• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 23, 2009

  WATATU STARS ULAYA NJE NJE

  Nizar Khalfan wa Tanzania akimtoka mchezaji wa Senegal


  ***
  na abdul mohammed, abidjan, Ivory Coast
  WACHEZAJI watatu wa timu ya Taifa, Taifa Stars huenda wakapata nafasi ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya mara baada ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN). Akizungumza jana mjini Abidjan, Ivory Coast wakala wa FIFA kutoka Senegal, Said Chang alisema timu za Ulaya zimemtuma kuangalia viwango vya wachezaji watatu wa Stars. “Kuna wachezaji watatu ambao nimepewa jukumu la kuangalia viwango vyao wakati wa michuano hii na baada ya hapo tutaangalia uwezekano wa kuwafanyia majaribio katika moja ya timu 12 za Ulaya,” alisema Chang. Hata hivyo, pamoja na kubanwa ili ataje majina ya wachezaji hao na timu wanazotarajia kwenda kufanya majaribio, Shang hakuwa tayari kufanya hivyo. Alisema kwamba asingependa kuona wachezaji wakiguswa na suala hilo na badala yake angependa kuona wachezaji hao wakicheza mpira wao kama kawaida na yeye akiendelea ‘kuwamulika’ katika mechi zote. “Ninachoweza kusema ni kwamba upo uwezekano mkubwa kwa wachezaji wa Tanzania kuvutia mawakala wa klabu za Ulaya, mimi ninaowamulika ni watatu tu,” alisema Chang. Pamoja na Chang kutokuwa tayari kuzitaja timu hizo, zipo habari kwamba wachezaji hao watapelekwa katika klabu maarufu za ama Uingereza au Ufaransa. Katika siku za hivi karibuni winga wa Yanga, Mrisho Ngasa amekuwa akihusishwa na mipango ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa Ulaya.

  Kongo ya Kinshasa yaifagilia Stars  KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Santos Mutubile amesema kwamba lengo kuu la timu yake ni kufikia hatua ya fainali na kubeba Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN).Akizungumza jana mjini hapa, Santos pia alisema timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imepiga hatua kubwa katika soka lake jambo ambalo alisema ni la kujivunia.Alisema DRC iliwahi kucheza mechi ya kirafiki na Stars na Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 na baada ya hapo timu hiyo imeendelea kuwa na mabadiliko ya kujivunia.Katika hatua nyingine, Santos pia alisema timu pekee ambayo DRC inaihofia ni Libya ingawa alisisitiza kwamba wachezaji wake watapigana kufa na kupona.Mbali na Libya, Santos pia alisema anazifahamu fika timu za Ivory Coast na Ghana kuwa ni timu kubwa lakini kwa kuwa shabaha yao ni kufika hatua ya fainali na kubeba kombe, watahakikisha wanapigana kufa na kupona.“Tunatambua ubora na ukubwa wa timu za Ghana na Ivory Coast lakini utakumbuka kuwa hadi kufuzu fainali hizi tumeitoa Cameroon ambayo pia ni timu kubwa, hivyo hata mbele ya Ghana na Ivory Coast tunaweza kushinda,” alisema.Alisema kwamba wanazitumia fainali za CHAN kufuta machozi ya mashabiki wa DRC ambao wana huzuni baada ya timu yao kukosa tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia na Mataifa ya Afrika 2010.DRC katika CHAN imepangwa Kundi B pamoja na timu za Ghana, Libya na Zimbabwe, leo timu hiyo itatupa kete yake ya kwanza dhidi ya Libya.


  Khatib: Ivory Coast tusaidieni soka la Tanzania  WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatib ameiombaSerikali ya Ivory Coast kusaidia maendeleo ya soka Tanzania. Khatib aliyasema hayo juzi katika mazungumzo yake na Waziri wa Ivory Coast anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amadou Kone ambaye pia ni msemaji wa serikali. Khatib alimtaka balozi wa Tanzania katika nchi za ECOWAS, Msuya Mangachi kulifanyia kazi suala hilo ili kuhakikisha Tanzania inafaidika. “Kiwango chenu cha soka kiko juu sana na Tanzania tuna mengi ya kujifunza ili kuhakikisha tunakuwa juu kupitia ushirikiano huu,” alisema Khatib. Alisema: “Soka inapendwa sana Tanzania na sisi tunataka tuwe na mafanikio kama nyinyi, mna wachezaji wengi nje ya nchi.” Kwa upande wake Kone alitaka suala hilo lishughulikiwe mapema na kushauri iundwe tume ya pamoja ya wataalam wa Ivory Coast na Tanzania ili kufanikisha suala hilo. Kone alidokeza kuwa nchi yake ina wachezaji zaidi ya 1,000 wanaocheza soka la kulipwa Ulaya na sababu ni kuwapo shule nyingi za soka nchini mwao. “Siri kubwa ni kuwapo kwa shule na vituo vya michezo, vya watu binafsi na hata vya serikali,” alisema. Khatib alimtaka Mangachi kutumia nafasi yake kuhakikisha soka inakuwa kwa kutumia mbinu zinazotumiwa na nchi za Afrika Magharibi.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WATATU STARS ULAYA NJE NJE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top