• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 09, 2009

  MJUE MAXIMO, KOCHA ALIYEREJESHA HADHI YA STARS

  HADI sasa ana sura mbili machoni mwa Watanzania, hii inamaanisha mashabiki wa soka nchini wanamwangalia kwa sura mbili hasa baada ya matukio ya timu ya taifa.
  Wakati anakuja kufundisha soka nchini alikuta uwanja wenye udongo mwekundu pale katika uwanja wa Karume ambapo sasa kuna ‘carpet’ la nyasi bandia.
  Mashabiki walimchukulia kama malaika aliyeleta neema katiak nchi yenye njaa, hawa hawakuwa na sala za kuwawezesha kupata pepo hiyo iliyoletwa naye
  Huyu si mwingine bali ni Marcio Maximo, Kocha wa timu ya soka ya Taifa, ‘Taifa Stars’ ambaye mwezi huu ilikuwa amalize mkataba wake wa miaka miwili kuifundisha timu hii.
  Katika kujua undani wake, DIMBA lilimtafuta Maximo na kufanya mahojiano naye, ifuatayo ni sehemu mazungumzo yake na mwandishi wa makala haya.
  Anaanza kwa kueleza historia yake ya mpira wa miguu: Alicheza soak katika klabu ya Botafogo ya Brazil katika miaka ya 1978 akiwa katika timu ya vijana.
  Lakini safari yake ya soka ilikwama mwaka 1980 baada ya kupata ajali ya gari iliyomweka nje ya uwanja kwa kipindi hicho.
  “Nilikuwa naelekea kutimiza miaka 18 ndipo siku moja nikapata ajali ya gari iliyositisha ndoto zangu za kuwa mwanasoka mahili duniani.
  “Lakini pamoja na hayo klabu yangu ya Botafogo ilinipa mkataba wa miaka miwili kuichezea wakiwa na lengo la kuniuza kwa Sport Prague ya Ureno, lakini pamoja na yote hayo sikupata nafauu ya kuniwezesha kurudi uwanjani.
  Niliumia sehemu ya kiuno kuelekea mgongoni jambo lilizima ndoto zangu za kujiunga na klabu hiyo ya Brazil japokuwa uwezo wa kucheza soka nilikuwa nao, majeraha yalinikimbiza uwanjani,” anasema Maximo.
  “Katika hili kila siku nawaambia vijana wasikate tama katika soka kwani ipo siku watakuja kuona matunda yake,” anasema Maximo.

  KITU KIPI KILIMVUTA KUWA KOCHA?
  “Kama nilivyokueleza hapo awali ajali niliyoipata ilinifanya niwahi kuwa kocha japokuwa awali nilikuwa na ndoto za kufanya kazi hiyo lakini si mapema kama ilivyokuwa.
  “Nikajiunga na Chuo kimoja Brazil (Edwards) na kuchukua masomo elimu ya viungo (Physical education) kwa muda wa miaka minne baadae nikatunukiwa shahada yangu,” anasema Maximo.
  Lakini pamoja na hali hiyo, kitendo cha kupata ajali alikikubali na hakutaka kuachana kabisa na mchezo wa mpira wa miguu jambo lililomlazimu kuwa kocha.
  “Sikutaka kujitenga na mpira wa miguu, kitu pekee ambacho kingenifanya kuwa karibu na mchezo huo ni kuwa mwalimu wake, nashukuru mpaka sasa upo karibu nami,” anasema Maximo.
  Alianza rasmi kazi ya ukocha mwaka 1982 lakini safari hiio akiwa kama mwalimu wa viungo katika timu kama ilivyokuwa kwa Amorin Itamor sasa katika timu ya Taifa.
  “Mwanzoni iliniwia vigumu hasa kutokana na umri wangu kuwa mdogo huku nikifundisha watu walionizidi umri,” anasema Maximo.
  “Kabla ya kukubali offer ya kuja kuifundisha Stars nilikuwa tayari nimeitwa na El Salvador, Umoja wa Falme za Kiarabu na klabu nyingine za Ulaya, lakini kwangu ilikuwa fahari kuja kuifundisha Tanzania kutokana na kiwango chake, nilitaka kupata changamoto ya kuinua soka na si kukuta kitu kizuri alafu kurekebisha kidogo.
  “Nimekuja kuweka misingi ya soka, nilikataa fedha nyingi kutoka El Salvador na Umoja wa Falme za Kiarabu lakini nilikubali kuja Tanzania lengo likiwa ni kubadili mpira wa hapa,” anasema Maximo.

  MATATIZO ALIYOKUTANA NAYO WAKATI ANAKUJA TANZANIA:
  “Naweza kusema nilikuwa na bahati sababu Rais Kikwete (Jakaya) na Tenga (Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania – TFF, Leodegar) walikuwa tayari wamedhamiria kuleta mapinduzi katika soka Tanzania.
  “Lakini kwa upande mwingine naweza kusema nilikutana na matatizo ya viwanja, kwa mfano uwanja wa Karume wenye udongo mwekundu usio na nyasi ni moja kati ya vitu ambavyo sitovisahau hapa nchini,” anasema Maximo.
  “Nashukuru ndani ya kipindi cha miezi mitatu mambo yakaanza kubadilika, baada ya timu ya taifa kupata udhamini pamoja na msaada wa FIFA (Shirikisho la Soka Kimataifa) na kuweza kujengwa Uwanja wa Karume.
  Nilikuta matatizo ya nidhamu kwa wachezaji huku kukiwa na uwazi mkubwa kwa wachezaji wenye miaka 19 mpaka 21 hawa hawakuwa na sehemu ya kwenda ndani ya miaka hiyo hivyo taifa lilikuwa likipoteza vipaji vingi,” anasema Maximo.
  “Wachezaji wa timu ya taifa walikuwa hawajiamini katika mchezo wowote ule kila mechi walijiwekea watafungwa tu, ilinilazimu kuwaweka sawa vijana ili wacheze mpira,” anasema Maximo.
  “Kikubwa cha kwanza ni kuhamasisha soka la vijana kwa timu zinazoshiriki ligi yoyote pia kuwapa nafasi wachezaji chipukizi katika kikosi changu.
  Pia niliwajenga kisaikolojia wachezaji kwa kuwaeleza kwamba wanaweza kucheza mechi na timu yoyote na kuifunga, nilihamasisha nidhamu kwa kila mchezaji jambo linaloisaidia timu leo hii,” anasema Maximo.
  “Kiasi Fulani kilikuwa safi kwangu kwani wachezaji walikuwa tayari wameshanielewa kuwa soka ni kitu gani nawakumbuka wakina Victor Costa, Mecky Mexime, Renatus Njohole, Said Maulid, Gaudence Mwaikimba na wengineo kuwa walikuwa ni moja ya mifano yangu kwa wakati huo,” anasema Maximo.
  “Kwanza kabisa tayari ninayo orodha ya wachezaji wasiopungua 100 ambao wapo tayari kuichezea Stars, kinachofanyika ni kufuatilia viwango vyao katika timu ili kujua kama vimeshuka au kupanda.
  Naangalia uwajibikaji wao ama mimi mwenyewe au kupitia kwa makocha wazawa waliojaa kila mkoa wa Tanzania, namaanisha kuwa mpaka sasa kila mkoa wa Tanzania kuna kocha anayetafuta wachezaji wa Stars,” anasema Maximo.
  “Kutoka TFF hakuna tatizo, kazi ilikuwapo kwa klabu hizi zilikuwa hazielewi umuhimu wa soka la vijana na utekelezaji wake, wangeelewa mapema umuhimu wake na kuandalia muthsari wake si ajabu sasa wangekuwa wanajivunia matunda yake pia kupata udhamini kutoka kwa wafadhili mbalimbali,” anasema Maximo.
  Lakini anaweka wazi kuwa angalau sasa ameeleweka kuhusu hilo na klabu kupitia kanuni mpya ya TFF zina timu za vijana ambazo baadae zitawawezesha kupata wachezaji wa kikosi cha kwanza.
  “Naishukuru FIFA kwa kutoa kozi ya uongozi kwa klabu za ligi kuu ambayo nina hakika imewabadilisha kwa kiasi Fulani,” anasema Maximo.

  USHIRIKIANO NA MAKOCHA ‘WAZAWA’:
  “Kama nilivyokueleza awali niano wengi ninaoshirikiana nao, kwanza kabisa yupo msaidizi wangu Bushiri (Ali) huyu ni mzawa nashirikiana naye kwa hali ya juu.
  KIla mkoa nina makocha wanaofanya kazi ya kuorodhesha wachezaji wenye vipaji vya soka,” anasema Maximo.
  “Angalau sasa tunaweza kuwapata kwa urahisi awali ilikuwa ngumu kufanya hivyo, hakukuwa na mashindano yoyote yale yaliyotuwezesha kupata chipukizi mwanzoni.
  Hawana (chipukizi) vituo vya kucheza soka pia hakuna fedha za kutosha kuwaweka kambini nashukuru sasa kuna mpango wa kuendeleza timu za taifa za vijana ambao utaruhusu kuwaeka kambini kila baada ya miezi miwili,” anasema Maximo.
  “Kocha huwa aridhiki na kiwango cha timu yake hata siku moja, atakayejibu anaridhishwa huyo atakuwa anatania ….ndiyo maana kila siku timu zinafanya mazoezi bado kazi ipo.
  “Japo kwa kiasi fulani tumepiga hatua ambayo tunaweza kuzungumza mambo ya baadae tofauti na hapo awali.
  Sifurahishwi na matokea ya mchezo dhidi ya Cameroon tuliocheza hivi karibuni bali naridhishwa na kiwango ilichoonesha Stars,” anasema Maximo.
  “Hakuna uchawi wowote ninaotumia hapa kwanza kuhakikisha maozezi ya nguvu kila wakatihawa, kuwa na mfumo mzuri wa kupata wachezaji chipukizi wengi, watakuwa wamelelewa katika mazingira ya mpira wa miguu.
  Pia kudumisha nidhamu ndani ya timu kwani wapo wachezaji waliotaka kuhiaribu timu kwa kuleta matatizo yaliyomo ndani ya klabu zao katika timu ya taifa, nashukuru nimejitahidi kuiondoa hali hiyo mapema kabla haijashika mizizi,” anasema Maximo.
  “Kwanza kabisa kitendo cha kujaza wachezaji wazee katika timu ya taifa ni tatizo, pia kutokuwa na vyuo vingi vya soka ni moja kati ya vitu vinavyochangia kuwepo hali hii.
  “Pia ushiriki wa manufaa katika michuano ya kimataifa ni moja kati ya matatizo yanayofanya tusiwe na wachezaji wengi wa kulipwa, ni ngumu kwa wakala kuja kufuata wachezaji wakati hatuna klabu inayoshiriki michuano mikubwa hata huyu mmoja tuliyenaye (Danny Mrwanda) alionekana akiwa na Stars huko Kuwait,” anasema Maximo.
  Anashangaa kwa nini Cape Verde yenye idadi ya watu milioni 2.5 imeweza kuwa na wachezaji 15 wa kulipwa huku Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 40 ina mchezaji mmoja tu wa kulipwa (hawausishi Mike Chuma na Renatus Njohole kutokana na madaraja wanayocheza).
  “Wachezaji kama Godfrey Bonny, Ivo Mapunda, Shedrack Nsajigwa na Salum Sued wana uwezo wa kucheza soka katika timu za madaraja ya chini huko Ulaya,” anasema Maximo.
  “Tunahitaji kujaza idadi kubwa ya wachezaji chipukizi katika kikosi cha Stars ili waweze kupata nafasi ya kucheza Ulaya kwani huko hawataki wazee kwenda kuzitumikia klabu zao.
  “Kuwa na vituo vingi vya kukuza wachezaji chipukizi itasaidia sambamba na klabu kubwa kuwapa nafasi vijana katika vikosi vyao vya kwanza,” anasema Maximo.
  Lakini Maximo anasema kikubwa ni kuwa na ushirikiano baina ya klabu na TFF ili ligi ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ianze ili kuwapata bora watakaoliwakilisha taifa siku za usoni kama ilivyokuwa kwa mchuano ya taifa ya vijana (Copa Coca Cola).
  “Mambo hayawezi kubadilika sana ni kama nilivyokueleza awali kuwa klabu lazima zitambue huwajibikaji wao katika kuimarisha timu ya taifa wanawajibu wa kuandaa vijana katika timu zao. Kwa upande wangu nitaendelea kuwatumia vyema chipukizi nitakaokuwa nawaona viwanjani, lakini nina uhakiak Tanzania itashiriki fainali za mataifa ya Afrika 2012 kutokana na matunda ya vijana wanaotokana na michuano ya Copa Coca Cola pia mipango ya kuwaweka kambini kila baada ya miezi miwili ni jambo la faraja kwetu, naamini tutafika,” anasema Maximo.
  Maximo anasema atawaita makocha wote kwa kuangalia madaraja waliyonayo ili apate mawazo na kubadilishana mambo mbalimbali yatakayoisaidia Stars kuwa nzuri zaidi.
  “Nitakaa na makocha wote wa Tanzania na kujadiliana kuhusu maendeleo ya Stars ninajua kuan vitu watapata kutoka kwangu nami kutoka kwao, pamoja tutafika tunakotaka..,” anasema Maximo.
  “Mbona hili suala lilishakwisha….sawa ngoja nikueleze kitu kimoja na sipendi kuzungumzia kuhusu mtu mmoja unajua hawa wachezaji wanapokuja katika kambi ya Stars huja na tabia zao kutoka klabu zao, sasa zipo ambazo hazifai kwa maendeleo ya soka na nyingine zinaimarisha.
  “Siwezi kuwa mjinga kuruhusu tabia mbovbu kutoka kwa wachezaji hao na nikibaini wanajihusisha na tabia mbovu sina samahani nawaondoa wote na sitowahitaji tena…huuu ni msimamo wangu tokea nimeanza kufundisha soka na si kwangu mimi tu,…kocha yeyote anayezingatia taaluma yake lazima awe mkali kuhusu tabia za wachezaji,” anasema Maximo.
  “Wananifurahisha sana sababu wao wanaheshimu matokeo ya aina moja tu…kushinda, tunakuwa pamoja pale tunapofanya vizuri lakini tukiteleza wanalaumu pasipo kuangalia kile tulichokifanya uwanjani.
  “Kwa upande mwingine naona wameonyesha tofauti kidogo kwani zamani hakukuwa na idadi ya mashabiki wengi wanaohudhuria mechi za Stars lakini sasa nawaona wengi wanakuja uwanjani.
  “Inapendeza kuoan familia nzima inakwenda uwanjani kuiangalia Stars ikicheza….huwa nawaona watoto wadogo na mama zao, wavulana na marafiki zao wa kike kwa kweli wananifurahisha, soka sasa ni mchezo wa furaha kwa watanzania tofauti na awali.
  “Lakini naona kama kuna wakati wanajisahau hasa pale walipotaka tuifunge Cameroon kwa idadi kubwa ya mabao huku wakisahahu hatua tuliyopo sasa wenzetu waliipitia miaka 20 iliyopita..mwihso wa yote wananifurahisha sana,” anasema Maximo.
  “Sikukataa kusaini kufundisha Stars nilichofanya ni kupunguza miaka niliyoombwa kuifundisha timu, sababu zipo mbili ambazo zilinilazimu kufanya hivyo.
  “Kwanza, nilikuwa naangalia mustakabali wangu hapa nilipoifikisha Stars palikuwa panatosha wacha nikatafute timu nyingine niweze kuiwekea misingi kama ilivyo kwa Tanzania.
  “Pia nilikuwa nataka mipango niliyoianzisha iendelezwe na kocha mwingine huu kwangu niliuona utaratibu mzuri kuliko mimi ‘kuzeekea’ hapa, najua akija mwingine ataendeleza niliachia mimi, msingi nimeshauweka tayari,” anasema Maximo.
  “Tayari nipo hapa kwa miaka miwili iliyopita lakini hata kama nikiondoka nitaisaidia Tanzania wakati wowote nitakapotakiwa kufanya hivyo bila gharama yoyote ile,” anasema Maximo.
  Awali TFF ilishauri kuongezwa kwa mkataba mpya wa Maximo ambao utakuwa wa miaka miwili, baada ya ule wa awali kuamliza Agosti mwaka huu.
  Wakati anawasili nchini Stars ilikuwa ipo nafasi ya 167 kwa ubora wa soka duniani lakini sasa ipo inashika namba 117 mbele ya Kuwait iliyo nafasi ya 119.
  “Japokuwa hatujapanda sana lakini naweza kusema mabadiliko yameonekana, pia kiwango cha uchezaji uwanjani ni tofauti na awali,” anasema Maximo.
  Hadi sasa Stars imeshatupwa katika kinyang’anyiro cha kuwamia ushiriki wa fainali za kombe la dunia na mataifa ya Afrika 2010 baada ya kucheza michezo mitano na kushinda mmoja, kufungwa miwili na kutoka sare miwili.
  Ina pointi tano ikiwa nyuma ya Cape Verde yenye pointi tisa na Cameroon inayoongoza kundi hilo la kwanza kwa kuwa na pointi 13. Timu zote zimecheza mechi tano kial moja.
  Lakini angalau ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mauritius Septemba 6 huko mjini Curepipe.
  “Tuliweza kuwafunga kutokana na jinsi walivyobadilika baada ya kuacha kutumia mtindo wao wa kila siku wa kukaba na kuanza kutushambulia, jambo lililowapanafasi washambuliaji wetu kufunga,” anasema Maximo akizungumzia ushindi huo. Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Mei 31, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
  “Kama nilivyokueleza hapo awali ili mchezaji acheze soka la kulipwa anahitaji vitu vingi vya msingi ikiwa pamoja na misingi ya soka, tupo katika hatua za kuimarish avitu hivyo sasa.
  Lakini kwa hapa nafikiri chipukizi wanaokuja kama wakian Tegete, Kigi ,Ngassa na Kingwande watakuwa na wajibu kufanya hivyo muda mfupi ujao lakini wachezaji kama wakina Bonny, Nsajigwa, Ivo na wale wenye umri mkubwa Stars wanaweza kucheza soka la kulipwa sasa lakini si katika ligi za juu,” anasema Maximo.
  “Katika maendeleo ya soka huwezi kujenga vitu vyote kwa wakati mmoja, Simba na Yanga zina wajibu wa kucheza mechi kati yao kila mara ili kuwaweka wachezaji katika hali ushindani kuliko ilivyo sasa….silazimishi ila ni kama ombi kwangu kutokana na tathmini yangu.
  Ni lazima tuwe na mfumo utakaomwezesha mchezaji kucheza mechi nyingi za ushindani zaidi ya ilivyo sasa, nimezizungumzia Simba na Yanga kwa kuwa ndiyo mhimili wa soka hapa nchini,” anasema Maximo.
  Anawashukuru makocha wa timu za mikaoni kwa kazi kubwa wanayofanya katika kusaka vipaji vya chipukizi amabao baadaye watakuwa hazina ya taifa.
  Lazima ziwepo ligi za vijana katika miji inayokua hii itarahisisha kupata wachezaji wengi wenye uwezo wa kucheza soka,” anasema Maximo.
  “Naziheshimu sana klabu hizi kwa kile wakifanyacho, lakini masuala mengine siwezi ku-comment hapa maana ni moja kati ya timu zenye upinazani na zilizobeba dhamana ya soak ya Tanzania,” anasema Maximo.

  VIPI AJAZE YANGA STARS?
  “Huwa sichagui mchezaji kwa misingi ya klabu yake mimi naangalia uwezo wa mchezaji hata kama watakuwa wote wazuri kutoka Mtibwa Sugar nitawabeba tu katika timu yangu.
  Hawa wachezaji wanaoonekana ni wa Yanga mimi nakataa kuhusu hilo sababu wote hawa nilianza kuwaita mimi Stars alafu baadae klabu hiyo ikawanunua.
  Naweza kusema Yanga ndiyo iliyochukua wachezaji Stars na si mimi kuchukau wachezaji katika klabu hiyo,
  Angalia Chuji (Athuman Idd) wakati namuita kwa mara ya kwanza alikuwa Simba lakini baadae akanunuliwa Yanga, huu ni mfano hai kuwa nilianza kuwaona mimi kwanza wachezaji hawa, kabla ya Yanga,” anasema Maximo.
  Anasema Abdi Kasim na Amir Maftah aliwaita wakiwa Mtibwa Sugar lakini baadae Yanga ikawasajili, Vivyo hivyo kwa Mrisho Ngassa, Vicent Barnabas ambao awali walikuwa Kagera Sugar. Ngassa alikuwapo katika orodha yake japokuwa alikuja kumia wakati ameshajiunga na Yanga.
  Wengine ni Godfrey Bonny aliyekuwa Prisons, Jerry Tegete aliyechukuliwa kutoka Makongo Sekondari, Kigi Makassy aliyetokea Mtibwa.
  Maximo anaye mke aitwaye Sabrina ambaye hata hivyo hajapata naye mtoto hata mmoja na hataki kufanya hivyo kwa sasa.
  “Nilikuwa na rafiki yangu mmoja ambaye ni kocha kama mimi wakati huo yeye alikuwa juu yangu (alikuwa anamsaidia) nilikuwa namuona jinsi anavyohangaika na watoto wake kila wakati huwezi kuwa na familia alafu unafanya kazi bara lingine kabisa utakuwa unahangaisha kichwa na kukosa umakini katika kile ukifundishacho,” anasema.
  “Anafanya kazi nzuri kimaslahi sasa hawezi kuacha kuja huku wakati mimi sitochukua muda mrefu hapa na katika maisha ya soka lakini nitakuwa na furaha ya kupat motto hivi karibuni,” anasema Maximo.
  “Hapo kabla mara baada ya kupata ajali ya gari niliwaza ni jnsi gain sitokuwa mbali na mchezo huu?...sababu nilipoteza uwezo wa kucheza katika hali ya ushindani..nikafikiria kuwa mwandishi wa habari za michezo lakini wakati huohuo yakaja mawazo ya kuwa kocha pia, mwishowe nikaangukia katika ukocha,” anasema Maximo.

  NUSURA AFUNDISHE SOUTHAMPTON NA ASTON VILLA ZA ENGLAND:
  “Kabla ya kuja Tanzania niliitwa kutembela klabu za Southampton na Aston Villa za England pia Grasgow Rangers ya Scotland, lakini hizo za England zilioyesha kuvutiwa nami lakini serikali ya Tanzania iliwawahi,” anasema huku akicheka.
  Huo ulikuwa mwaka 2006 aliitwa kuzitembelea na kujifunza mambo mbalimbali ya klabu hizo.
  “Kuna wakati huwa naona kama sistahili sifa hizo, maana unasifiwa mpaka inapiliza najiona si sahihi yake lakini sina la kufanya,” anasema Maximo.

  TANZANIA NA MAXIMO:
  “Naipenda sana Tanzania kwa sababu nimegundua raia wake wanapenda sana nchi yangu (Brazil) nachukizwa na tabia ya watu wanaoibeza nchi hii tena wengi wao ni Watanzania, nipo tayari kupigana nao ili kuitetea nchi hii yenye amani tele,” anasema Maximo.
  WASIFU:
  TAALUMA:
  Degree ya elimu ya viungoa liyoipata mwaka 1989 Universidade Federal do Rio de Janeiro – (UFRJ).
  Ana Degree ya Ukocha wa mpira wa miguu aliyoipata Universidade Federal do Rio de Janeiro – (UFRJ) mwaka 1992.
  Akiwa ni mwanachama wa wa Chama cha makocha wa mpira wa miguu Brazil (ABTF)aliwahi kuhudhuria kozi ya wakufunzi wa soka wa (FIFA) iliyofanyika huko Cayman mwaka 2000
  Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ mwaka 2006/2007/2008, alishiriki katika kampeni ya Stars ya kushiriki kombe la mataifa ya Afrika 2008.
  Mshauri wa ufundi na mratibu wa kozi mbalimbali za ukocha za ABTF mwaka 2005
  Mwaka 2003/2004 alikuwa Kocha Mkuu wa Livingston F. C ya Scotland iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu ya U-Skoch. Hii ilimfanya kuwa kocha wa kwanza kutoka Brazil kufundisha timu ya Ligi Kuu Uingereza
  Alikuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya visiwa vya Cayman mwaka 1999/2002, aliiongoza katika michuano ya kombe la
  Caribean mwaka 2001 na kupata mafanikio makubwa. Pia aliiongoza kuiongoza katika mbio za kuwania kucheza kombe la dunia 2002.
  Mwaka 1998Alifundisha soka katika kituo cha F.C. Union Berlin huko Rio de Janeiro kilichokuwa na mkataba wa kubadilishana taaluma na Ujerumani – Brazil Germany Interchange
  Mwaka 1996 alikuwa kocha mkuu wa timu ya kulipwa ya mji wa Rio de Janeiro. Timu hiyo ilishiriki michuano ya kimataifa ya Ugiriki (Athens), Ufaransa (Marselle) na Korea katiak mji wa Seul.
  Mwaka 1995 alitwaa ubingwa wa kombe la Mfalme akiwa Kocha Mkuu wa timu ya Al Ahli ya Jeddah, Saudi Arabia
  Mwaka 1994 aliifundisha timu ya taifa ya Qatar na kuiongoza katika kuwania ubingwa wa Asia, hapo alikuwa akiinoa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 iliyoshiriki kombe la Asia huko Indonesia chini ya Shirikisho la Soka Asia.
  Mwaka 1992 mpaka 1993 anakuwamo katika vikosi vya vijana vya timu ya taifa ya Brazil wenye umri chini ya miaka 17 na 20. Timu hizo zilikuwa zikishiriki michuano ya awali ya kombe la America Kusini.
  Mwaka 1994 aliifundisha Barra da Tijuca Futebol Clube ya Brazil ambayo ilikuja kuwa mabingwa wa Ligi daraja la kwanza.
  Mwaka 1992 alifundisha Mesquita Football Club iliyokuwa ikishiriki daraja la kwanza Brazil.
  Anachaguliwa kuwa mmoja wa watafuta wachezaji (Scout) wa Clube de Regatas Vasco da Gama mwaka 1990.
  Mwaka 1988 mpaka 1991 chini ya UFRJ anapata nafasi ya kuwa kocha mkuu katika mpango maalum wa kukuza vipaji huko Rio de Janeiro, Brazil uliokuwa ukijulikana kama
  Futebol Esperança Project
  International ‘Know-how’
  1982 kwenda mbele kocha msaidizi katika klabu mbalimbali za Brazil zikiwemo alizocheza awali.
  1976 kurudi nyuma- (Kama mchezaji) Aragatuba FC (Sao Paul), Vasco Da Gama na Botafogo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MJUE MAXIMO, KOCHA ALIYEREJESHA HADHI YA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top