• HABARI MPYA

  Monday, August 07, 2017

  'GWIJI' WA SOKA MWANZA, IBRAHIM MAGONGO KUZIKWA KESHO

  Na Hilal Riyami, MWANZA
  MCHEZAJI maarufu wa zamani mkoani Mwanza, Ibrahim Hamisi Magongo aliyefariki dunia mchana wa leo, anatarajiwa kuzikwa kesho.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online, ndugu wa marehemu, Khalfan Ngassa amesema kwamba mazishi yatafanyika kesho katika makaburi ya Kirumba, Mwanza.
  Kihistoria, Ibrahim Hamis Magongo aliibukia timu ya Toto Africans mwaka 1976 kabla ya kuhamia kwa mahasimu wa Jiji jilo, Pamba mwaka 1979.
  Lakini pia, akiwa mwanafunzi wa sekondari ya Lake mjini Mwanza, Magongo na aling’ara katika michuano ya Shule za Sekondari (UMISETA) na kuchaguliwa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20.
  Kikosi hicho kilichokuwa na wachezaji wengine kama George ‘Best’ Kulagwa, Mohammed ‘Adolf’ Rishard, Nicodemus Njohole, Abbas Kuka na wengineo kilikwenda kucheza na Zambia mwaka 1978.
  Katika kikosi cha Pamba kilichokuwa na nyota wengine kama Joram Mwakatika, James Ng'ong'a, Khalid Bitebo ‘Zembwela’, Abu Juma, Amri Ibrahim na wengineo – Magongo alikuwa anacheza kama beki wa kati, namba nne au tano.
  Alistaafu soka mwaka 1987 na baadaye akawa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Mwanza (MZFA) chini ya uongozi wa Jackson Songora.
  Marehemu Magongo, ambaye ndugu yake, Abbas Magongo alicheza Gor Mahia ya Kenya kabla ya naye kukumbwa na umauti, alianza kusumbuliwa na maradhi ya moyo na ugonjwa wa mapafu kujaa maji kuanzia mwishoni mwa mwaka 2014 kabla ya kupata ahueni mwak 201.
  Lakini hali yake ikabadilika tena mapema Machi mwaka huu hadi kulazwa katika hospitali ya Sekou Toure, lakini akapata nafuu na kuruhusiwa hadi akahudhuria mchezo wa Tanzania na Rwanda Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mwezi uliopita kuwania tikerti ya CHAN.
  Alasiri ya leo Mwenyezi Mungu amekichukua kiumbe chake, Ibrahim Magongo na kuwaachia simanzi wana Mwanza na familia ya wapenda soka kwa ujumla. Mungu ampumzishe kwa amani marehemu. Amin. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: 'GWIJI' WA SOKA MWANZA, IBRAHIM MAGONGO KUZIKWA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top