• HABARI MPYA

  Tuesday, July 09, 2024

  SADIO KANOUTE SI MCHEZAJI WA SIMBA SC TENA


  KLABU ya Simba imeachana na kiungo wa Kimataifa wa Mali, Sadio Kanoute (27) baada ya miaka mitatu tangu awasili mwaka 2021 kutoka Stade Malien ya kwao, Bamako.
  Huyo anakuwa mchezaji wa saba kuachwa Simba baada ya mabeki, Mkongo Henock Inonga Baka ‘Varane’, Kennedy Wilson Juma, viungo, Mrundi Saido Ntibanzokiza, Luis Jose Miquissone wa Msumbiji na washambuliaji John Raphael Bocco na Shaaban Iddi Chilunda.
  Aidha, Simba imesajili wachezaji wapya 12, ambao ni mabeki, Mburkinabe Valentin Nouma (24) kutoka FC Saint-Éloi Lupopo ya DRC, wazawa, Abdulrazack Mohamed Hamza (21) kutoka SuperSport United ya Afrika Kusini na Lameck Elias Lawi (18) kutoka Coastal Union.
  Wengine ni viungo, Mnigeria, Augustine Okejepha (20) kutoka Rivers United ya kwao, Port Harcourt, Omary Abdallah Omary (23) kutoka Mashujaa FC ya Kigoma, Yusuph Ally Kagoma (28) kutoka Singida Big Stars, Mzambia, Joshua Mutale (22) kutoka Power Dynamos ya kwao, Kitwe, Débora Fernandes Mavambo (24) mwenye uraia pacha wa Kongo - Brazzaville na Angola kutoka Mutondo Stars ya Zambia.
  Kuna washambuliaji pia, Mganda, Steven Mukwala (24) kutoka Asante Kotoko ya Ghana na Muivory Coast, Jean Charles Ahoua (22) kutoka Stella Club d'Adjamé ya kwao, Abidjan na mzawa, Valentino Mashaka Kusengama (22) kutoka Geita Gold.
  Simba SC pia imeleta Kocha Mkuu mpya, Fadluraghman ‘Fadlu’ Davids (43) raia wa Afrika Kusini kuwa Kocha wake mpya Mkuu, akichukua nafasi ya Mualgeria Abdelhak Benchika aliyeondoka April 28, mwaka huu.
  Fadlu Davids amekuja na safu yake nzima ya Wasaisizi, wote raia wenzake wa Afrika Kusini, Kocha Msaidizi, Darian Wilken, Kocha wa Makipa, Wayne Sandilands, Kocha wa Fitness, Riedoh Berdien na Mchambuzi, Mueez Kajee.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SADIO KANOUTE SI MCHEZAJI WA SIMBA SC TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top