• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 25, 2009

  SIKIA KILIO CHA JELLAH MTAGWA...

  UNAPOZUNGUMZIA wachezaji mahiri nchini ambao ni kati ya waliyoiweka Tanzania katika medani za juu kisoka, basi miongoni mwao huwezi kuacha kulitaja jina la Jella Mtagwa.
  Rudisha akili yako nyuma hadi miaka ya ‘80 pale kwa mara ya kwanza Tanzania iliposhiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika katika mji wa Lagos nchini Nigeria, Jella ndiye aliyekuwa nahodha wa kudumu wa kikosi hicho akisaidiwa na Leodger Tenga.
  Wote mtakumbuka jinsi Tanzania wakati huo ilivyokuwa imesheni vipaji lukuki mmoja wao ni Augustino Peter (Peter Tino) ambaye bao lake halitasahaulika ndilo lililofanya tuipate nafasi hii na wengine wengi.
  Hata hivyo Stars haikufika mbali kwani ilitolewa baada ya kuchapwa na Nigeria 3-1, Misri 2-1 na Ivory Coast 1-1 tangu tuliposhiriki fainali hizo hatukupata tena nafasi hiyo mpaka mwaka huu tunaposhiriki fainali kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) zinazofanyika nchini Ivory Coast.
  Si hivyo tu huyu ndiye mchezaji pekee ambaye sura yake ilipata kuwekwa katika stampu za posta hiyo ilikuwa mwanzoni mwa mwaka 1982.Kutokana na umaarufu huo na sasa akiwa kama amesahaulika katika soka la bongo, Mtanzania liliamua kumtafuta na kuzungumza naye ambapo alikuwa na haya ya kusimulia.
  “Ndio nipo hapa hapa mjini na pengine sisikiki tena katika medani ya soka labda walioshika mpini katika hawaoni kama kuna umuhimu wa kunishirikisha lakini nipo ingawa kwa sasa kama unavyoniona nina maradhi haya ya Stroke (Paralaizi) yaliyonichukua kwa takribani mwaka wa pili na nusu sasa.
  “Hivi unavyoniona angalau nina unafuu ndio maana nyakati zingine nafika maeneo haya klabu yangu ya zamani Pan Afrika kama moja ya mazoezi ambayo nimeshauriwa na daktari kutembea tembea kwasababu ni mdau wa soka naona nije huku kubadilishana mawazo na wenzangu” alianza Jella kusimulia.
  Kama tunafuatilia mambo mbalimbali hapa nchini, moja ya mambo hayo ni hali hiyo ya Jella Mtagwa kwani ilikuwa ni moja ya mjadala uliowahi kujadiliwa Bungeni ili asaidiwe kutokana na mchango wake kwa Taifa kama nilivyoanisha baadhi ya mchango wake mwanzoni mwa makala haya, mwenyewe anauzungumziaje mjadala huo?
  “Sikiliza mwandishi, sipendi hilo tulizungumzie sana kwasababu ni moja ya mambo yanayonikera ugonjwa wangu kufanywa ishu na kuzua mijadala isiyokuwa na msingi pengine walioanzisha walikuwa na lengo la kujipatia umaarufu.
  “Lakini ukweli kwamba tangu uliposikia hadithi ya afya yangu kujadiliwa Bungeni binafsi sijamuona hata Mbunge mmoja angalau kunipa hata Shilingi mia naweza kuwaita wanafiki” alisema Jella.
  Alisema suala la afya yake ni la kibinafsi zaidi na kuwaonya wachache wanaotaka kutafuta umaarufu kupitia yeye waache kama wanatambua ana mchango katika Taifa hili basi suala hilo lisingekuwa mjadala angeweza kusaidiwa ipasavyo kama yeye alivyofanya wakati huo akicheza soka.
  Alipoulizwa endapo atakutana na Rais Kikwete yeye anaweza kumueleza nini hasa kuhusiana na afya yake ambayo imekuwa mjadala Jella alisema Rais anawajua watu wenye mchango katika nchi hii akiamini anafahamu na mchango wake pia hivyo atamtaka amkumbuke sasa angali mzima asisubiri afe na kumzika ama kuchangia haitamsaidia kauli hiyo pia inawahusu wanaojadili afya yake.
  Kama nilivyoainisha mwanzoni kwamba huyu ndiye mchezaji pekee mpaka sasa Tanzania ambaye sura yake iliwahi kuchapwa katika stampu hiyo ilikuwa mwaka 1992.Akizungumzia hilo na jinsi alivyonufaika huyu hapa Jella anasema.
  “Kwa kweli sura yangu ilichapishwa bila idhini yangu wala sikuhusishwa kwahiyo kama wapo walionufaka mimi sijui kwani hadi leo sikupewa hata shilingi moja, mimi niliona tu katika stampu hizo na nilipouliza kwa chama cha soka wakati huo (TFF) kilichokuwa kikiongozwa na Mwenyekiti Said El Maamry na Katibu Mkuu Patrick Songoro (Sasa marehemu) waliniambia Posta waliwaomba.
  “Walinieleza kuwa Shirika la Posta nchini liliomba kwa chama hicho kuwapa mchezaji watakayeona anafaa kuwekwa katika stampu zao kama moja ya vivutio na kuitangaza Tanzania katika soka ndipo kama viongozi walinichagua mimi na kikubwa walichozingatia nilikuwa mchezaji bora mwishoni mwa ligi mwaka 1981 hivyo ndivyo ilivyokuwa” alisema Jella.
  Anapoizungumzia historia yake katika soka Jella anasema alianza kucheza kandanda mwaka 1970 akivutiwa baada ya Mkoa wake Morogoro kutwaa ubingwa wa Taifa (Taifa Cup).Kabla ya kujitumbukiza kucheza soka la ushindani alikuwa ni mchezaji aliyeonyesha kipaji chake tangu alipokuwa anasoma shule ya Msingi Mwembesongo iliyopo huko huko Morogoro.
  “Kama una kipaji na kitu fulani basi hakuna atakayeweza kukiondoa hivyo hata mimi nafikiri kwangu mpira ni kipaji kutoka kwa Mwenyeji Mungu kwani sikutegemea kama ningekuwa mmoja wa wasukuma gozi mahiri nchini.
  “Nilianza kwa kuwaokotea mpira Nyota Afrika ambao uwanja wao ulikuwa jirani na nyumbani kama wakipiga mashuti yanaangukia nyumbani kwetu hivyo nikaanza kuupenda na wakati mwingine nilipokuwa nikienda kuwatazama kama hawakutimia kitimu walinipa nafasi ya kucheza hapo ndipo kipaji kilianzia huo ulikuwa mwaka 1972 ” alisema Jella.
  Anasema kutokana na umahiri alioanza kuonyesha katika soka alichaguliwa kuwa mmoja wa wachezaji wa kombaini ya mkoa wa Morogoro mwaka 1973 akiwa mmoja wa wachezaji waliousaidia mkoa wake kuibuka mabingwa mwaka huo walipoichapa Tanga 2-1 mchezo uliochezwa Nyamagana Mwanza ndipo Yanga wakamuona na kumsajili lakini wakati huo alikuwa bado anasoma Morogoro Sekondari.
  Wakati huo Yanga iliyokuwa ikiongozwa na Tabu Mangala chini ya timu meneja Shirazi Sharifu iliwalazimu kumfuata Jella Morogoro Sekondari kila ilipomhitaji na kumrudisha kwani alibakiza mwaka mmoja wa masomo.Alimaliza elimu yake ya Sekondari mwaka 1975 ndipo alipokuja jijini Dar es Salaam na kuendelea na timu yake hiyo mpya.
  Alipokuja Dar es Salaam na kuungana na Yanga alikutana na wachezaji kadhaa kama vile Maulid Dilunga, Elias Michael, Abdalah Juma, Muhidin Fadhili, Athuman Kilambo, Omary Kapera, Leonard Chetete na wengine.
  Moja ya mechi anazokumbuka mara tu alipotua Yanga baada ya kumaliza shule mwaka huohuo ni siku walipotwaa ubingwa wa Afrika Mashariki baada ya kuwachapa watani zao wa jadi Simba mabao 2-0 katika fainali zilizofanyika Zanzibar.
  Awali waliziondosha Express ya Uganda kwa mabao 5-1, Mufulila Wonderes 4-1 kisha watani zao hao.Siku hiyo katika mechi yao na watani zao kikosi chao kilikuwa Patrick Nyaga, Ally Yusuf, Juma Shaaban, Leodger Tenga, Omary Kapera, Jella Mtagwa, Bona Maxi, Sunday Manara, Mwinda Ramadhani, Sembuli Gibson na Muhaji Mukhi.
  Aliitwa kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars mwaka 1973 baada ya mkoa wake wa Morogoro kuwa mabingwa wa Taifa Cup na moja kwa moja walikwenda kushiriki michuano ya kombe la Challenge iliyofanyika Kampala.Anasema walifika hadi fainali na kutolewa na Uganda kwa kichapo cha mabao 2-1 ingawa yeye na wenzake walioitwa katika kikosi hicho hawakucheza kwani walikuwa wadogo.
  Katika kikosi hicho kilichokuwa kikinolewa na kocha Paul West Gwivaa, wasiocheza kutokana na kuelezwa ni wadogo mbali ya yeye alikuwapo Idd Juma, Godfrey Nguruko, Mohamed Mussa na wengine hawakumbuki anasema walikuwa kama wachezaji sita hivi.
  Anachokumbuka wao ambao hawakucheza wote walichukuliwa kushiriki michuano ya kombe la Chalenji kwa vijana na kuungana na akina Sunday Manara, Mohamed Tall, Miraji Salum, Lucas Mkondora, Salum Mwinyimkuu, Shiwa Liambiko na wengine kwa pamoja wakafanikiwa kuchukua kombe baada ya kuwafunga Uganda 3-0.Kikosi hicho kilikuwa kikinolewa na kocha Marijani Shaaban.
  Waliporejea ndio waliokuwa kikosi cha timu ya Taifa na wakati huu ndipo alipoachiwa unahodha na Omari Zimbwe baada ya kuindosha Uganda the Cranes katika michuano ya kombe la Chalenji sasa kwa wakubwa walipoichapa jumla ya mabao 6-5 ikiwa ni mikwaju ya penati michuano iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
  Jella aliamua kuuacha unahodha baada ya kuutumikia kwa miaka 10 tangu 1973-1983 alipomuachia Charles Mkwasa na yeye akiamua kutundika daluga mwaka mmoja baadaye (1984) wakati huo alikuwa tayari amejiunga na Pan Afrika na tangu hapo hakucheza soka kwani aliumia goti lake la kushoto lililomlazimu kufanyiwa upasuaji (operation) na bingwa wa mifupa Dk Philemon Sarungi.
  Mwenyewe anasema aliumia goti hilo katika moja ya misukusuko ya mechi alipo ‘slaide’ kumzuia mshambuliaji wa Zambia Michael Chabala na wakati mshambuliaji huyo alipojaribu kumruka kwa bahati mbaya goti (La Chabala) lilimgonga na ndio mwanzo wa kusumbuliwa na tatizo hilo wakati mwingine hadi sasa zaidi anapokimbia.
  Jella hakukaa sana Yanga pengine si kwa makusudio yake ila ni ule mgogoro wa uongozi uliowahi kuitikisa klabu hiyo mwaka 1976 mpaka timu yao kusambaratika yeye akiamua kurejea Nyota Afrika iliyokuwa na maskani huko Morogoro.
  Mwaka huo huo aliamua kujinga na Pan Afrika baada ya kupigiwa simu na uongozi kuwa imeanzishwa timu mbadala ya Nyota Afrika sasa maskani yao yakihamia Dar es Salaam wakati anapata simu hiyo alikuwa ziarani nchini China na kikosi cha timu ya Taifa hivyo waliporejea moja kwa moja walijiunga na timu hiyo mpya aliyodumu mpaka alipotundika daluga mwaka 1984.
  Kama alivyoanisha baadhi ya matukio anayokumbuka wakati akicheza Yanga na timu ya Taifa, pia akiwa na Pan Afrika anaihusudu sana timu hiyo ilivyokuwa tishio ikisheheni wasukuma gozi mahiri waliokuwa wakizipa tumbo joto timu za Simba na Yanga.
  Kikubwa ni walipotwaa ubingwa wa ligi ya bara mwaka 1981 lakini mara zote walikuwa wakikamata nafasi ya pili tangu ilipoanzishwa timu hiyo akisema hali hiyo ilichangiwa na ligi kuchezwa katika vituo hivyo ilikuwa ikifanyiwa fitina mpaka mwaka huo ilipobadilishwa na kuanza kuchezwa kwa mtindo na ugenini.
  Akitoa maoni yake kuhusu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na timu ya Taifa (Taifa Stars) alisema kwa sasa linajitahidi sana hasa kwa kuweka uwazi na kuwashirikisha wadau mara kwamara huku akipongeza hatua ya timu ya Taifa kutokuwa kichwa cha mwendawazimu.
  “Stars inajitahidi sana kwani karibu kikosi chote hakuna mchezaji hata mmoja aliyetoka katika misingi thabiti ya soka tofauti na wengine, hapa naamanisha wangapi waliopo katika kikosi chetu ambao wamepita katika shule ‘Academies’ za soka? Alihoji.
  Lakini alitaka TFF kutumia wachezaji wakongwe katika ushauri wa masuala mbalimbali hasa kuzungumza na wachezaji waliowahi kupitia katika michuano kama hii ya CHAN ambapo wapo waliokuwapo katika fainali za mataifa ya Afrika mwaka 1980 inaweza kusaidia kwani watawaeleza jambo wanalolijua kwa makini tofauti na wengine.
  Mchezaji aliyekuwa akimsumbua sana wakati anacheza ni Sunday Manara ‘Compyuta’ huku akitanabaisha kuvutiwa kiuchezaji na Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ lakini kwa sasa hakuna.Wachezaji wa nje anaovutiwa nao Samuel Etoo na Ronaldinho Gaucho.Ni mshabiki wa Yanga, Pan na Manchester.
  Jella Mtagwa ni miongoni mwa wanasoka mahiri waliojipatia umaarufu ndani na nje ya Tanzania ambaye anaheshimika mno alizaliwa mwaka 1953 Morogoro mjini akapata elimu ya msingi shule ya Mwembesongo na baadaye kujiunga na Sekondari ya Morogoro (Moro Sec) na kumaliza mwaka 1975.Kwasasa anaishi Friends Corner jijini Dar es Salaam pamoja na mkewe waliojaliwa kupata watoto wanne kati yao wa kiume mmoja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIKIA KILIO CHA JELLAH MTAGWA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top