• HABARI MPYA

  Sunday, July 07, 2024

  VALENTIN ‘MBAVU YA KUSHOTO’ KUTOKA BURKİNA FASO MALI MPYA SIMBA SC


  KLABU ya Simba imemtambulisha beki wa kushoto wa Kimataifa wa Burkina Faso, Valentin Nouma (24) kutoka klabu ya FC Saint-Éloi Lupopo kuwa mchezaji wake mpya wa 10 kuelekea msimu ujao.
  Wachezaji wengine wapya Simba ni mabeki wazawa, Abdulrazack Mohamed Hamza (21) kutoka SuperSport United ya Afrika Kusini na Lameck Elias Lawi (18) kutoka Coastal Union.
  Wengine ni kiungo wa ulinzi, Mnigeria, Augustine Okejepha (20) kutoka Rivers United ya kwao, Port Harcourt, kiungo mzawa Omary Abdallah Omary (23) kutoka Mashujaa FC ya Kigoma na winga Mzambia, Joshua Mutale (22) kutoka Power Dynamos ya kwao, Kitwe.
  Wapya wengine ni kiungo mshambuliaji, Débora Fernandes Mavambo (24) mwenye uraia pacha wa Kongo - Brazzaville na Angola kutoka Mutondo Stars ya Zambia na  washambuliaji Mganda, Steven Mukwala (24) kutoka Asante Kotoko ya Ghana na Muivory Coast, Jean Charles Ahoua (22) kutoka Stella Club d'Adjamé ya kwao, Abidjan na mzawa, Valentino Mashaka Kusengama (22) kutoka Geita Gold.
  Aidha, Simba SC jana ilimtambulisha Kocha Mkuu mpya, Fadluraghman ‘Fadlu’ Davids (43) raia wa Afrika Kusini kuwa Kocha wake mpya Mkuu, akichukua nafasi ya Mualgeria Abdelhak Benchika aliyeondoka April 28, mwaka huu.
  Fadlu Davids amekuja na safu yake nzima ya Wasaisizi, wote raia wenzake wa Afrika Kusini, Kocha Msaidizi, Darian Wilken, Kocha wa Makipa, Wayne Sandilands, Kocha wa Fitness, Riedoh Berdien na Mchambuzi, Mueez Kajee.
  Kikosi kinatarajiwa kuondoka Jumatatu kwenda mjini Ismailia nchini Misri kuweka kambi ya wiki tatu kujiandaa na msimu mpya. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: VALENTIN ‘MBAVU YA KUSHOTO’ KUTOKA BURKİNA FASO MALI MPYA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top