• HABARI MPYA

  Wednesday, August 09, 2017

  MAYAY AZINDUA KAMPENI AKISINDIKIZWA NA MAGWIJI MOGELLA NA KHALID ABEID

  NA Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  MGOMBEA Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika uchaguzi wa Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma, Ally Mayay Tembele amezindua kampeni zake leo kwa kaulimbiu ya "Turudishieni Mpira Wetu" akisindikizwa na wachezaji wenzake wa zamani wa klabu mbalimbali nchini.
  Nahodha huyo wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars aliyechezea pia Milambo ya Tabora na CDA ya Dodoma, amezindua kampeni zake katika mkutano na Waandishi wa Habari ukumbi wa hoteli ya Lamada katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
  Miongoni mwa waliomsindikiza Mayay ni wachezaji wa zamani wa Simba, kiungo Khalid Abeid na mshambuliaji Zamoyoni Mogella na wachezaji wa zamani wa Yanga, beki Lawerence Mwalusako na Mohammed 'Adolph' Rishard.   
  Hotuba kamili ya Mayay hii hapa;
  Ally Mayay (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo. Wengine pichani ni Zamoyoni Mogella (katikati) na Lawrence Mwalusako  
  Ally Mayay (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari. Kulia ni Khalid Abeid
  "1. UTANGULIZI; Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia wote afya njema na kutuwezesha kufika hapa salama.
  Niwashukuru kwa dhati kabisa waandishi wote mliojitokeza hapa leo.
  Na nikiwa kama mgombea, na kwa matiki hiyo mwenye mkutano huu, nichukue fursa hii kuwakaribisha wote mliofika hapa leo.
  2. Utambulisho
  Kama wengi mnavyonifahamu, mimi naitwa Ally Mayay Tembele mchezaji wa zamani na elimu yangu ya juu ni Shahada ya Uzamili, nikibobea katika masuala ya Masoko (Marketing).
  Katika mpira wa miguu, nimefanikiwa kucheza kuanzia ngazi za chini kabisa  ya soka la nchi hii, yaani Ligi Daraja la Nne  hadi  ngazi ya juu kabisa ya Ligi Kuu kwa sasa ikiitwa Premier League
  Aidha, nje ya mfumo rasmi wa soka nimeshiriki mashindano ya mpira wa miguu kuanzia shule za msingi (UMITASHUMTA), Sekondari (UMISSETA), Vyuoni (SHIMIVUTA) na hatimaye kazini (SHIMIWI). 
  Hivyo, nadiriki kusema kuwa nimeuishi mpira wa nchi nii na ninafahamu changamoto zilizopo ndani ya uwanja, ndani ya vyumba vya kubadilishia jezi vya wachezaji (dressing room), zilizopo majukwaani kwa washabiki na zile zilizo katika vikao vya bodi za uongozi kwa kuwa nimepita katika maeneo yote na nimekuwa nikijifunza kila kukicha. 
  Kwa  zaidi ya miaka kumi sasa nimekuwa nikifanya kazi na vyombo mbalimbali vya habari kama Televisheni, Redio na magazeti zinazohusiana na mchezo wa soka ikiwemo uandishi wa makala za michezo katika magazeti ya michezo pamoja na uchambuzi wa mechi katika televisheni na redio.
  Katika eneo la uongozi, nimekuwa nahodha tangu mwaka 1987 nilipokuwa Darasa la Nne, nimekuwa nahodha wa timu ya Shule yangu ya Msingi katika mashindano ya UMISHUMTA mkoa wa Kigoma.  Aidha  nimekuwa pia nahodha katika timu ya  CDA, Yanga na Timu ya Taifa. Pia nimekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga na baadae Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga.
  Aidha, nimekuwa Mjumbe wa Kamati ya Kuendeleza Soka la Vijana ya TFF ,lakini pia nimekuwa  Waziri wa michezo katika serikali  ya Wanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE) na baadae kuwa Rais wa Serikali ya wanafunzi. Pia niliteuliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kuwa Mjumbe wa Bodi  ya Uongozi ya Chuo cha CBE  kwa miaka mitatu.
  Kwa sasa ni Mjumbe wa Chama cha Wachezaji SPUTANZA nikikiwakilisha chama kwenye Mkutano Mkuu wa TFF kwa mwaka wa nne sasa.
  3. Kwa nini nagombea?
  Kama nilivyoeleza awali, nimeuishi mpira wa nchi hii na nimeziishi changamoto zilizopo katika  mpira wa miguu kwa ujumla, hivyo;
  3.1. Cha kwanza kilichonivuta kugombea ni kutumia uzoefu wangu na uelewa wangu wa changamoto zilizopo katika mpira  na kutengenza utaratibu bora wa kushirikiana katika kuzitatua kwa pamoja kulingana na mahitaji ya soka la karne hii ya 21. Changamoto hizi zilikuwepo na bado zinaendelea kuwepo hadi leo licha ya mazingira na mahitaji ya  soka kubadilika kwa kiwango kikubwa kutokana maendeleo ya sayansi na teknolojia  na kuwepo kwa utayari mkubwa wa wadhamini. Hivyo nagombea ili kutatua changamoto hizi kwa kutumia uzoefu nilionao katika sekta hii.
  3.2. Cha pili, ni kuona jinsi ambavyo mpira wetu umekuwa ukiendeshwa bila ya kuwa na Dira ya Maendeleo yenye kuonyesha wapi viongozi waliotuomba kura wanaupeleka mpira wetu na lini wanatuahidi kuufikisha huko? Hivyo mahitaji ya kuandaa dira ya maendeleo ya mchezo ni kitu kinachihitajika sana kwa sasa. 
  3.3. Cha tatu na cha mwisho, ni kuwa mimi nina mapenzi ya dhati ya mpira na maisha yangu ni kielelezo cha mapenzi hayo hivyo, nimeona sasa ni wakati muafaka wa kugombea nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu kwenye kuuinua mpira wa nchi hii ambao wengi tunaupenda.
  4. Mipango yangu
  4.1. Kuanzisha Mkakati wa maendeleo ya soka la Tanzania (Football Development Vision)
  Kama nitapata ridhaa, nitaanzisha mara moja mchakato shirikishi kutengeneza Dira ya Maendeleo ya mpira wa miguu nchini kama ilivyo kwa taifa letu ambapo tuna Dira ya Maendeleo ya Taifa iliyoanzishwa mwaka 1994 na kuibuliwa rasmi mwaka 1999 ikitupa mwongozo wa nini cha kufanya kufikia malengo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa itakapofika mwaka 2025.
  Dira hii itakuwa na malengo ya muda mrefu, wa kati na mfupi na nitapenda uongozi wangu upimwe kutokana na kufikiwa au kutofikiwa kwa malengo hayo ndani ya vipindi tutakavyokubaliana na wadau
  Dira hii itakuwa na vitu kama maendeleo ya mpira wa vijana na wanawake, ujenzi wa miundombinu, unoreshaji wa ushiriki wa timu zetu kwenye mashindano ya kimataifa, kujenga uwezo wa walimu, na kadhalika
  4.2. Urasimishaji wa Mpira wa Miguu (Formalisation of Tanzania Football)
  Pamoja na mpira wa miguu kutoa ajira nyingi kwa wachezaji, makocha, madaktari na watoa huduma mbalimbali zinazohusiana na mchezo wa soka  hivyo  kuchangia katika pato la Taifa, lakini  bado sekta hii haijarasimishwa  na hatimaye kupelekea kukosa fursa  nyingi ambazo zingepatikana kama sekta hii ingekuwa rasmi. 
  Hili litakuwa ni miongoni mwa majukumu yangu ya awali kwa kushirikiana na serikali kurasimisha sekta hii muhimu na sekta kufaidika kutoka na urasimishaji huo.
  4.3. Kujenga na kuboresha miundombinu ya mpira wa miguu
  Kutokana na gharama kubwa za ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya kuendeleza mpira wa miguu ikiwemo viwanja, gyms, shule (Football Academies), na kadhalika; Mkakati wangu kwenye eneo hili utalenga maendeo manne:
  i. Kuishawishi serikali kuandaa mpango wa pamoja (Joint Strategy) wa uendelezaji na ujengaji wa miundombinu hii;
  ii. Kushirikiana na mataifa rafiki yenye uwezo wa kusaidia; na
  iii. Kushirikiana kwa karibu zaidi na FIFA ili izidishe mchango wake kwenye suala hili ambalo kwa sasa limeishia kwenye uwekaji wa nyasi bandia.
  iv. Kuhakikisha uwepo wa maeneo ya wazi katika maeneo ya makazi mapya kwa kushirikisha vyama vya soka vya mikoa, wilaya na halmashauri za miji ili kuwapa watoto fursa ya kucheza mpira katika maeneo yao.
  4.4. Uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu
  Mafanikio yoyote ninayoyatazamia kwenye uongozi  yatatokana na uongozi  wangu utakaoongoza kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ambayo ni :Uwazi, uwajibikaji,Utawala wa sheria, ushirikishwaji,usawa, ufanisi na tija, mwitikio, maridhiano na uadilifu.
  Katika eneo la uwazi , mapato yote yanayoingia katika shirikisho yatawekwa wazi kwa wadau ikiwemo fedha za msaada kutoka FIFA na CAF kama kanuni za fedha za Shirikisho zinavyosema.
  Katika eneo la ushirikishwaji, tutaangalia namna bora ya kuwashirikisha wadau kama wadhamini na washabiki kuwemo  katika sehemu za maamuzi ili kuweza kulinda maslahi yao moja kwa moja.
  Katika eneo la ushauri wa kitaalamu, tutakuwa na Bodi ya ushauri itakayokuwa na wataalamu wenye weledi mtambuka kwa ajili ya kuishauri kamati ya utendaji katika maswala ya kitaalam kabla ya kamati ya utendaji kufanya maamuzi .
  Katika eneo la ushirikishwaji , tutaanzisha utaratibu mpya wa kushirikisha vyama vya mikoa na kugawa majukumu ya kutekeleza kutokana na makubaliano tutakayokubaliana katika mikutano.
  Pia tutaanzisha rasmi mfumo wa mawasiliano wa kielektroniki ambao mahsusi kwa sekretarieti utakaotumiwa na makatibu wa vyama vya mikoa kuwasiliana moja kwa moja na Katibu Mkuu  katika maswala ya utendaji wa shughuli za kila siku. Mfumo huu utawezehsa makatibu wote kupata taarifa za utendaji za makatibu wenzao katika mikoa yote.
  4.5. Uendelezaji wa Soka la Wanawake na la Ufukweni
  Ukizingatia kuwa mafanikio kimataifa tuliyopata japo kidogo kwenye soka la wanawake licha ya kutokuwa na ligi rasmi hadi mwaka huu 2017, soka la wanawake linaonyesha  kuwa na hazina hazina kubwa ya vipaji vya soka kwa wanawake. Nitashirikiana na TWFA kuhamasisha wanawake /vijana nchini kucheza na kuunga mkono soka la wanawake kwani uwezo wa kushiriki michuano ya kimataifa kwa soka la wanawake umekwishaonekana. 
  Aidha Ligi ya wanawake iliyoanzisha hivi karibuni, tutahakikisha inaendelea kwa kuongeza idadi ya timu na kupata wafadhili (sponsors) watakaosaidia katika uendeshaji wa ligi hiyo ili isambae nchi nzima.
  Katika eneo la ufundi , tutaandaa program maalumu ya kuongeza  idadi ya waamuzi, makocha na madaktari wa michezo  wanawake ili kuwezesha soka la wanawake kukua zaidi nchini.
  Soka la ufukweni ni mchezo mpya kwa watanzania walio wengi hivyo inahitaji nguvu ya ziada kutumika katika kuutangaza mchezo huu hasa ukizingatia kuwa nchi yetu ni moja kati ya nchi zenye pwani ndefu  kwenye bahari ya hindi, inayokadiriwa kuwa na urefu wa km 800 hivyo kutokuwa na changamoto ya kutafuta viwanja vya mazoezi kama ilivyo kwenye baadhi ya nchi ambazo hazina pwani. 
  Tutahamasisha wadau kushiriki katika soka la ufukweni ili kutumia vema fursa hii na kuweza kufikia mafanikio katika soka la ufukweni.
  4.6. Mkakati wa Maandalizi ya Fainali za CUF za U-17 mwaka 2019 hapa Tanzania
  Mwaka 2015 walichaguliwa vijana wenye umri chini ya miaka 13 na kutengeneza kikosi cha vijana kwa ajili ya kuandaa timu ya U-17 ya mwaka 2019. Vijana hao wapo katika kituo cha Alliance jijini Mwanza wakiendelea na masomo pamoja huku wakipata mafunzo ya mpira wa miguu katika kituo hicho. Kuwaandalia programu maalum ya kuwaweka pamoja ikiwemo mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 mwezi disemba 2017 na mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 16 mwaka 2018 kabla ya kufika mwaka 2019.
  Katika mashindano hayo vijana watakaoonekana wanafaa watajumuishwa katika kikosi hicho na kuendelea na program itayopangwa na benchi la ufundi.
  Mkakati wa fedha za kuendesha program hii ya miaka mitatu utasimamiwa na Shirikisho kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine ambapo uwazi katika mahitaji na matumizi ya fedha  ndio utakuwa  msingi wa uendeshaji wa program hii.
  Tathmini ya mahitaji ya miundombinu (viwanja vya mechi na mazoezi ) kwa ajili ya fainali za U-17 za mwaka 2019 itafanyika chini ya uratibu wa kamati ya ufundi na kamati ya mashindano  pamoja na serikali ili kujua mahitaji halisi ya viwanja na ubora utakaokidhi  mahitaji ya CAF.
  Mashindano haya tunatakiwa kuyatumia sio kutangaza tu wachezaji wetu bali hata kutangaza vivutio vingine vilivyopo nchini  kwa kuwa tunatarajia kuwa na mataifa nane (8) kutoka katika bara la Afrika na vyombo vya habari vikubwa vyote vitaripoti mashindano haya hivyo ni fursa pia kwa makampuni na  wafanyabiashara wa Tanzania kutangaza bidhaa zao. 
  5. Kwa nini nataka mpira urejeshwe kwa wenyewe (Bring back our Ball)
  5.1. Naamini kwa dhati kabisa  kuwa Watanzania wapenzi wa soka wana mapenzi ya dhati kabisa na mchezo huu na wamekuwa na kiu ya muda mrefu ya kutaka mafanikio katika mchezo huu lakini bahati mbaya mafanikio hayo yamekuwa hayapatikani kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za kiuongozi . Kurejesha soka kwa wenyewe ni kuweka viongozi wanaothibitika kuwa na mapenzi ya dhati na mchezo huu ambao wataweza kutoa matumaini ya mafanikio kwa watanzania kutoka an mipango yao . 
  5.2. Kutokana na hilo ndio maana nikaona sasa kampeni yangu iongozwe za dhamira ya kuurejesha mpira kwa walio na uchungu na mpira wa nchi hii ambao ni wadau wa soka tukiwemo tuliowahi kuucheza.Ahsanteni kwa kunisikiliza, nakaribisha maswali,"mwisho wa hotuba hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAYAY AZINDUA KAMPENI AKISINDIKIZWA NA MAGWIJI MOGELLA NA KHALID ABEID Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top