• HABARI MPYA

  Jumanne, Februari 03, 2009

  Maximo: Hakuna mwenye namba Stars

  KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, Marcio Maximo, amesema wachezaji wote 27 waliochaguliwa katika kikosi chake wana nafasi ya kusafiri kuelekea Ivory Coast kwenye michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN.
  “Nilisema pale awali kwamba baadhi ya wachezaji nitawaita ili kuwapa uzoefu kwa ajili ya kuichezea timu hii siku zijazo. Kauli hii isiwavunje moyo wale ambao hawakuwa na timu iliposhiriki Chalenji kule Uganda. Kila mmoja ana nafasi, kutegemea na jinsi atakavyojituma mazoezini pamoja na nidhamu ya uchezaji.
  “Hawa wote ni Watanzania, wana nafasi sawa katika timu yao. Hakuna mwenye timu. Kama Kazimoto atafanya vizuri mazoezini, hakuna sababu kwa nini asiende Ivory Coast eti kwa sababu tu yeye ni mara yake ya kwanza kuitwa kwenye timu.
  “Wachezaji wote walioitwa ni wazuri na hii haimaanishi pia kwamba wale ambao hawakuitwa ni wabaya. Kama ninavyosema siku zote, Taifa Stars siyo mali ya mtu, kila mchezaji Mtanzania ana nafasi sawa, kitu kinachoangaliwa ni kiwango cha mchezaji katika wakati husika, nidhamu na ushirikiano.”
  Juzi Jumatatu, Maximo alitaja kikosi cha wachezaji 27 watakaoingia kambini leo jioni, kikiwa na sura mpya mbili, Mwinyi Kazimoto wa JKT Ruvu pamoja na Zahoro Pazi wa Mtibwa Sugar. Aidha, wachezaji wanne waliowahi kuichezea timu hiyo siku za nyuma na kuachwa, wamerejeshwa, ambao ni Salvatory Ntebe na Erasto Nyoni wa Azam FC, Uhuru Selemani wa Mtibwa na Jabir Aziz wa Simba.
  Ni mchezaji mmoja tu, Meshack Abel wa Simba, ndiye aliyeachwa kwenye kikosi kilichoshiriki Chalenji na kushika nafasi ya tatu nchini Uganda mwishoni mwa mwaka jana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: Maximo: Hakuna mwenye namba Stars Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top