• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 25, 2009

  KUMBE 'MINAZI' YA SENEGAL NDIO ILIILEWESHA STARS!

  Hizi ndio ndumba za Senegal


  na abdul mohammed, Abidjan
  VITENDO vya ushirikina vimeonekana kupewa umuhimu wa kipekee na timu ya Taifa ya Senegal ambayo Jumapili iliyopita iliilaza Taifa Stars kwa bao 1-0.
  Stars na Senegal zote ziko katika Kundi A kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) inayoendelea mjini hapa, timu nyingine katika kundi hilo ni Zambia na wenyeji Ivory Coast.
  Juzi, ikiwa ni siku moja baada ya Senegal kuifunga Tanzania baadhi ya wachezaji na viongozi wa Senegal walionekana wakiwa katika chumba kimoja kwenye hoteli ya Golf walikofikia Senegal na Stars huku vitendo vinavyoaminika kuwa ni vya kishirikina vikiendelea.
  Katika chumba hicho jezi na viatu vya wachezaji wa timu ya Taifa ya Senegal viliwekwa chini pamoja na nazi na vitu vingine huku mambo mengine yanayoaminika kuwa ni ya kishirikina yakiendelea.
  Wachezaji, kocha na watu wengine wanaoaminika kuwa ni viongozi au wamo katika msafara wa Senegal walionekana wakiingia na kutoka kwa zamu katika chumba hicho.
  Juhudi za kuzungumza na kocha mkuu wa Senegal, Joseph Koto ili kuelezea mambo mengine kuhusu timu yake pamoja na nini hasa kilichokuwa kikifanywa kutumia nazi, jezi na viatu vya wachezaji wake lakini haikuwezekana kumpata kocha huyo kwa haraka.
  Hata baada ya kukutana naye ghafla nje ya chumba hicho katika eneo la mapokezi, Koto alisema kwamba hana tatizo lakini angezungumza baadaye na waandishi wa habari.
  Hata hivyo Mkurugenzi wa Ufundi wa Senegal, Barnoun Ell alipoulizwa kuhusu ushirikina na soka la Senegal alisema kwamba kitu hicho kipo na ni cha kaaida wala hakuna ajabu.
  "Kwa Senegal hilo jambo lipo na hata wachezaji mnaowasikia wamefika Ulaya pia wanaamini sana katika suala hilo, si kitu kipya," alisema akionekana mwenye kujiamini n.
  Ell ambaye alionekana kuguswa na hoja hiyo huku akicheka alisema kwamba anaamini mambo ya ushirikina ambayo alipenda kutumia neno 'juju' hayapo Senegal pekee bali Afrika yote kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na mambo ya aina hiyo.
  Baadhi ya Watanzania walioandamana na Stars wamehusisha tukio hilo na kufungwa kwa Stars huku wengine wakiamini kwamba halina uhusiano wowote na ushindi wa Senegal kwa Stars.

  Kocha Ivory Coast tumbo joto kwa Stars

  na abdul mohammed, abidjan
  KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Ivory Coast, Kouadio Georges amesema kwamba anaiogopa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kwamba mechi ya leo dhidi ya timu hiyo itakuwa ngumu. Georges alisema kwamba hapo kabla alikuwa akiijua Stars kupitia katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) lakini kwa sasa timu hiyo imebadilika hususan baada ya kuiona ikicheza na Senegal.
  Stars itaumana na Ivory Coast leo katika michuano ya Kombe la Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) mechi ambayo inazikutanisha timu zilizopoteza mechi zao za kwanza za Kundi A. Stars ilifungwa na Senegal bao 1-0 wakati Ivory Coast ambao ndio wenyeji walifungwa mabao 3-0 na Zambia.
  Georges alisema kwamba aliiona mechi ya Stars na Senegal ilivyokuwa ngumu na Stars ilijitahidi kupigana licha ya kupoteza mechi hiyo. Akifafanua zaidi kuhusu ugumu wa mechi ya leo, Georges alisema kwamba unatokana na ukweli kwamba timu zote zimepoteza mechi za kwanza hivyo zinahitaji kuitumia vizuri mechi ya pili ili kuibuka na ushindi.
  "Wote tumetoka kushindwa, hivyo kila mmoja wetu atahitaji kushinda mechi ya kesho (leo) ili aweze kusonga mbele vinginevyo kushindwa ni kujiweka mahali pabaya, alisema.
  Katika mechi nyingine za Kundi B zilizochezwa juzi jioni, Zimbabwe iliilazimisha Ghana sare ya mabao 2-2 wakati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ililaza Libya kwa mabao 2-0. Akizungumzia mechi hizo kocha wa Stars, Marcio Maximo alisema kwamba Zimbabwe imeweza kuonyesha uhai na kuthibitisha kwamba ni moja ya timu bora licha ya baadhi ya watu kuidharau.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KUMBE 'MINAZI' YA SENEGAL NDIO ILIILEWESHA STARS! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top