• HABARI MPYA

  Friday, July 05, 2024

  MSAUZI MUIBUA VIPAJI NDIYE KOCHA MPYA SIMBA SC


  KLABU ya Simba imemtambulisha Fadluraghman ‘Fadlu’ Davids (43) raia wa Afrika Kusini kuwa Kocha wake mpya Mkuu, akichukua nafasi ya Mualgeria Abdelhak Benchika aliyeondoka April 28, mwaka huu.
  Fadlu Davids ni mshambuliaji wa zamani wa klabu za Mother City, Manning Rangers, Engen Santos, Chernomorets Burgas, Avendale Athletico, Vasco da Gama, HP Silver Stars na Maritzburg United zote za kwao.
  Baada ya kustaafu soka mwaka 2012 akawa Msaidizi wa Kocha Mjerumani, Ernst Middendorp klabu ya Maritzburg United. 
  Aliteuliwa kuwa Kocha wa amuda wa Martizburg United mwaka 2016 kufuatia Middendorp kuondoka na baadaye, Julai 2016 akapewa Ukocha Mkuu na huo ukawa mwanzo wa safari yake ya Ukocha akafundisha pia Orlando Pirates.
  Sifa kubwa ya Davids ni kuibua vipaji vya wachezaji wadogo wakiwemo Siphesihle Ndlovu‚ Bandile Shandu na Mlondi Dlamini, ambao wote walianza kama waokota mipira maarufu kama ‘Ball Boys’ Maritzburg United.
  Tayari Simba SC imemtambulisha wachezaji sita wapya, wakiwemo mabeki wazawa, Abdulrazack Mohamed Hamza (21) kutoka SuperSport United ya Afrika Kusini na Lameck Elias Lawi (18) kutoka Coastal Union.
  Wengine ni winga Mzambia, Joshua Mutale (22) kutoka Power Dynamos ya kwao, Kitwe na washambuliaji Mganda, Steven Mukwala (24) kutoka Asante Kotoko ya Ghana na Muivory Coast, Jean Charles Ahoua (22) kutoka Stella Club d'Adjamé ya kwao, Abidjan na mzawa, Valentino Mashaka Kusengama (22) kutoka Geita Gold.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MSAUZI MUIBUA VIPAJI NDIYE KOCHA MPYA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top