• HABARI MPYA

  Ijumaa, Februari 20, 2009

  MAKINDA YA TOTO HOI KWA VILLA

  na mohamed mharizo
  TIMU ya soka ya Villa Squad ya jijini Dar es Salaam jana imeifunga timu ya Toto Africa ya Mwanza mabao 2-1 katika mchezo wa ligi ya vijana uliofanyika katika uwanja wa Karume.
  Villa walikuwa wa kwanza kuliona lango la Toto ambapo katika dakika ya 19 ya kipindi cha kwanza,Abdallah Mohamed alifunga bao baada ya kona iliyochongwa na Kassim Mohamed.
  Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu,lakini Villa walilisakama lango la Toto na katika dakika ya 50 ya kipindi cha pili,Hemed Hamad aliipatia Villa bao la pili kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Toto Juma Biliyomo.
  Mara baada ya bao hilo,Toto walikuja juu na katika dakika ya 82 ya kipindi cha pili,walipata bao lililofungwa na William Mahalu baada ya mlinda mlango wa Villa kutema shuti lililopigwa na Vedastus Mabori.
  Akizungumza baada ya pambano hilo,kocha wa timu ya Villa Squad,Richard Mbuya alisema ushindi huo unatokana na mazoezi ya pamoja ya wachezaji wake na kujituma uwanjani na kuongeza kuwa matarajio yao ni kucheza fainali na kuibuka na ubingwa wa michuano hiyo.
  Wakati huo huo,timu ya Polisi Dodoma,imejinyakulia pointi za bure baada ya timu ya Kagera Sugar kushindwa kutokea uwanjani,hii ni mara ya pili kwa timu hiyo kutoonekana uwanajani ambapo pia ilifanya hivyo katika pambano lake la awali dhidi ya Toto Africa.


  YANGA, SIMBA HOI BIN TAABAN LIGI YA VIJANA
  na mohamed mharizo
  WAKATI Yanga Jumatano ilifungwa 2-1 na Azam katika michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kutoka vikosi vya Ligi Kuu, Simba nayo Jumanne iliendeleza uteja katika ligi hiyo, baada ya kufungwa mabao 4-0 na JKT Ruvu katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
  JKT Ruvu walijipatia bao lao la kwanza katika dakika ya 5 lililofungwa na Omari Matata kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Simba Moses Pascal. Dakika ya 42, vijana hao wa maafande walijipatia bao la pili lililowekwa kimiani na mshambuliaji wake Abdul Mwarami kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Inga Abdallah.
  Kipindi cha pili Simba walionesha uhai lakini katika dakika ya 47, JKT Ruvu walipata bao la tatu lililofungwa tena na mshambuliaji Abdul Mwarami baada ya pasi nzuri ya Nuru Mandemba.
  Na mnamo dakika ya 78, JKT Ruvu walihitimisha kalamu ya mabao ambapo mshambuliaji Omari Matata aliipatia bao baada ya kupangua ngome ya Simba na kuachia shuti lililomshinda kipa wa Simba Moses Pascal.
  Wachezaji Omari Mtata na Abdul Mwarami walikuwa nyota wa mchezo huo kwa kuonesha umahiri wa pasi za uhakika na kushangiliwa na mashabiki waliohudhuria mchezo huo.
  Katika mchezo wa kwanza, Simba walifungwa mabao 3-0 na vijana wenzao wa Moro United.
  Akizungumza mara baada ya mchezo huo kocha wa JKT Ruvu Lawrence Uyalo alisema amefurahishwa na mchezo mzuri uliooneshwa na timu yake na kusema wamerekebisha makosa baada ya kufungwa 4-1 na timu ya Mtibwa Sugar katika pambalo lao la kwanza.

  ...Yanga hoi, Prisons yashinda

  MSHAMBULIAJI wa timu ya soka ya Azam FC, Herry Habib jana aliiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa ligi ya vijana chini ya miaka 20 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja w Karume
  Bao la kwanza la Azam lilipatikana katika dakika ya 30 na Habib baada ya kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa timu ya Yanga Hamisi Yusuph, mara baada ya bao hilo,vijana wa Yanga walikuja juu na katika dakika ya 38 walijipatia bao la kusawazisha lililofungwa na mshambuliaji Edo Christopher baada ya kuunganisha pasi safi kutoka kwa Razack Juma.
  Vijana wa Azam walikuja juu, katika dakika ya 72 Herry Habib tena aliipatia timu yake bao la pili na ushindi baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mau Ally.
  Mwamuzi wa pambano hilo Andrew Shamba alimuonyesha kadi nyekundu mchezaji wa Yanga Focus Mloka kwa kumchezea rafu mbaya Mau Ally wa Azam.
  Akizungumza mara baada ya pambano hilo, Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega alilalamikia mwamuzi Andrew Shamba kwa kuonyesha upendeleo kwa timu ya Azam na kuongeza kuwa timu yake ilicheza vizuri, ilistahili ushindi.
  Naye Meneja wa Azam FC, Herry Mzozo alisema kuwa mafanikio ya ushindi huo ni usajili wa wachezaji nyota waliosajiliwa kutoka katika timu ya France Rangers na timu ya Copa Coca Cola.
  Wakati huo huo timu ya Prisons iliifunga Moro United mabao 3-2 katika mchezo wa ligi hiyo uliofanyika jana kwenye Uwanja huo huo, Prisons walijipatia bao la kwanza katika dakika ya 20 lililofungwa na mshambuliaji Francis Castro na katika dakika ya 33 Moro United walijipatia bao la kusawazisha lililofungwa na Msafiri Juma.
  Mshambuliaji Francis Castro aliipatia timu yake ya Prisons bao la pili katika dakika ya 23, bao hilo liliwazindua wachezaji wa timu ya Moro United na katika dakika ya 50, Salum Telela aliipatia timu hiyo bao la kusawazisha kwa njia ya penati baada ya Msafiri Juma kuchezewa faulo katika eneo la hatari.
  Prisons walijipatia bao la ushindi katika dakika ya 83 lililofungwa na Hamisi Ally baada ya kuitoka ngome ya Moro United na kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa Moro.
  Akizungumza baada ya mechi hiyo, kocha wa Moro United Abed Mziba alisema kuwa pamoja na kufungwa wanajipanga vizuri ili waweze kufanya vizuri katika mchezo ujao.


  Stars yakabidhiwa vifaa na wadhamini

  WADHAMINI wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Kampuni ya bia ya Serengeti na benki ya NMB Jumatano waliikabidhi vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 35 vitakavyotumika kwa ajili fainali za wachezaji wanaocheza ligi za ndani CHAN zinazotarajiwa kuanza Jumapili nchini Avory Coast
  Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa jana kwa nahodha msaidizi wa timu hiyo, Shedrack Nsajigwa katika hafla fupi iliyofanyika kwenye hoteli ya New Afrika na kuhudhuliwa na katibu Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania TFF, Fedrick Mwakalebela, wawakilishi wa Serengeti na benki ya NMB
  Vifaa vilivyokabidhiwa jana ni pamoja na suti kwa wachezaji wote wa Stars zenye rangi ya bluu, jezi seti tano, viatu, soksi, vilinda ugoko vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 35.
  Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja uhusiano wa Serengeti, Teddy Mapunda alisema kuwa vifaa hivyo vimetolewa kwa ushirikiano wa NMB na Serengeti ili vitumike katika fainali hizo ambazo ni mara yake ya kwanza kufanyika na Tanzania kupata nafasi.
  Katibu Mkuu wa TFF, Fedrick Mwakalebela alisema kuwa katika mashindano hayo, Stars itakuwa ikivaa jezi mpya katika kila mchezo watakaocheza
  Naye nahodha wa timu hiyo, Nsajigwa alisema kuwa vifaa vilivyotolewa na wadhamini hao vinawapa faraja ya kufanya vizuri kwenye mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kujituma zaidi
  “Vifaa hivi vinazidi kutupa morari na kujituma zaidi nina imani kwamba tutafanya vizuri kwenye mashindano hayo kinachotakiwa ni dua za watanzania “ alisema na kusisitiza kuwawashukuru wadhamini hao kwa kuwapa suti ambazo zitawafanys kuonekana nadhifu watakapokuwa wanaondoka nchini hii leo
  Naye Katibu Mkuu wa TFF,Fedrick Mwakalebela aliwashukuru wadhamini kwa kutoka vifaa hivyo ambapo ni jitihaza zao kuona kwamba timu hiyo inafanya vizuri kwenye mashindano hayo.
  Alisema kuwa maandalizi yote kwa ajili ya safari hiyo yamekamilika, msafara wa watu 60 unatarajiwa kuondoka nchini hii leo saa 11 alfajiri, kati ya hao wachezaji 22, viongozi sita , waaadishi wa habari na wadau wa soka hapa nchini.  Kondic huyoo Afrika Kusini

  KOCHA Mkuu wa mabingwa wa soka nchini, Mserbia Dusan Kondic aliondoka nchini jana kuelekea Afrika Kusini, ilipo familia yake kwa ajili ya kubadilisha hati yake ya kusafiria.
  Akizungumza siku moja tu baada ya kikosi chake kurejea nchini kikitokea Comoro, ambako kiliibuka na ushindi wa 6-0 katika mchezo wa marudiano Raundi ya Awali michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo kuibuka na ushindi wa jumla 14-1, kocha huyo alisema pasipoti yake imejaa.
  “Hivi sasa siwezi kusafiri, hati yangu ya kusafiria imejaa, hainiruhusu kwenda sehemu yoyote tena,” alisema kocha huyo.
  Alisema atakuwa nchini Afrika Kusini kwa muda wa siku saba kabla ya kurejea kuendelea na kazi. Wachezaji wengine wa kikosi chake wanaobaki nyumbani baada ya wenzao kuelekea Ivory Coast na Taifa Stars, wamepewa mapumziko mafupi.
  Kondic anaondoka huku kikosi chake kikiwa na kibarua kizito dhidi ya mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo mikubwa kabisa ngazi ya vilabu, Al Ahly ya Misri, baada ya kufuzu kwa raundi ya kwanza.
  Katika mchezo wake wa marudiano dhidi ya mabingwa hao wa Comoro, Yanga, ikiwa na kikosi chake kamili, kilitoa kipigo cha mabao 6-0.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAKINDA YA TOTO HOI KWA VILLA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top