• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 16, 2009

  SASA RASMI, YANGA KUIVAA NATIONAL AL AHLY

  WINGA machachari wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa (pichani juu) jana alipachika mabao manne, kwenye Uwanja wa Said Mohamed Cheikh mjini Mitsamihuly, kilomita 40 kutoka mji mkuu wa Comoro, Moroni wakati klabu yake, Yanga inaibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Etoile d'Or Mirontsy ya Comorro katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Kwa matokeo hayo sasa, Yanga imesonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 14-1 baada ya awali kuichapa 8-1 Etoile katika mchezo wa kwanza uliochezwa wiki mbili zilizopita Uwanja Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam.
  Yanga sasa itavaana na mabingwa mara sita Afrika, Al-Ahly (National) ya Misri katika raundi ya kwanza itakayochezwa mwezi ujao.
  Hata hivyo, Etoile ililazimika kutumia Uwanja huo wenye nyasi bandia kutokana na kutokea katika kisiwa cha Anjoun, ambako hakuna Uwanja wenye hadhi ya kimataifa. Ngassa alikuwa `mwiba` wa kweli kwa Wacomoro hao na mara nyingi alikuwa akiwachachafya kwa chenga za maudhi na kasi yake uwanjani hata akafunga mabao yake yote kipindi cha kwanza kabla ya kutolewa na Kocha Dusan Kondic wakati kipindi cha pili kilipoanza.
  Ngassa alizamisha bao lake la kwanza katika dakika ya tatu akiuganisha kona iliyochongwa na Amir Maftah, wakati la pili alifunga dakika ya 33 baada ya kuunganisha krosi ya Fred Mbuna. Bao bora la mechi hiyo lilikuwa la tatu katika dakika ya 39, wakati Ngassa alipowachambua viungo na mabeki wa Etoile kuanzia katikati ya Uwanja kabla ya kumfikia kipa wao na kumtesa pia.
  Hilo ni bao ambalo wapenzi wa Yanga walilifananisha na lile la nyota wa zamani wa Argentina, Diego Maradona alilowafunga England katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986 nchini Mexico. Maradona aliwapiga chenga mabeki wanne wa England kabla ya kuujaza mpira kimiani wakati Argentina inashinda 2-1.
  Ngassa alifunga mahesabu yake katika dakika ya 41 wakati alipounganisha krosi ya mshambuliaji Mkenya, Boniphace Ambani, kabla ya Vincent Barnabas kufunga la tano katika dakika ya 77 na Ambani kuhitimisha karamu hiyo ya mabao, kwa bao la sita dakika ya 88 baada ya kuwahi mpira uliotemwa na kipa.
  Yanga inakuwa timu pekee ya Tanzania kusonga mbele, baada ya wawakilishi wengine kutolewa. Prisons, imetupwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya bao 6-0, baada ya juzi kukubali kichapo cha bao 4-0 kutoka kwa wapinzani wao Khalij Sert ya Libya. Katika mchezo huo uliochezwa Tripol, Prisons ilitakiwa kushinda bao 3-0,ili iweze kusonga mbele kutokana na kukubali kichapo cha bao 2-0, katika mchezo wa awali uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru zamani uwanja wa taifa, jijini Dar es Salaam. Prisons, ilionekana thaifu mbele ya Khalij Sert kutokana na kucheza hovyo katikadakika zote za mchezo, ambapo iliwachukua muda mfupi walibya hao kupachika bao la kuongoza. Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka Libya zimeeleza kuwa wawakilishi hao wa Tanzania walishindwa kufurukuta mbele ya khalij, ambapo hawakufanya hata shambulizi la maana langoni mwa wapinzani wao. Kwa matokeo hayo Prisons itakuwa imeungana na wawakilishi wengine wa Zanzibar kutolewa kwenye michuano ya kimataifa,ambazo ni timu ya Miembeni na Mundu, ambapo Miembeni imetolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Monomotapa ya Zimbabwe kwa jumla ya bao 3-2. Mundu imetolewa na Red Arrows ya Zambia kwa jumla ya bao 7-0, baada ya kukubali kichapo cha bao 6-0,kwenye mchezo wa awali na katika mchezo wa marudiano uluiochezwa jijini Dar es salaam timu hiyo ilifungwa bao 1-0. Hiyo ni mara ya tatu kwa Prisons kushindwa kufanya vizuri kwenye michuaano ya kimataifa kutokana na kutolewa katika hatua za awali katika miaka yote iliyowahi kushiriki. Timu hiyo inatarajia kurejea jijini Dar es Salaam keshokutwa na mara baada ya kutua jijini itakaa kwa muda mfupi kabla ya kurejea Mbeya kuendelea na maadalizi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SASA RASMI, YANGA KUIVAA NATIONAL AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top