• HABARI MPYA

  Sunday, July 07, 2024

  BEKİ WA KATI KUTOKA IVORY COAST AJIUNGA NA SIMBA SC


  KLABU ya Simba imemtambulisha beki wa kati, Chamou Karaboué (29) kuwa mchezaji wake mpya kuelekea msimu ujao kutokea klabu ya Racing Club d'Abidjan ya kwao Ivory Coast.
  Huyo anakuwa mchezaji wa 11 mpya Simba SC mabeki wengine, Mburkinabe Valentin Nouma (24) kutoka FC Saint-Éloi Lupopo ya DRC, wazawa, Abdulrazack Mohamed Hamza (21) kutoka SuperSport United ya Afrika Kusini na Lameck Elias Lawi (18) kutoka Coastal Union.
  Wengine ni kiungo wa ulinzi, Mnigeria, Augustine Okejepha (20) kutoka Rivers United ya kwao, Port Harcourt, kiungo mzawa Omary Abdallah Omary (23) kutoka Mashujaa FC ya Kigoma na winga Mzambia, Joshua Mutale (22) kutoka Power Dynamos ya kwao, Kitwe.
  Wapya wengine ni kiungo mshambuliaji, Débora Fernandes Mavambo (24) mwenye uraia pacha wa Kongo - Brazzaville na Angola kutoka Mutondo Stars ya Zambia na  washambuliaji Mganda, Steven Mukwala (24) kutoka Asante Kotoko ya Ghana na Muivory Coast, Jean Charles Ahoua (22) kutoka Stella Club d'Adjamé ya kwao, Abidjan na mzawa, Valentino Mashaka Kusengama (22) kutoka Geita Gold.
  Aidha, Simba SC imeleta Kocha Mkuu mpya, Fadluraghman ‘Fadlu’ Davids (43) raia wa Afrika Kusini kuwa Kocha wake mpya Mkuu, akichukua nafasi ya Mualgeria Abdelhak Benchika aliyeondoka April 28, mwaka huu.
  Fadlu Davids amekuja na safu yake nzima ya Wasaisizi, wote raia wenzake wa Afrika Kusini, Kocha Msaidizi, Darian Wilken, Kocha wa Makipa, Wayne Sandilands, Kocha wa Fitness, Riedoh Berdien na Mchambuzi, Mueez Kajee.
  Kikosi kinatarajiwa kuondoka Jumatatu kwenda mjini Ismailia nchini Misri kuweka kambi ya wiki tatu kujiandaa na msimu mpya. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BEKİ WA KATI KUTOKA IVORY COAST AJIUNGA NA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top