• HABARI MPYA

  Saturday, July 06, 2024

  HISPANIA NA UFARANSA ZATINGA NUSU FAINALI EURO 2024


  TIMU za Hispania na Ufaransa zimefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya ‘Euro 2024’ baada ya kuzitoa Ujerumani na Ureno usiku wa jana.
  Walianza Hispania kuwang’oa wenyeji, Ujerumani kwa kuwachapa mabao 2-1 katika mchezo uliodumu kwa dakika 120 Uwanja wa Stuttgart Arena Jijini Stuttgart.
  Dakika 90 zilimalalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1, mshambuliaji wa RB Leipzig, Dani Olmo akianza kuifungia Hispania dakika ya 51 akimalizia pası ya kinda wa miaka 16 wa Barcelona, Lamine Yamal.
  Lakini kiungo wa Bayer Leverkusen, 
  Florian Wirtz akaisawazishia Ujerumani dakika ya 89 akimalizia kazi nzuri ya nyota wa Bayern Munich, Joshua Kimmich.
  Shujaa wa Hispania alikuwa ni kiungo wa Real Sociedad, Mikel Merino aliyefunga bao la ushindi dakika ya 119 baada ya kazi nzuri ya Dani Olmo.
  Hispania ilimaliza pungufu baada ya beki wa kulia wa Real Madrid, Dani Carvajal kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 120.
  Nayo Ufaransa ililazimika kusubiri hadi mikwaju ya penaltı ili kuitoa Ureno kwa penaltı 5-3 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 120 Uwanja wa Volksparkstadion Jijini Hamburg.
  Waliofunga penalti za Ufaransa ni Ousmane Dembélé, Youssouf Fofana, Jules Koundé, Bradley Barcola na Théo Hernández, wakati za Ureno waliofunga ni Cristiano Ronaldo, Bernardo Silva na Nuno Mendes huku João Félix pekee akikosa.
  Mechi za mwisho za Robo Fainali zinachezwa leo, England na Uswisi Saa 1:00 usiku na Uholanzi na Uturuki Saa 4:00 usiku.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HISPANIA NA UFARANSA ZATINGA NUSU FAINALI EURO 2024 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top