• HABARI MPYA

  Monday, August 07, 2017

  NIYONZIMA, GYAN WAWASILI KUANZA KAZI SIMBA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MFUNGAJI bora wa Ligi Kuu ya Ghana, Nicholas Gyan na Nahodha wa Rwanda, Haruna Niyonzima wamewasili Alfajiri hii kukamilisha usajili wa kikosi cha Simba kwa msimu wa 2017- 2018.   
  Lakini majina yao tayari yalikwishatumwa kwenye usajili wa Wekundu hao wa Msimbazi tangu jana mapema tu kabla ya dirisha la usajili nchini kufungwa.
  Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Iddi Kajuna alikuwepo Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mjini Dar es Salaam Alfajiri hii pamoja na viongozi wengine wa klabu, akiwemo Juma Ndambile kuwapokea wachezaji hao pamoja na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi.
  Haruna Niyonzima akiwa amembeba mwanawe baada yaa kupokewa na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Iddi Kajuna (kushoto

  Haruna Niyonzima akiwa na kiongozi waa Simba, Juma Ndambile baada ya kuwasili JNIA
  Nicholas Gyan akikumbatiana na kiongozi wa Simba, JUma Ndsambile baada ya kuwasili JNIA
  Na watatu hao wanakwenda kuungana na Method Mwanjali kutoka Zimbabwe, Juuko Murshid, kutoka Uganda, James Kotei kutoka Ghana na Laudit Mavugo kutoka Burundi kukamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni Simba kwa mujibu wa kanuni, baada ya kuachwa kwa kipa Mghana, Daniel Agyei, beki Mkongo Janvier Besala Bokungu na mshambuliaji Muivory Coast, Frederick Blagnon.
  Wakati Gyan anatokea klabu ya Ebusua Dwarfs ya kwao, Ghana, Niyonzima anatokea kwa mahasimu wa jadi, Yanga aliojiunga nao mwaka 2011, akitokea APR ya kwao, Rwanda aliyoanza kuichezea mwaka 2007 baada ya kujiunga nayo kutoka Rayon Sport iliyomsajili mwaka 2006 kutoka Etincelles iliyomuibua kisoka nchini humo.
  Baada ya misimu sita mizuri akiwa na Yanga, Haruna anabadili upepo kwa kuhamia kwa mahasimu wao jadi, Simba, timu ambayo mashabiki wa timu yake wa zamani walikuwa wakimlalamikia kuwa na mapenzi nayo na kucheza chini ya kiwango kila watani hao wa jadi wanapokutana.
  Haruna na Gyan pamoja na wachezaji wote wengine wa Simba watatambulishwa Jumanne katika tamasha maalum la klabu hiyo la kila mwaka lijulikanalo kama Simba Day ambalo litahusisha pia mchezo wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa Rwanda, Rayon Sport Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NIYONZIMA, GYAN WAWASILI KUANZA KAZI SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top