika hapa nyumbani.
    ``Mchezo ulipomalizika kule Sudan na tukiwa tumeshinda 2-1 nilisikia furaha kuliko siku zote ambazo nimekuwa karibu na Stars, nilikuwa siamini kama tutafanikiwa kushinda kwa sababu tulichokifanya sisi hapa nyumbani na wenzetu wangeweza kukifanya kwao,`` aliongeza.
    Alisema kuwa mechi hiyo iliwapa hofu lakini anawapongeza wachezaji, viongozi na wote walioshiriki kwa namna yoyote kuhakikisha ushindi unapatikana.

    SAKATA LAKE NA CECAFA
    Hivi karibuni, Asha alikuwa jijini Kampala na timu hiyo ambayo katika mashindano ya Chalenji yanayoandaliwa na Shirikisho la soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) hujulikana kama Kilimanjaro Stars kwa lengo la kuishangilia na kuwapa moyo wachezaji wa timu hiyo.
    Katika mashindano hayo, shabiki huyo alinusurika kufungiwa kutazama mechi za michuano hiyo kutokana na kutoa lugha chafu kwa Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Nicholas Musonye na kutakiwa kulipa faini ya Dola za Marekani 200.
    Viongozi waliokuwa Uganda, baada ya shabiki huyo kulalamikiwa na ushahidi wa picha ya video kuonyeshwa walimuombea msamaha na walimlipia faini hiyo.
    ``Ni kweli nilitukana, hasira zilinishika kutokana na timu yetu kuonewa katika mchezo ule (Kilimanjaro Stars vs Kenya, Harambee Stars), na walionekana wanataka kutimiza mipango ya kuiondoa Tanzania katika mashindano,`` alisema.
    Aliongeza kuwa anawashukuru viongozi wa TFF kwa kumpa ushirikiano na kuwataka kuwa pamoja na mashabiki wao wakati wote.
    ``Walionyesha kuwa wananithamini, sitaacha kuishangilia Stars ila nililazimika kumtukana Musonye kwa sababu ya uchungu niliokuwa nao,`` aliongeza.
    Malalamiko hayo yalitokana na CECAFA kumpanga mwamuzi mwenye uraia wa Somalia lakini anayeishi Kenya katika mchezo wa nusu fainali iliyowakutanisha Kilimanjaro Stars na Harambee Stars.

    MAANDALIZI YA IVORY COAST
    Alisema kuwa maandalizi ya kwenda Ivory Coast ameshayaanza na anaamini kwamba atafanikiwa kwenda kuishangilia timu yake.
    ``Kama kawaida yangu, nimeshaanza kuwaomba wadau wangu ili niweze kusafiri na timu, naamini watanipa ushirikiano, ila nawashukuru sana TFF kwa sababu wao wanachangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha safari zangu,`` alisema.
    Alisema pia ni wakati umefika Watanzania wakawa kama mashabiki wa nchi nyingine ambao hujitokeza kwa wingi kusafiri na timu zao katika mechi za nje ya nchi.
    Asha pia amekuwa akisafiri na klabu yake ya Yanga katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu ya Tanzania Bara inapokwenda mikoani na mwaka 2007 alifanikiwa kwenda nayo Sudan ilipokuwa inashiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya timu ya El Mereikh.
    Shabiki huyo amezaliwa hapa jijini Dar es Salaam na amejaaliwa kupata watoto watatu ambapo mwanae wa mwisho wa kiume anayeitwa Salum ndiye anaonekana kufuata mapenzi aliyonayo mama yake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: Mjue Asha, ‘Mama Yanga’ aliyepigwa faini na CECAFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top